Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CLARA LUVANGA: Kutoka kulima mpunga hadi chaguo la kwanza la soka Saudia

Muktasari:

  • Unapoitaja Al Nassr Women unazungumzia timu ya soka ya wanawake inayofanya vizuri nchini humo, lakini upande wa wanaume ndiyo timu anayoichezea supastaa wa kimataifa wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo ambaye pia ni mshindi mara tano wa tuzo ya Balon d'Or ya mwanasoka bora wa dunia.

KUNA wakati ndoto huanza kama hadithi za kawaida kabisa. Msichana mdogo kutoka mashamba ya mpunga mkoani Iringa, miguu ikiwa imejaa tope kutoka kwenye majaruba, daima kichwani alidumu na ndoto ya kucheza soka kwa kiwango cha juu kiasi cha kumvusha mipaka ya nchi.

Hivyo ndivyo ilivyoanza safari ya Clara Luvanga, nyota wa soka la wanawake nchini anayekipiga katika Klabu ya Al Nassr Women nchini Saudi Arabia.

Unapoitaja Al Nassr Women unazungumzia timu ya soka ya wanawake inayofanya vizuri nchini humo, lakini upande wa wanaume ndiyo timu anayoichezea supastaa wa kimataifa wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo ambaye pia ni mshindi mara tano wa tuzo ya Balon d'Or ya mwanasoka bora wa dunia.

Kwa sasa Clara ni chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Al Nassr Women, lakini nyuma ya mafanikio hayo kuna jasho lililomwagika kuanzia shambani, maumivu ya kukataliwa na uthubutu wa kuamua kuwa tofauti.


SAFARI ILIVYOANZA

Clara alizaliwa Kilindi mkoani Tanga, lakini kwenye harakati za wazazi kujitafuta kimaisha wakajikuta wamedondokea Iringa ambako walikuwa wanafanya kilimo cha mpunga.

Katika mahojiano na Azam TV anasema: "Nilikuwa nalima mpunga asubuhi, lakini jioni nikiona wavulana wanacheza mpira nikawa natoroka nyumbani na kujiunga nao.

“Nina tabia ya kujichanganya na watoto wa kiume, ile ilikuwa inanipa nafasi kwa sababu ikifika jioni wale walikuwa wanaenda kucheza na nilianza kucheza na watoto wa kiume na nilishawahi kucheza timu ya kijiji changu na nikajichanganya humo.”

Wakati wengi wakiona ni mchezo wa wavulana, yeye aliuona kama tiketi ya kubadili maisha. Hapo ndipo alipoanza kupambana sio tu na wapinzani uwanjani, bali pia mitazamo ya jamii.

“Kijijini nimecheza timu nyingi, Pawaga kisha nilienda Panama nilicheza pale kidogo, wakasema sina kiwango cha kucheza hiyo timu kuna rafiki yangu akaniambia niende Mapinduzi ikabidi nikafanye kibarua cha kulima mpunga ili nipate nauli ya kwenda huko walikokuwa wanacheza Ligi Daraja la Kwanza na hapa ndipo Yanga waliponiona,” anasema.


YANGA ILIMFUNGULIA MLANGO

Mwaka 2022 Yanga Princess ilimsajili baada ya kufanya vizuri akiwa na Mapinduzi alipoonyesha kiwango kikubwa kwenye mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza na ndipo kocha wa 'wananchi' hao Edna Lema akamsajili.

Lakini, mambo hayakuwa rahisi. Akiwa Yanga, Clara alikuwa analipwa Sh100,000 kwa mwezi kiasi ambacho kwa wengi kinaweza kuonekana kidogo, lakini kwake kilikuwa kikubwa.

Pesa yake ya kwanza ya usajili (sign-on fee) ilikuwa Sh2 milioni ndani ya miaka miwili. Hiyo ilikuwa fedha kubwa kwa msichana aliyewahi kutegemea mavuno ya mpunga.

"Nilipopokea milioni mbili kwa mara ya kwanza, ilikuwa pesa nyingi kwangu. Milioni moja ya kwanza nilitengeneza nyumbani kwetu kwa sababu maisha hayakuwa mazuri,” anasema mwanasoka huyo katika mahojiano na Mwanaspoti.

Baada ya mkataba wa kwanza kumalizika, alisaini mwingine wa miaka miwili. Safari hii maslahi yaliboreshwa, mshahara ukapanda hadi Sh700,000 kwa mwezi na alipewa ada ya usajili (sign-on fee) Sh6 milioni.


KULE HISPANIA

Kipaji chake kilianza kuvuka mipaka. Akasajiliwa na klabu ya Dux Logrono ya Hispania mwaka 2023, hatua iliyomfungulia mlango wa soka la Ulaya.

Alicheza kwa miezi mitatu tu na mshahara wake alikuwa analipwa takribani Sh2 milioni kwa mwezi, kiwango kikubwa zaidi ya alichowahi kupata kabla. Lakini zaidi ya fedha, Hispania ilimpa uzoefu, nidhamu na ushindani wa hali ya juu.


NAMBA MOJA SAUDIA

Baada ya kufanya vizuri Hispania akajiunga na Al Nassr Women ya Saudi Arabia. Huko, ndiko moto wa Clara unakoendelea kuwaka, tangu amejiunga na timu mwaka 2023 bado ameendelea kuwa staa wa kikosi cha kwanza.

Saudi Arabia imewekeza kwa kiasi kikubwa katika soka la wanawake, na wachezaji wa kigeni wenye ubora wanathaminiwa. Clara ameonyesha thamani yake kwa mabao, pasi za mwisho na juhudi zisizo na kuchoka.

Msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na asisti saba, uliopita alifunga mabao 21 na asisti saba, na msimu huu tayari ameweka kambani mabao 16 na asisti tatu.

Inaelezwa uhamisho wake kutoka Hispania uligharimu kiasi cha Sh51 milioni za pesa ya usajili, lakini mshahara wake ndani ya miaka mitatu, mwaka wa kwanza alikunja milioni 19, mwaka jana alilipwa Sh23 milioni na mwaka huu analipwa kwa mwezi Sh27 milioni ambao ndio msimu wake wa mwisho.

Hata hivyo, baadhi ya taarifa zinadai kuwa huenda Clara akasajiliwa Ligi Kuu England msimu ujao kwani timu kama Chelsea ya wanawake zimeonyesha nia ya kumtaka.

Kutoka kulima mpunga Iringa hadi kucheza kwenye viwanja vya kisasa vya Riyadh, safari yake ni ushuhuda kuwa ndoto hazina mipaka.


KWA NINI ALICHAGUA SOKA?

Kwa Clara, mpira haukuwa burudani tu, ulikuwa matumaini. Aliona wazi kuwa vipaji vya michezo vinaweza kufungua milango ambayo elimu pekee isingeweza kufungua haraka.

"Nilitaka kusaidia familia yangu. Niliona kupitia mpira naweza kufika mbali zaidi kuliko kitu kingine kwa sababu sikuwa na fani nyingine nje ya mpira hata masomo sikusoma sana niliishia darasa la saba,” anasema.

“Nilicheza mpira bila kujua mbele nitafanikiwa kiasi gani, nimefanikiwa nimejenga na kuna mashamba ya mpunga nalima hivyo mpira kwa kiasi chake umenisaidia kuwekeza huko.”


WA UKWELI

Clara ni mfano wa mwanamke anayepanda ngazi kwa jasho na bidii. Amevunja dhana kwamba soka si mchezo wa wanawake na ameonyesha kuwa vipaji vya Tanzania vinaweza kushindana kimataifa.

Leo hii, wasichana wengi Iringa na mikoa mingine wanapomwona Clara wakicheza, wanaona mwanga. Wanaona inawezekana kutoka kijijini hadi Ulaya na Mashariki ya Kati kupitia mpira.

Kwa hakika Clara siyo tu mchezaji, bali ni alama ya mabadiliko ya soka la wanawake Tanzania. Ni mfano bora katika hadithi ya msichana aliyekataa kubaki kwenye mipaka ya mashamba ya mpunga na kuchagua uwanja wa mpira kama jukwaa lake la maisha. Na safari bado haijaisha.