Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wesley aumia, Ederson kuchukua nafasi Brazil

EDERSON Pict

Muktasari:

  • Wesley, anayekipiga AS Roma ya Italia, alitoka uwanjani huku akibubujikwa na machozi baada ya kucheza dakika 15 pekee katika mechi ya kirafiki ambayo Brazil ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Misri kwenye mechi ya mwisho ya maandalizi ya Kombe la Dunia.

RIO DE JANEIRO, BRAZIL: TIMU ya taifa ya Brazil imepata pigo kubwa wakati fainali za Kombe la Dunia zikikaribia, baada ya beki wake wa kulia, Wesley kutangazwa kukosa mashindano hayo kutokana na majeraha ya misuli ya paja, huku kiungo Ederson akiitwa kuziba nafasi yake.

Wesley, anayekipiga AS Roma ya Italia, alitoka uwanjani huku akibubujikwa na machozi baada ya kucheza dakika 15 pekee katika mechi ya kirafiki ambayo Brazil ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Misri kwenye mechi ya mwisho ya maandalizi ya Kombe la Dunia.

Baada ya kufanyiwa vipimo vya kina, Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) lilithibitisha nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 amepata tatizo kubwa la misuli ambalo litamfanya ashindwe kushiriki michuano hiyo inayotarajiwa kuanza wiki hii Marekani, Canada na Mexico.

EDER 02

“Uchunguzi wa MRI umeonyesha majeraha ya kukaza misuli ya paja lake la kushoto,” ilisema taarifa ya CBF.

“Tunasikitishwa na majeraha haya. Wesley ni mchezaji anayependwa sana ndani ya kikosi na ataendelea kuwa sehemu muhimu ya familia ya timu hii inayopambana kutafuta taji la sita la Kombe la Dunia.”

Kutokana na hali hiyo, Kocha Carlo Ancelotti ameamua kumuita Ederson ambaye anatarajiwa kujiunga na Manchester United mwezi Julai baada ya klabu hiyo kufikia makubaliano ya Pauni 35 milioni na Atalanta ya Italia.

Ederson, 26, atajiunga na kambi ya Brazil nchini Marekani na kurejea kwenye kikosi hicho kwa mara ya kwanza tangu alipocheza mechi yake ya mwisho ya kimataifa mwezi Machi mwaka jana.

Katika mchezo huo dhidi ya Misri, Brazil ilianza vizuri kwa bao la Bruno Guimaraes dakika ya saba kabla ya Mostafa Zico kuisawazishia Misri dakika nne baadaye kutokana na makosa ya Marquinhos.

EDER 03

Baada ya mapumziko, straika chipukizi wa Real Madrid, Endrick mwenye miaka 19, alifunga bao la ushindi baada ya kupokea pasi ya Raphinha.

Kocha Ancelotti amesema ameridhishwa na kiwango cha timu yake baada ya ushindi huo baada ya ule wa mabao 6-2 dhidi ya Panama wiki iliyopita.

“Nadhani timu ilicheza vizuri, kwa kasi, nidhamu na mpangilio mzuri. Tulifanya presha kubwa kwa wapinzani na hilo limenifurahisha,” amesema Ancelotti.

Brazil itaanza kampeni zake za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco kabla ya kucheza na Haiti na baadaye Scotland katika hatua ya makundi.