SMZ yatenga Sh5 bilioni maandalizi AFCON 2027
Muktasari:
- Wadau wa michezo walieleza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta hiyo utasaidia kuinua viwango vya michezo, kuvutia mashindano ya kimataifa na kutoa fursa zaidi kwa vijana kujiajiri kupitia shughuli zinazohusiana na michezo.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, hatua inayotarajiwa kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Ali Abdulgulam Hussein, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Mao wakati wa bonanza la michezo lililowashirikisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wanamichezo wa klabu ya wazee ya Arusha.
Amesema, maandalizi ya AFCON 2027 yatafungua fursa nyingi za ajira kwa vijana pamoja na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“Tunatarajia kuona manufaa makubwa kupitia AFCON mbali na michezo mashindano haya yatachochea uchumi, kuongeza ajira na kuvutia wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali,”€ amesema.
Aidha, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya michezo ikiwemo mradi wa Fumba ambapo mradi huo unahusisha ujenzi wa uwanja wa michezo, viwanja viwili vya kuogelea pamoja na miundombinu mingine itakayosaidia kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha michezo ya kimataifa.
Sambamba na hayo, Naibu huyo aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuidhinisha Sh243 bilioni kuwa bajeti ya wizara hiyo mwaka wa fedha 2026-2027, ambayo imeweka mkazo mkubwa katika kuendeleza sekta ya michezo na maandalizi ya mashindano makubwa ya kimataifa.
Wadau wa michezo walieleza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta hiyo utasaidia kuinua viwango vya michezo, kuvutia mashindano ya kimataifa na kutoa fursa zaidi kwa vijana kujiajiri kupitia shughuli zinazohusiana na michezo.