Prime
Wasauzi waichokonoa Yanga
Muktasari:
- Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza mazungumzo ya awali na wawakilishi wa mshambuliaji huyo tayari yameshafanyika, huku mchezaji mwenyewe akionyesha nia ya kucheza katika timu hiyo, kutokana na kuvutiwa na mradi uliopo kikosini humo.
WAKATI mabosi wa Yanga wakipiga hesabu za kumsajili mshambuliaji wa Power Dynamos ya Zambia, Mkenya Moses Shumah ghafla mabwanyenye wa AmaZulu FC kutoka Afrika Kusini wameingilia kati dili hilo.
Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza mazungumzo ya awali na wawakilishi wa mshambuliaji huyo tayari yameshafanyika, huku mchezaji mwenyewe akionyesha nia ya kucheza katika timu hiyo, kutokana na kuvutiwa na mradi uliopo kikosini humo.
Hata hivyo, taarifa hizo zinaeleza hakuna makubaliano rasmi yaliyofanyika kati ya mchezaji huyo na AmaZulu, japo tayari kuna mazungumzo ya awali ambayo inaelezwa huenda dili hilo likakamilika na kuiacha Yanga inayomuhitaji ikiwa njia panda.
Mwanaspoti linatambua Yanga inatafuta mshambuliaji mpya ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho, kwani kwa sasa inadaiwa huenda ikaachana na Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ raia wa Angola aliyejiunga nayo dirisha dogo la Januari 2026.
Depu aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Radomiak Radom FC ya Poland kwa chaguo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves raia wa Ureno, licha ya kuifungia Yanga mabao sita ya Ligi Kuu msimu huu, ila bado inadaiwa huenda akaondoka.
Kwa upande wa Shumah anayepigiwa hesabu na Yanga, katika Ligi Kuu Zambia msimu wa 2025-2026 amemaliza akiwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21 katika mechi 25 za Power Dynamos akionyesha kiwango kizuri kinachovutia timu mbalimbali.
Mabao hayo 21 yamemwezesha kuvunja rekodi ya Mkenya mwenzake, Jesse Were aliyeifungia Zesco United FC mabao 18 msimu wa 2017, huku akimpiku pia aliyekuwa nyota wa Azam FC, Mkongomani Idriss Mbombo aliyeifungia Nkana FC mabao 20, mwaka 2018.