Prime
‘Sekunde za moto’ zinavyolinasua soka la Kombe la Dunia
Fainali za Kombe la Dunia zimeanza Marekani, Canada na Mexico, ikiwa ni mara vya kwanza kwa mashindano hayo makubwa duniani katika soka kuandaliwa na mataifa matatu baada ya Korea Kusini na Japan kuwa nchi za kwanza kuandaa kwa pamoja mwaka 2002.
Kwa mara ya kwanza, fainali hizo zitashirikisha nchi 48, ikiwa ni ongezeko la nchi 16 kutoka fainali za Qatar zilizofanyika mwaka 2022, huku Afrika ikiwakilishwa na mataifa 10, ikiwa ni rekodi kwa bara hili baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuiondoa Canada katika mechi za mchujo baina ya wawakilishi wa mabara.
Jukwaa hilo kubwa la michezo linafuatiliwa na mabilioni ya wakazi wa dunia na hivyo kuvuta macho ya kampuni kubwa duniani ambazo hunufaika na jukwaa linalotengenezwa na fainali hizo kutangaza bidhaa au huduma mbalimbali.
Ni kwa jinsi hiyo, fainali za Kombe la Dunia zimekuwa chanzo kikubwa cha mapato cha Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) ambalo huandaa mashindano hayo kila baada ya miaka minne. Mapato hayo ndiyo yanaitamanisha Fifa kuandaa fainali hizo kila baada ya miaka miwili, jambo linalopingwa sana na vyama vya nchi, klabu na umoja wa wachezaji.
Fainali hizo pia ni siasa kubwa kwa nchi zinazoshiriki na zinazoandaa kwa kuwa mafanikio uwanjani huwezesha wanasiasa kuyatumia kwa masilahi yao au ya nchi zao, huku uandaaji hutumiwa kwa njia nyingi kisiasa na kiuchumi.
Ni kutokana na thamani inayotengenezwa na fainali hizo, Fifa hukodolea macho yote katika kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ufanisi, haki, uwazi na mambo mengine ambayo yatawafanya wadau wake wamalize wakiwa na roho safi.
Ndiyo maana kumekuwepo na uboresha wa sheria 17 za soka kwa kuweka tafsiri mpya katika sheria ambazo zitawezesha mchezo kutosimamasimama ovyo au kuboresha kanuni kama za matumizi ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R).
Wachezaji wanaopoteza muda wakati wa kurusha mpira, wataziponza timu zao kwa kuwa wamepewa sekunde chache na wasipofanya hivyo ndani ya muda huo, timu pinzani itapewa faida hiyo. Kipa naye atasababisha kona iwapo atashindwa kuanzisha mpira uliotoka golini mwake ndani ya sekunde nane.
Mchezaji anayebadilishwa, akichelewa kutoka atasababisha mchezaji anayeingia asubiri nje kwa dakika moja. Hali kadhalika mchezaji atakayetibiwa uwanjani, atalazimima kusubiri dakika moja nje ndipo aingie. Hiyo haitafanyika kwa kipa.
Fifa pia imeboresha kanuniza V.A.R kwa kuongeza tukio la kadi ya pili ya njano. Kwamba awali, mchezaji akionyeshwa kadi ya pili ya njano, hakukuwa na ulazima wa kuangalia marudio ya video kujua kama alifanya kosa au hakufanya. Hii ni kwa sababu kadi ya pili ya njano humaanisha mchezaji atoke nje au humaanisha ni kadi nyekundu, hali ambayo huathiri timu moja na hivyo Fifa imeona ni vizuri uamuzi wa tukio linaloweza kuathiri idadi ya wachezaji uwanjani, ufanywe kwa usahihi.
Kuna ripota wangu mmoja ambaye kila ilipofika muda wa mashindano kama hayo alizoea kuandika katika safu yake akisema “tuangalie fainali hizo ili tujifunze”. Ni kweli kuna mengi ya kujifunza katika fainali hizo.
Na kubwa ambalo naliona ni hili la uamuzi, protokali za V.A.R na mambo mengine.
Fifa inajua jinsi fainali hizo zilivyo muhimu kwake kutokana na ukweli zinagusa hisia za mashabiki, viongozi wa nchi, viongozi au wamiliki wa kampuni kubwa duniani, warushaji wa matangazo na wadau wengine wengi na ndiyo maana imeona kitu cha kwanza na muhimu, ni kuhakikisha mchezo hauwi wa kuudhi na kukera, bali wenye mvuto kwa wakati wote.
Inataka kuhakikisha timu haipati ushindi kwa kubahatisha baada ya kupata bao na kutumia sehemu kubwa ya mchezo kujilinda na kupoteza muda. Hata mashabiki wa timu inayoongoza, hukosa raha halisi pale timu yao inapofanya kazi moja tu ya kuzuia na kupoteza muda, ingawa ushindi kwao ndio kitu kikubwa. Lakini ushindi ni matokeo na si mchezo. Ni lazima mchezo wenyewe uvutie, ufurahishe na uburudishe.
Pia Fifa inafanya uteuzi wa waamuzi kwa makini kuhakikisha ‘makosa ya kibinadamu’ hayazinyongi timu zinazostahili kupata matokeo mazuri, Ndiyo maana refa aliyefanya makosa fainali ya Ligi ya Mabingwa baina ya Arsenal na Paris Saint Germain ameondolewa dakika za mwisho.
Hii yote ni kutuma ujumbe kuwa suala la uamuzi ni moja kati ya misingi minne mikuu ya mpira wa miguu.
Ingawa uamuzi katika fainali za Kombe la Dunia umewezeshwa sana na teknolojia, bado kuna mambo mengi ambayo mamlaka za soka nchini itabidi wayaangalie kwa makini, kuyatafakari na kuyatafutia suluhisho linalolingana na kiwango chetu cha maendeleo.
Hivi sasa tumefikia hatua mbaya ya kamati kufanya uamuzi uliostahili kufanywa na refa. Hii si hatua nzuri hata kidogo. Kama kamati inafanya uamuzi wa kumuadhibu mchezaji kwa kucheza rafu ambayo ama mwamuzi hakuiona au hakuichukulia hatua, kuna uwezekano wa kuizuia kamati hii kufikia hatua ya kufuta goli?
Hata kwa wenzetu barani Ulaya kabla ya kuanza kutumia teknolojia ya V.A.R, hawakufikia hatua ya kumwadhibu mchezaji ambaye hakuadhibiwa kwa kosa alilofanya na refa hakulipulizia filimbi. Waliweza kuchukua hatua tu pale na mchezaji alifanya kosa wakati mchezo umesimama.
Adhabu kama ya Ibrahim Bacca na Jonathan Sowah hazijawahi kutolewa duniani na mamlaka zozote. Kama mwamuzi anafanya kosa, basi yeye ndiye huwajibishwa kwa kuwa ndiye aliyepewa mamlaka yote uwanjani.
Tutaona katika fainali hizi wajibu wote anapewa refa na si baadhi ya mamlaka kuchukuliwa na kikundi cha watu. Iwapo kuna tukio tata linalolazimisha mwamuzi kwenda kuangalia marudio kwenye runinga iliyopo pembeni ya uwanja, basi mwamuzi huyo anatakiwa atangaze kwa mashabiki wote waliopo uwanjani kuwa ameona nini na sheria inasemaje na tafsiri yake ni nini na hivyo kutangaza uamuzi.
Huku ni kumbebesha refa wajibu kwa mashabiki na si kusubiri eti kwenda kuangalia marudio katika vifaa au teknolojia na haijaruhusiwa na Fifa na kufanya uamuzi ambao refa hakuufanya kwa kujua hakutakiwa kufanya au kwa kutoliona tukio vizuri.
Arsene Wenger, kocha wa zamani wa Arsenal, aliwahi kusema ili mwamuzi afanye uamuzi wa penati, ni muhimu akawa na uhakika wa asilimia zaidi ya 70 ya tukio hilo. Ndiyo maana V.A.R ikabuniwa ili angalau kumwezesha refa kuwa na uhakika wa asilimia 90 ili afanye uamuzi sahihi.
Hawa wanaokaa mezani kumsahihisha refa wanatuhumia teknolojia gani iliyoruhusiwa na Fifa? Maana hadi sasa ni teknolojia ya V.A..R na ya mstari wa goli (goal line) ndizo zinazotumika kuamua. Vipi mamlaka za kwetu?
Kwa hiyo, tafsiri ya vitendo vitakavyokuwa vinafanywa na waamuzi kwenye fainali hizi, iangaliwe kwa mazingira yetu na kiwango cha maendeleo na teknolojia tuliyonayo. Tusikimbilie kutaka kuiga maamuzi yao wakati maendeleo yetu hayajafikia huko.
Misingi ya maamuzi yetu iendelee kubakia kulingana na kiwango chetu, lakini taratibu za kuamua ziboreshwe ili kusiwe na mijadala kila siku ya ‘makosa ya kibinadamu’ ya waamuzi wetu.