Messi aandika rekodi, afunga hat-trick ya kwanza Kombe la Dunia
Muktasari:
- Nyota huyo ameiongoza Argentina kuichapa Algeria mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi J uliochezwa alfajiri ya leo, Jumatano mjini Kansas City.
NAHODHA wa Argentina, Lionel Messi ameendelea kuthibitisha kuwa umri ni namba baada ya kuandika rekodi nyingine katika Kombe la Dunia 2026 kwa kufunga mabao matatu (hat-trick) ya kwanza kwenye fainali za michuano hiyo.
Nyota huyo ameiongoza Argentina kuichapa Algeria mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi J uliochezwa alfajiri ya leo, Jumatano mjini Kansas City.
Messi, mwenye umri wa miaka 38, alionekana kuwa katika kiwango chake bora zaidi akifunga mabao yote matatu dakika za 17, 60 na 76 na kuifanya Argentina kuanza kampeni ya kutetea ubingwa kwa ushindi mnono mbele ya maelfu ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo.
Bao la kwanza la nyota huyo lilitokana na pasi ya Rodrigo De Paul katika dakika ya 17 ambapo Messi alitumia nafasi hiyo kwa ustadi kuipa Argentina uongozi wa bao 1-0 uliodumu hadi mapumziko.
Algeria walijaribu kurejea kipindi cha pili, lakini walikutana na ukuta mgumu wa Argentina iliyokuwa ikiongozwa na Messi aliyekuwa kila mahali uwanjani.
Dakika ya 60 aliongeza bao la pili baada ya kipa Luca Zidane kushindwa kuudhibiti mpira uliopigwa na Alexis Mac Allister na kumwachia Messi kazi rahisi ya kuusukuma wavuni.
Akiwa ameonyesha kiu ya kuendelea kuweka rekodi mpya, Messi alikamilisha hat-trick yake dakika ya 76 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Nico Gonzalez na kuachia shuti kali lililomshinda Zidane na kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki wa Argentina.
Hat-trick hiyo sio kwamba imeiwezesha Argentina kupata pointi tatu muhimu, bali pia imemfanya Messi kuingia kwenye vitabu vya historia ya Kombe la Dunia kwa kufikisha mabao 16 katika michuano hiyo, idadi inayomfanya afungane na mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani, Miroslav Klose ambaye alikuwa akishikilia rekodi ya mabao mengi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.
Kwa mujibu wa takwimu za FIFA, Messi sasa ameifikia rekodi hiyo katika Kombe la Dunia lake la sita, jambo linaloonyesha uimara wake wa ajabu katika soka la kimataifa kwa zaidi ya miongo miwili.
Hat-trick hiyo pia ni ya kwanza kufungwa katika Kombe la Dunia tangu Kylian Mbappe alipofanya hivyo kwenye fainali ya mwaka 2022 dhidi ya Argentina nchini Qatar.
Tofauti ni kwamba safari hii Messi ndiye aliyefanya maajabu hayo na kuonyesha kuwa bado ana uwezo wa kubadili matokeo ya mechi kubwa.
Baada ya kufunga mabao matatu, kocha wa Argentina aliamua kumpumzisha dakika ya 79 na nafasi yake kuchukuliwa na Nico Paz huku mashabiki wakisimama kumpigia makofi nahodha huyo aliyekuwa ameandika historia nyingine kubwa katika maisha yake ya soka.
Ushindi huo unaifanya Argentina kuanza vyema mbio za kutinga hatua ya mtoano, huku macho ya dunia sasa yakielekezwa kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Austria.
Endapo Messi atafunga tena katika mchezo huo, atavunja rasmi rekodi ya Klose na kuwa mfungaji bora wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia.