Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeya City na mkasa wa Ghana Kombe La Dunia 2014

PUMZI Pict


MBEYA City imemfukuza kazi kocha wake, Mecky Maxime, baada ya kufungwa mabao 6-0 na Yanga. Siyo tu timu hiyo ilicheza vibaya kwenye ule mchezo, bali ilipanga wachezaji wasio tegemeo kikosini. Hili likaibua maswali mengi, yawezekana ulikuwa mpango maalumu wa kutengeneza matokeo.


Lakini siku iliyofuata, Mecky Maxime akafanya mahojiano na vyombo vya habari na kuelezea mkasa mzima. Akasema alilazimika kupanga wale wachezaji kwa sababu ndio waliokuwepo. Wachezaji wengine muhimu walifungiwa na viongozi kwa kile alichoeleza ni utovu wa nidhamu.


"Viongozi waliniambia nitumie wachezaji waliopo, kama watatushusha daraja na watushushe, wakitubakisha na watubakishe," alinukuliwa akisema Mecky.

Ukiwa katikati ya msimu, matokeo yako sio mazuri na jahazi la timu linaelekea kuzama unasimamisha wachezaji muhimu, unafungwa mabao 6-0, unafukuza kocha!

PUM 01

Walichokifanya Mbeya City ndicho walichokifanya Ghana kwenye Kombe la Dunia la 2014 kule Brazil. Wakiwa kundi G pamoja na Ujerumani, Marekani na Ureno, Ghana au Black Stars waliishangaza dunia kwa kuwasimamisha wachezaji wao muhimu kuelekea mechi ya kihistoria.

Ghana ilianza mashindano kwa kupoteza kwa mabao 2-1 kwa Marekani, lakini ilibadilika mchezo wa pili dhidi ya Ujerumami. Mechi hiyo ilishuhudia ndugu wawili wa familia ya Boateng; Jérome Boateng (Ujerumani) na Kevin-Prince Boateng (Ghana) wakiweka rekodi ya kuwa wanandugu wawili kukutana mara mbili kwenye Kombe la Dunia wakitumikia mataifa tofauti, walikutana mara ya kwanza 2010.

Mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2 ilikuwa moja ya mechi bora za Kombe la Dunia la 2014 na bila shaka ndio mechi ngumu zaidi kwa waliokuja kuwa mabingwa (Ujerumani). Baada ya mechi hiyo Ghana ikabaki na mechi moja dhidi ya Ureno, ikishinda inafuzu.

PUM 02

Ureno hadi hapo walitoka kupoteza mchezo wa kwanza mabao 4-0 dhidi ya Ujerumani na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Marekani. Asubuhi ya siku ya mchezo, Ghana ikawafukuza nyota wake wawili muhimu sana kikosini, Kevin-Prince Boateng na Sulley Muntari. Timu ikapoteza morali na kufungwa mabao 2-1 na kutolewa. Matumaini ya Ghana na Afrika yakaishia hapo.

Miaka mingi baadaye Kevin-Prince Boateng akaelezea kilichotokea hadi yeye na Muntari wakafukuzwa kambini. Akasema wachezaji walikuwa hawaridhishwi na huduma walizopewa na chama chao cha soka. Wakiwa kwenye kikao, yeye alimwambia rais wa chama cha soka wao kama viongozi hawawajali wachezaji.

PUM 03

Chama kinapata pesa nyingi kupitia timu ya taifa, lakini matunzo ya timu ni ya kiwango cha chini, ikiwemo posho za wachezaji.  Akasema alishangaa alipoamka asubuhi akakuta kikaratasi kimepenyezwa mlangoni kwake. Akakiangalia lakini hakukisoma kwa sababu akili zake zilikuwa zinaiwaza mechi.

Ghafla akapigiwa simu na rafiki yake ambaye ni mwandishi wa habari kutoka Ujerumani, akampa pole ya kufukuzwa timu ya taifa. Yeye hakuwa na hizo habari, akabisha, "mbona hapa nipo kambini." Yule mwandishi akasema, "sisi tumepigiwa simu na Chama cha Soka cha Ghana na hii habari tayari ni kubwa sana hapa."

Akahisi labda kile kikaratasi ndicho kina ujumbe, akaenda kukichukua na kukisoma.

PUM 04

Kiliandikwa, "Kevin, umeondolewa kwenye timu ya taifa kwa utovu wa nidhamu na una dakika 15 tu za kurudisha chumba uondoke." Hapo simu alikuwa hajakata, akamrudia yule mwandishi na kumwambia, "kumbe ni kweli", akakata simu na kufungasha vitu vyake na kuondoka. Akaenda kumgongea Sulley Muntari, ili ampe hizo taarifa. Muntari akajua tu huyo ni Kevin, akamjibu hivi, "hata mimi nimefukuzwa, napanga vitu vyangu niondoke."

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Ghana 2014 na bila shaka ndivyo imekuwa kwa Mbeya City. Tofauti ni bado wachezaji wa Mbeya City hawajasema kilichotokea kwao hadi kusimamishwa.

Lakini viongozi wa mpira wakati mwingine huathiri timu kwa kukosa busara. Timu ipo kwenye mashindano na inahitaji wachezaji wake muhimu ili ipambane. Unakwenda kusimamisha wachezaji hao bila kujali nini kitaikuta timu. Hiki ni kipindi ambacho huwezi kusajili wachezaji wengine lazima utumie walewale ulionao.

PUM 05

Jambo la busara ni kupiga moyo konde na kuwatumia wachezaji wako muhimu ili kuiokoa timu. Msimu ukiisha achana nao wote sajili wengine kwa ajili ya msimu ujao. Lakini kusimamisha wachezaji tegemeo wakati wa mashindano ni jaribio la kujiua. Kwa timu kama Mbeya City ambayo kikosi chake lazima kitakuwa chembamba ni muhimu sana kutanguliza busara kabla ya kuchukua uamuzi wa hovyo kama huu.

Haya tayari wamefungwa mabao 6-0 na kocha amefukuzwa. Swali, wale wachezaji watawasamehe au kocha mpya atapewa kazi ya kupambana na hawa hawa? Timu hiyo imecheza mechi 19 hadi sasa ikiwa nafasi ya 13 juu ya Fountain Gate, Tanzania Prisons na KMC. Bado kuna mechi 11 za kujitetea, lakini kwa mwenendo huu yawezekana wakaanguka zaidi.

Ni wakati wao wa kuzika tofauti zao na wachezaji wao muhimu. Watafute kocha mpya na kumpa timu kamili waanze kupambania angalau nafasi ya kucheza mechi za mchujo (play off), ili kulinda hadhi yao ya Ligi Kuu. Bila hivyo, watarudi walikotoka, Championship!