Lakes yamtolea macho Robinson wa Knicks
Muktasari:
- Msimu wa mapumziko ukiwa unakaribia na timu kadhaa zikitafuta kuimarisha vikosi vyao, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ameibuka kuwa mmoja wa majina yanayozungumzwa zaidi katika soko la usajili na kubadilishana wachezaji.
NEW YORK, MAREKANI: WAKATI New York Knicks wakiendelea kuzingatia kampeni yao ya Fainali za NBA, hawawezi kupuuza kelele zinazozidi kuongezeka kuhusu mustakabali wa nyota wake Mitchell Robinson.
Msimu wa mapumziko ukiwa unakaribia na timu kadhaa zikitafuta kuimarisha vikosi vyao, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ameibuka kuwa mmoja wa majina yanayozungumzwa zaidi katika soko la usajili na kubadilishana wachezaji.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari za NBA, Jake Fischer, timu ya Los Angeles Lakers imejitokeza kama moja ya maeneo yanayowezekana kwa Robinson kutua.
Vyanzo vya ligi vinaeleza kuwa Lakers ni miongoni mwa timu kadhaa zinazofuatilia kwa karibu hali yake huku akielekea kuingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake wa miaka minne wenye thamani ya dola60 milioni.
Timu nyingine pia zinamwania
Sacramento Kings wamekuwa wakihusishwa na Robinson kwa muda mrefu. Meneja Mkuu wa Kings, Scott Perry, ambaye alimchagua Robinson wakati akiwa Knicks, bado anaamini uwezo wake, nguvu zake za kimwili na mchango wake ndani ya uwanja.
Timu nyingine zinazoripotiwa kufuatilia maendeleo yake ni pamoja na Chicago Bulls, Charlotte Hornets na Toronto Raptors, ambazo zote zinatafuta kuimarisha nafasi ya center kabla ya msimu mpya kuanza.
Knicks wanakabiliwa na uamuzi magumu ya kifedha
Kwa upande wa Knicks, hali si rahisi. Huku Karl-Anthony Towns akiwa amejiimarisha kama center wa kwanza wa timu na huku masharti ya kifedha ya NBA yakiongeza presha ya matumizi, kuendelea kumbakisha Robinson kunaweza kuwa gharama kubwa.
Hata hivyo, uwezo wake wa kulinda, kuchukua rebound za mashambulizi na kubadilisha mwelekeo wa mashuti ya wapinzani unamfanya kuwa mchezaji muhimu anapokuwa fiti.
Robinson amekuwa nguzo muhimu kwa Knicks, hasa katika upande wa ulinzi. Uwepo wake umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu katika misimu ya hivi karibuni, ikiwemo safari yao ya sasa ya kufika Fainali za NBA dhidi ya San Antonio Spurs.
Mustakabali wake bado haujulikani
Kwa sasa, Robinson ameweka nguvu zake zote katika kusaidia Knicks kutafuta ubingwa wa NBA. Hata hivyo, mustakabali wake baada ya msimu huu unatarajiwa kuwa moja ya simulizi kubwa zaidi katika kipindi cha mapumziko.
Iwapo ataendelea kubaki New York au ataamua kujaribu soko la usajili, uwezo wake mkubwa wa ulinzi na rebounding utamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotafutwa zaidi. Kwa sasa, Lakers pamoja na timu nyingine za Western Conference zinaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya hali hiyo zikisubiri kuona kitakachotokea mara tu msimu utakapomalizika.