Dili iliyokufa - 12
ILIPOISHIA
Siku iliyofuata baada ya Wakwetu kuondoka nyumbani kwenda kazini kwake, Sharifa naye alitoka. Alikodi teksi iliyompeleka Kwaminchi kwa mwanawe.
Alimkuta majaliwa akijiandaa kwenda sokoni kununua viazi na mahitaji mengine ya biashara yake.
“Ndio unataka kwenda sokoni?” Mama yake akamuuliza.
“Ndiyo nilikuwa nataka kutoka”
“Hebu kaa kidogo. Kuna kitu ninataka kukueleza”
Majaliwa akakaa na mama yake naye akakaa.
“Sikiliza mwanangu bila kutumia ujanja tutakufa masikini. Yule mume wangu ana watoto wake anawatafuta, sidhani kama atawapata lakini kama atafanikiwa kuwapata ndio watakuwa warithi wake. Sasa mimi nataka nikupachike wewe pale nyumbani ujifanye ni mmoja wa hao watoto wake. Unasemaje utaweza?”
“Endelea kunieleza ili nipate kuelewa jinsi ambavyo tutafanya mpaka aone kuwa mimi ni mtoto wake”.
SASA ENDELEA...
“MIMI nataka kumshauri atoe tangazo gazetini la kuwatafuta watoto wake. Litakapotoka hilo tangazo kwa vile atakuwa ameweka na namba yake ya simu nataka umpigie ujitambulishe kuwa wewe ni mwanawe umeona hilo tangazo kwenye gazeti. Umenielewa”
“Mpaka hapo nimekuelewa. Enhe…?”
“Ukishampigia simu na kumueleza maneno hayo lazima atataka kuonana na wewe, atakuita ofisini kwake au nyumbani kwake ambako atakuuliza maswali. Sasa hapo kwenye maswali ndio unatakiwa uwe makini sana”
“Kwa mfano ataniulizaje?”
“Atakuuliza unadhani yeye ni baba yako kivipi? Kwanza nataka ujue watoto wake anaowatafuta ni wawili. Hao watoto ni mapacha na wote ni wanaume. Mama yao alikuwa akiitwa Zainab, aliwazaa kwa operesheni lakini alifariki wakati wa operesheni hiyo. sasa wale watoto walilelewa na bibi yao ambaye pia alikuwa anaitwa jina hilo hilo la Zainab. Umenielewa. Zingatia haya ninayokueleza”
“Ninakuelewa, endelea kunieleza”
“Enhee…sasa yule bibi aliyekuwa akiwalea naye alikufa wakati wale watoto bado wakiwa wadogo. Sasa inasemekana walichukuliwa na mama mmoja wa kiarabu aliokwenda kuwalea nyumbani kwake eneo la Nguvumali. Wale watoto walipofikia umri wa kwenda shule aliwapeleka shule lakini inaelezwa kuwa mume wake yule mama alifariki. Kwa hiyo mwanamke huyo akaamua kurudi kwao Oman. Baada ya hapo haikujulikana wale watoto walikwenda wapi”
“Na wakati hao watoto wanazaliwa mpaka wanalelewa na huyo mwanamke wa kiarabu, huyo baba alikuwa wapi?”
“Nimesahau kukueleza. Huyo baba yao ambaye ndiye mume wangu hivi sasa alikuwa ameondoka kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha. Alimuacha mke wake akiwa na mimba. Yule bwana alivyoondoka ndio hakurudi tena hadi mwaka juzi. Amerudi akiwa mtu mzima, ndio akaambiwa mke wake alikufa na watoto wake hawajulikani wako wapi. Ndio sasa ameanza kuwatafuta”
Sharifa aliendelea kumueleza Majaliwa.
“Kuna mzee mmoja aliyekuwa akiishi jirani na nyumba aliyokuwa akiishi huyo bibi alimwambia kuwa kuna taarifa kuwa hao watoto wako Zambia lakini haifahamiki wako kwa nani na wanafanya nini huko. Kwa hiyo akikuuliza ulikuwa wapi mwambie nilikuwa Lusaka Zambia”
“Umesema kwamba hao watoto walikuwa wawili, si ataniuliza huyo mwenzangu yuko wapi?” Majaliwa akamuuliza.
“Mwambie alipata homa akafariki huko huko Zambia tangu mwaka juzi”
“Akiniuliza tulikuwa tunaishi kwa nani nimjibu nini?”
“Mwambie mlikuwa mnakaa geto, geto la vijana wa kitanzania waliokwenda huko kutafuta maisha”
“Na labda atataka kujua tulikuwa tunafanya kazi gani?”
“Mwambie mlikuwa mnafanya vibarua kama vile kuosha magari, kubeba mizigo na kazi zingine zisizohitaji elimu”
“Sasa mimi sina paspoti, anaweza kuniuliza paspoti yangu iko wapi”
“Vijana wengi wanaotorokea nchi za jirani wanatumia njia za panya. Hawatumii paspoti”
“Sasa nimwambie nimerudi lini kutoka huko Zambia?”
“Mwambie umerudi miezi michache tu iliyopita ukapangisha chumba hapa Kwaminchi na kuanzisha mradi wa chipsi. Hata kama atataka kuja kuuona unaweza kuja naye”
“Mpaka hapo nimekuelewa. Sasa kuhusu tulivyochukuliwa na huyo mwanamke wa kiarabu. Ataniuliza alitupeleka wapi na maisha yalikuwaje”
“Nimekwambia kwamba huyo mwanamke aliishi na wale watoto Nguvumali. Mwambie mlichukuliwa mkiwa wadogo na hamkuwa na fahamu. Mlipopata fahamu mlijikuta mko kwa mwanamke huyo. Mlipotimiza umri wa miaka saba akawapeleka shule lakini kabla ya kumaliza kidato cha nne, mume wa huyo mwanamke alifariki dunia, huyo mwanamke akaamua kurudi zake kwao Oman”
“Halafu sisi tutakuwa tumekwenda wapi au ndio tukaenda Zambia?”
“Hapana. Mwambie yule mama alitupangia vyumba kule kule Nguvumali, akatupa na pesa tuanzishe biashara lakini tukaona maisha ni magumu tukatorokea Zambia pamoja na vijana wenzetu. Maswali mengine utajibu kwa akili yako tu”
“Kwa mfano anaweza kuniuliza nimejuaje kuwa yeye ndiye baba yangu?”
“Mwambie huyo mwanamke wa kirabu aliwaeleza historia yenu akawapa na jina la baba yenu na la mama yenu. Kwa hiyo uliposoma lile tangazo ukatambua kuwa yeye ndiye baba yako”
“Basi mshawishi atoe hilo tangazo, nitampigia simu”
Baada ya Sharifa kupanga mkakati huo na mwanawe ndipo ukafuatia mkakati mwingine wa kumshawishi Wakwetu atoe tangazo hilo la kuwatafuta wanawe kwenye gazeti.
Wakwetu alipopewa wazo hulo na Sharifa alimsifu kuwa alimpa wazo la akili.
“Unajua umenipa wazo la maana sana, sikuwahi kufikiria hata siku moja nitoe tangazo kwenye gazeti” Wakwetu akamwambia Sharifa.
“Unajua nimefikiria kuwa huenda hao watoto wako hapa hapa Tanga wanahangaika tu, wakiona hilo tangazo wanaweza kujitokeza”
“Ni kweli, nitalipeleka hilo tangazo leo leo”
“Ukilipeleka leo, kesho litatoka. Na kesho hiyo hiyo unaweza kufanikiwa kuwapata watoto wako”
“Ni kweli mke wangu, nashukuru sana kwa kunipa wazo hilo”
Siku hiyo hiyo Wakwetu alipeleka tangazo hilo kwenye gazeti. Alilipeleka pamoja na picha yake. Tangazo hilo liliandikwa na Sharifa kwenye karatasi na Wakwetu akaridhia litoke hilo hilo.
Baada ya kupeleka tangazo hilo na kulipia nusu ukurasa ili liweze kuonekana vizuri, siku ya pili yake tangazo likatoka.
Alipoliona tangazo hilo kwenye gazeti, Wakwetu alimpigia simu mke wake.
“Lile tangazo limetoka”
“Limetoka pamoja na picha yako?” Sharifa akamuuliza.
“Ndiyo, limetoka pamoja na picha yangu na maaelezo yote uliyoandika”
“Pamoja na namba zako za simu?”
“Ndiyo”
“Basi subiri, katika siku mbili tatu hizi lazima watu watakupigia simu”
“Ndiyo nasubiri”
Baada ya kuzungumza na mume wake Sharifa akampigia mwanawe Majaliwa.
“Lile tangazo nililokwambia limeshatoka kwenye gazeti la leo” Sharifa alimwambia na kumtajia hilo gazeti.
Akaendelea kumwambia.
“Nenda kalinunue usome hilo tangazo na umuone huyo baba yako, picha yake ipo hapo”
“Halafu nimpigie simu?”
“Usimpigie leo, subiri hadi kesho utampigia asubuhi. Nataka umpigie simu asubuhi kabla hajatoka hapa nyumbani”
“Kama saa ngapi?”
“Mpigie saa moja asubuhi”
“Basi nitampigia muda huo”
“Sasa kalinunue hilo gazeti ili upate namba yake ya simu”
“Nitakwenda kulinunua sasa hivi”
“Hilo tangazo liko ukurasa wa nane wa hilo gazeti”
“Sawa. Nitaliona”
Siku ile mpaka inafika jioni Wakwetu alipigiwa simu na watu mbalimbali ambao walidai kuwa wanatafuta wazazi wao. Lakini baada ya kuwauliza maswali machache tu kwenye simu, aligundua kuwa hawakuwa watoto wake.
Aliporudi nyumbani jioni, alimueleza mke wake kuwa alipigiwa simu kadhaa kutoka kwa watu mbalimbali.
“Wamekwambiaje?”
“Ni watu wanaotafuta wazazi wao lakini baada ya kuwauliza maswali yangu nimegundua kuwa sio watoto wangu”
“Uwe makini, watu wengine ni matapeli. Mtu akikupigia simu lazima akupe historia yake na ifanane na ile unayoijua wewe”
“Ndio maana nikatambua kuwa hao walionipigia sio watoto wangu. Walikuwa wananieleza historia tofauti”
“Nafikiria Wako wengine watakaoendelea kukupigia pengine kesho au keshokutwa”
“Nawasubiri”
“Wanaohusika utawapata tu”
“Tuombe Mungu”
“Inshaalah kwa uwezo wa Mmenyezi Mungu watajitokeza, ondoa wasiwasi mume wangu”
Alfajiri ya siku ya pili yake Sharifa aliamka akatoka uani akiwa na simu yake mkononi. Akampigia mwanawe Majaliwa.
Simu iliita sana kabla ya kupokelewa. Ilipopokelewa sauti ya Majaliwa ilikuwa nzito ikionesha kuwa aliamshwa usingizini.
“Shikamoo mama”
“Marahaba. Yaani bado umelala hadi muda huu?”
“Niliamka mapema”