Mbappe mfungaji bora Ufaransa, akiwapiku Giroud, Pele, Messi
Muktasari:
- Mabao mawili aliyofunga nyota huyo katika ushindi wa timu hiyo wa 3-1, dhidi ya Senegal katika mechi ya Kombe la Dunia kundi I, yamemfanya kufikisha 58 na kuivuka rasmi rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Olivier Giroud aliyefunga mabao 57.
NEW JERSEY, MAREKANI: MSHAMBULIAJI wa Ufaransa, Kylian Mbappe ameandika rekodi mpya leo baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa timu hiyo wa 3-1, dhidi ya Senegal na kuibuka mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo.
Mabao mawili aliyofunga nyota huyo katika ushindi wa timu hiyo wa 3-1, dhidi ya Senegal katika mechi ya Kombe la Dunia kundi I, yamemfanya kufikisha 58 na kuivuka rasmi rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Olivier Giroud aliyefunga mabao 57.
Katika mechi ya leo iliyopigwa East Rutherford, New Jersey, Marekani, Mbappe alifunga mabao hayo mawili na moja lilifungwa na Bradley Barcola huku la kufuatia machozi kwa Senegal likifungwa na Ibrahim Mbaye.
Mbappe mwenye umri wa miaka 27, analingana na gwiji wa Ujerumani Magharibi Gerd Müller kwa mabao 14 ya Kombe la Dunia baada ya kufunga mabao hayo mawili, akishika nafasi ya tatu kwenye orodha ya muda wote nyuma ya Miroslav Klose wa Ujerumani aliyefunga 16 na Ronaldo wa timu ya taifa ya Brazil mwenye 15.
Nyota huyo wa Real Madrid alianza mechi hiyo dhidi ya Senegal akiwa nafasi ya sita kwenye orodha hiyo sambamba na Pele wa Brazil mwenye mabao 12, lakini kiwango chake bora alichokionyesha kwenye Uwanja wa MetLife kimewapita Pele aliyefunga 12 na Lionel Messi wa Argentina na gwiji wa Ufaransa, Just Fontaine waliofunga 13, kila mmoja na kuingia katika orodha ya wafungaji watatu bora.
Mabao yake hayo mawili yamefanya afikishe mabao 58 na kuibuka mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa, akimpita aliyekuwa mshambuliaji wa Arsenal, Chelsea na AC Milan, Olivier Giroud aliyefunga 57.
Kwa sasa Mbappe amefunga katika Kombe la Dunia mara tatu mfululizo, akiwa ni mchezaji wa pili, baada ya Geoff Hurst wa England mwaka 1966, kufunga mabao matatu (Hat-Trick) katika fainali ya Kombe la Dunia.
Kwa upande wa Mbappe alifunga Hat-Trick katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia kati ya Ufaransa dhidi ya Argentina iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lusail, Qatar, Desemba 18, 2022.
Katika mechi hiyo, licha ya Mbappe kufunga mabao matatu (Hat-Trick), ila Ufaransa ilishindwa kutamba na kukubali kichapo kwa mikwaju ya penalti 4-2, dhidi ya Argentina baada ya sare ya 3-3, katika dakika zote 120.