Bilo FC, Ruangwa Queens hatihati kubaki WPL
Muktasari:
- Changamoto kubwa kwa Bilo FC imekuwa safu dhaifu ya ushambuliaji baada ya kufunga mabao matano huku Ruangwa Queens ikiruhusu mabao sita.
KUNA nafasi ndogo kwa Ruangwa Queens na Bilo Queens zilizopo mkiani kusalia Ligi Kuu ya Wanawake msimu ujao kutokana na muendelezo mbaya wa ligi hiyo.
Katika mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki hii, Bilo FC ilikubali kichapo kingine baada cha mabao 3-0 dhidi ya Bunda Queens, huku Ruangwa Queens ikiambulia kipigo kizito cha mabao 4-0 katika mechi za raundi ya 18.
Matokeo hayo yamezidi kuzikandamiza timu hizo mkiani mwa msimamo wa ligi huku zikiwa na nafasi ndogo ya kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
Baada ya raundi 18, Bilo FC inaburuza mkiani ikiwa na pointi nane pekee baada ya kucheza mechi 18, huku Ruangwa Queens ikiwa nafasi ya 11 na pointi tisa.
Licha ya tofauti ndogo ya pointi kati yao, takwimu zinaonyesha safari ya kubaki ligi kuu kwa timu hizo ni chache kutokana na ratiba ngumu ya mechi zilizosalia pamoja na mwenendo wao mbaya msimu huu.
Ruangwa Queens kwenye mechi nne zilizosalia itacheza dhidi ya JKT Queens Mei 27 kabla ya kuivaa Alliance Girls Mei 31, kisha Ceasiaa Queens Juni 5 na kumalizia dhidi ya Fountain Gate Princess Juni 10.
Kwa upande wa Bilo FC, wao watakuwa na kibarua dhidi ya Alliance Girls Mei 27 kabla ya kucheza na Ceasiaa Queens Mei 31, kisha kuvaana na Yanga Princess Juni 5 kabla ya kuhitimisha msimu dhidi ya Mashujaa Queens Juni 10.
Kwa namna msimamo ulivyo sasa, timu hizo zinahitaji kushinda mechi zao zilizosalia huku zikitegemea pia matokeo mabaya kwa wapinzani wao Bunda na Ceasiaa ambazo zina pointi 15 zipoteze mechi zilizosalia na kisha Ruangwa na Bilo ishinde mechi zote.
Changamoto kubwa kwa Bilo FC imekuwa safu dhaifu ya ushambuliaji baada ya kufunga mabao matano huku Ruangwa Queens ikiruhusu mabao sita.