Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hohehahe hawezi kumvaa Perez urais Real Madrid

ZENGWE Pict


Pengine ni kutokana na utamaduni wetu uliojengwa kwa kiasi fulani na misingi ya siasa za ujamaa, uchaguzi huwa hauangalii sana hali ya kiuchumi ya mgombea, hata wa nafasi kubwa kama ya urais wa taasisi au klabu za michezo.


Hii ni kwa sababu ya imani zetu, binadamu wote ni sawa na uongozi ni haki ya kila mtu bila ya kujali rangi yake, hali ya kiuchumi kabisa na mambo mengine yanayoweka ubaguzi wa aina fulani.


Katika mazingira hayo, ni thamani ya fomu tu ndiyo inaweza kutofautiana kati ya nafasi moja na nyingine na mara nyingi katika uenyekiti au urais wa klabu zetu, hasa za soka, fomu ya nafasi hizo hufikia hadi Sh1 milioni.

Kwa sababu ya utamaduni wetu, mgombea anaweza asitoe hata senti moja kwa kuwa wanaomuunga mkono wanaweza wakachanga na kwenda kumlipia na kumchukulia fomu. Ama mwanachama mmoja anaweza kujitolea kumlipia hiyo fomu na mambo yakaendelea.

ZENG 01

Labda sifa zilizowekwa kwenye katiba na kanuni za uchaguzi ndio zinaweza kutofautisha wagombea, hasa inapofikia suala la muda wa uzoefu, lakini elimu si kikwazo wala stadi nyingine muhimu katika uongozi.

Kwa hiyo, mgombea anaweza kupitishwa kugombea nafasi kubwa kabisa bila ya hiyo taasisi kuwa na uhakika wa hali yake ya kiuchumi, ambayo inaweza kusababisha asiweze kumudu masuala ya uongozi vizuri au akaingia kwa lengo la kujijenga kiuchumi.

Baadhi ya wenye uwezo kidogo, huingia kwenye purukushani za kugombea uongozi kwa lengo la kutumia taasisi au klabu hiyo kama ngazi ya kupandia kwenda kwenye masuala ya kisiasa, ambako uchumi ni mzuri na matarajio ya kupandishwa juu zaidi kama kwenye nafasi za uwaziri, ni makubwa pia.

ZENG 05

Hata hivyo, Real Madrid, moja ya klabu kubwa za michezo duniani, imeweka utaratibu tofauti ambao unamzuia mtu asiye na uchumi mzuri kugombea nafasi ya urais.

Kwa sasa klabu hiyo inaenda kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Juni 7 baada ya rais wa sasa, Fiorentine Perez Rodrigue kuiagiza Bodi ya Uchaguzi kuitisha mchakato huo kutokana na chokochoko nyingi zilizokuwa zinaendelea baada ya vigogo hao wa soka Ulaya na duniani kutokuwa na msimu mzuri.

Perez alichaguliwa kwa mara ya mwisho mwaka 2025 akiwa mgombea pekee na alitakiwa akae madarakani hadi mwaka 2029, lakini kelele za kutaka mabadiliko zilizosababishwa na timu kukosa mataji miaka ya karibuni, zilisababisha Perez kuitisha uchaguzi, akisema kelele hizo zinasababishwa na watu wanaoutaka urais na akaamua kuitisha uchaguzi ili wajitokeze.

ZENG 02

Hadi mapema wiki hii, Bodi ya Uchaguzi ilisharidhika na wagombea wawili, yaani Perez, mwenye miaka 79 na mfanyabiashara mwenye kampuni za ujenzi, Enrique Riquelme (37). Kwa mujibu wa sheria ya klabu hiyo, Bodi ya Uchaguzi inaweza kuamua wanachama wapige kura pale inaporidhika wagombea kuanzia wawili wamekidhi vigezo vilivyowekwa kikatiba.

Ikisharidhika ndipo hutangaza tarehe ya uchaguzi na ikiwa ni mmoja tu aliyekidhi vigezo, huchukuliwa ndiye aliyechaguliwa. Mara ya mwisho kwa wanachama wa Real Madrid kupiga kura ya kumchagua rais ilikuwa mwaka 2006, wakati miaka mingine Perez alipita kutokana na kukosa mpinzani wa kukidhi kigezo hicho cha kifedha.

Bodi pia hutangaza sehemu ambazo wanachama watapiga kura. Wale ambao hawawezi kwenda vituoni, huweza kupiga kura kwa barua pepe lakini kwa masharti makali yaliyowekwa kwenye kanuni.

ZENG 04

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi, Jose Manuel de Carlos Gau, uchaguzi huo utafanyika Juni 7 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

Taarifa hiyo inaeleza wanachama watapiga kura kwenye banda la timu ya mpira wa kikapu ya Real Madrid, Avenida Alejandro de la Sota s/n Madrid. Wanachama watatakiwa kuthibitisha ushiriki wao au kutoshiriki kwa kutumia ofisi ya mtandaoni ya wanachama (online Member Support Office).

Wakati wanachama wakienda kwenye uchaguzi, wagombea wanatakiwa wawe na sifa kadhaa, ikiwemo hiyo muhimu ya hali ya kiuchumi kwa sasa.

Sharti la kwanza ni lazima mgombea awe ni raia wa Hispania na mwenye haki zote kamili za uanachama wa Real. Anatakiwa awe mwanachama aliyesajiliwa (socio member) kwa angalau miaka 20 mfululizo.

Sharti ambalo lingekuwa gumu kwa wagombea wa klabu na taasisi zetu ni lile la hali ya kiuchumi. Mgombea anatakiwa awasilishe dhamana ya benki (bank guarantee) iliyo sawa na asilimia 15 ya bajeti ya klabu ya mwaka.

Mgombea anatakiwa asiwe na nafasi kwenye menejimenti ya klabu nyingine kuepuka mgongano wa masilahi na hatakiwi kuwa anaendelea kucheza soka, kocha, refa au awe kwenye timu ya ufundi ya klabu.

Mgombea anatakiwa awasilishe orodha kamili ya wajumbe wa bodi anaotarajia kufanya nao kazi. Anatakiwa kufanya hivyo ndani ya siku 10 tangu kutangazwa kwa uchaguzi

ZENG 03

Kiwango hicho, kwa mujibu wa bajeti ya mwaka huu na mali za klabu, ni sawa na Euro 187 milioni (sawa na Sh3.06 bilioni). Kiwango hicho kinakwenda sambamba na utajiri binafsi na mali binafsi za mgombea.

Kwa kigezo hicho, wagombea hupata shida kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais na pengine ndiyo maana Perez ameitisha uchaguzi ghafla, akijua wapinzani wake hawawezi kupata muda wa kutosha kukusanya nyaraka za kutosha kwa ajili ya kuziwasilisha.

“Ni upuuzi kwangu kwamba kugombea urais wa Real Madrid unahitaji kuwa na takriban Euro milioni 200 za dhamana zako binafsi benki,” alisema Riquelme, kwa mujibu wa Fabrizio Romano, mwandishi maarufu anayesifika kwa habari za usajili.

“Nina uhakika kuna wanachama wengi wa Real Madrid ambao wangekuwa wagombea bora zaidi kuliko mimi na Perez, lakini hawawezi kugombea kwa sababu hawana fedha za hivyo,” alisema Riquelme.

Kwa mujibu wa tovuti ya MUNDODEPORTIVO.com, awali benki za Hispania, Santander na BBVA zilikataa kumuunga mkono Riquelme kwa kumpa dhamana hiyo, lakini baadaye alithibitisha alishapata Euro milioni 193.7, fedha ambazo imeripotiwa zimetoka taasisi ya Andbenk iliyosajiliwa Hispania.

Riquelme, ambaye ni mfanyabiashara, alipata dhamana hiyo kutokana na kuwa na hisa katika kampuni ya Cox zenye thamani ya Euro milioni 700, kwa mujibu wa Russpain.

Perez, ambaye aliingia madarakani mara ya kwanza kwa kuahidi kumsajili mshambuliaji aliyekuwa Barcelona, Luis Figo na kuigeuza klabu kuwa chapa ya dunia, anafanya kampeni na kaulimbiu ya “Historia Zaidi Kuandikwa” huku akiwa ameshamteua Jose Mourinho kuwa kocha mkuu ajaye, akiwa kama anaongeza nguvu katika kampeni.

Perez alisajili kikosi kilichojaa nyota kutoka sehemu mbalimbali duniani (galactico), kama Ronaldo de Lima, David Beckham, Figo na Roberto Carlos alipoingia kwa mara ya kwanza madarakani, lakini hakuweza kupata na akaondoka. Lakini aliporudi ameweza kutwaa mataji saba ya Ulaya, yakiwemo matatu aliyotwaa miaka mitatu mfululizo.

Riquelme, ambaye amekuwa akiponda ukarabati uliofanywa kuboresha uwanja wa Santiago Bernabeu kuwa umesababisha kuwe na sehemu finyu za kukaa, ameahidi kufanya mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa klabu hiyo, huku akiahidi kusajili nyota wa kimataifa.

Riquelme pia ameahidi kugeuza uwanja wa mazoezi wa Real Madrid wa Valdebebas kuwa jiji la wanachama, Ciudad del Socio. Kwa mujibu wa mpango wake, eneo hilo litakuwa na hoteli, mabwawa ya kuogelea, gym, viwanja vya tenisi na soka kwa ajili ya wanachama kukutana na kuwa karibu zaidi na klabu.

Pia ameahidi kujenga uwanja wa mpira wa kikapu wenye uwezo wa kuchukua watu 15,000 na kutumika pia kwa matamasha, huku akiahidi kupunguza ada ya uanachama kwa asilimia 50 na kutenga tiketi 10,000 za msimu zitakazopatikana kwa bahati nasibu ili kupunguza kero ya wanachama kusubiri kwa miaka mingi kupata tiketi hizo.

Perez anaweza kuwa ni rais mwenye mafanikio makubwa baada ya kutwaa mataji saba ya Ulaya kati ya 14 ambayo klabu hiyo imeyatwaa tangu arejee madarakani, lakini kuboronga kwa hivi karibuni kwa timu ya soka kunampa mwanya Riquelme kupenya kirahisi katika mbio hizo baada ya kuvuka kikwazo kikubwa cha kifedha.