Prime
Ishu ya kutumia waamuzi wa nje yachukua sura mpya, hoja sita zatajwa
UAMUZI wa kuleta waamuzi kutoka nje ya nchi kusimamia mechi kubwa, hususan Dabi ya Kariakoo kati ya Simba dhidi ya Yanga, umeendelea kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini, huku kukiwa na hoja sita.
Wapo wanaounga mkono wakiamini mpango huo unaongeza haki, pia kuna wanaohoji athari zake kwa maendeleo ya waamuzi wa ndani.
Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu wanachokifanya waamuzi hasa kwenye mechi za presha kubwa.
Hali hiyo imesababisha mamlaka za soka kuchukua hatua ya kutumia waamuzi wa kigeni kama njia ya kupunguza lawama na kulinda taswira ya ligi.
Ishu ya kutumia waamuzi kutoka nje kuchezesha mechi za Ligi Kuu Bara ilianza msimu uliopita katika Dabi ya Kariakoo iliyochezwa Juni 25, 2025 na Yanga kushinda 2-0.
Mchezo huo uliamuliwa na waamuzi kutoka Misri ambapo Amin Omar alikuwa mwamuzi wa kati, wasaidizi wake ni Mahmoud El Regal na Samir Mohamed, huku mwamuzi wa nne mezani akiwa Ahmed Elghandour. Kwa upande wa mtathimini waamuzi alikuwa Alli Mohamed kutoka Somalia.
Msimu huu pia katika Dabi ya Kariakoo iliyochezwa Mei 3, 2026 na zilitoka sare ya mabao 2-2, mwamuzi wa kati alikuwa Hamza El Fareq akisaidiwa na Lahsene Agaou na Hamza Massiri.
Nafasi ya mwamuzi wa nne ni Mustapha Kechaf, hawa wote ni raia wa Morocco. Lakini je, hatua hii ina manufaa ya kudumu au ni suluhisho la muda mfupi?
Kumekuwa na mambo kadhaa yanatajwa yakiwahusu waamuzi wa Tanzania kuchangia kutofanya vizuri kwa baadhi ya mechi.
ISHU ZA MALIPO
Kumekuwa na madai waamuzi wanaochezesha mechi za Ligi Kuu Bara wamekuwa wakicheleweshewa malipo yao na mmoja wa waamuzi amefichua imekuwa ikifika hadi miezi mitatu bila kulipwa.
“Kuna muda inaweza kupita miezi mitatu baadhi yetu hakuna malipo kitu ambacho kinaleta changamoto kubwa kwani wengi wetu tunategemea uamuzi kuendesha maisha kwani hakuna shughuli nyingine zinazotuingizia fedha,” alisema mwamuzi huyo ambaye hakupenda kuanikwa jina lake.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassoro Hamduni, alisema: “Hilo sio la kweli, waamuzi wanapata stahiki zao kwa wakati ikiwemo malipo, kama wangekuwa hawapati wanachotaka basi kungekuwa na malalamiko muda mrefu ila ukiona huu utulivu ujue mambo yako shwari.
“Kuhusu dabi au mechi kubwa kusimamiwa na waamuzi wa nje, utaona mara nyingi kuna presha kubwa ambayo inaanzia kwenye mitandao ya kijamii mpaka mechi husika kwa hiyo unafaida zake na uzui inaruhusiwa kisheria.”
Kwa mujibu wa vyanzo, mwamuzi wa Ligi Kuu Bara analipwa kati ya Sh300,000 hadi Sh400,000 kwa mechi, huku wale wanaokuja kutoka nje inakadiriwa kuwa Dola 1,000 (Sh2.6 milioni) kwa mechi.
ZANZIBAR BALAA
Kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Zanzibar, Waziri Sheha, katika Ligi Kuu Zanzibar, mwamuzi analipwa Sh20,000 hadi Sh30,000 kwa mechi moja visiwani humo.
Sheha aliyasema hayo Oktoba 2025 alipohojiwa na Mwanaspoti akibainisha kwamba, malipo hayo madogo inachangia kwa waamuzi kuchezesha kwa upendeleo kwani baadhi ya viongozi wa klabu huwashawishi kwa kuwapa fedha zaidi.
MAKONDA APIGILIA MSUMARI
Aprili 30, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika jijini Arusha, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliitaka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na wadau wa soka nchini kuongeza umakini katika usimamizi wa waamuzi, akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi muhimu wa kuhakikisha michezo inachezwa kwa haki na ufanisi.
Kauli ya Makonda ilikuja baada ya mwamuzi kutoka Kenya, Dickens Mimisa Nyagrowa aliyechezesha Dabi ya Kariakoo ambayo Simba iliichapa Yanga bao 1-0, Aprili 29, 2026 kwenye fainali ya Kombe la Muungano 2026, kusifiwa kwa kufanya vizuri, jambo ambalo amesisitiza siyo afya kwa soka la Tanzania.
Makonda alisema ameridhishwa na kiwango cha mchezo huo, huku akibainisha maeneo ya kuboreshwa hususani kwa waamuzi akiona kuna changamoto kubwa.
Aliitaka Bodi ya Ligi Tanzania kuongeza umakini katika upangaji na usimamizi wa waamuzi, akisisitiza umuhimu wa maadili na nidhamu katika kuhakikisha haki inatendeka uwanjani.
“Tunataka umakini wa hali ya juu kwa waamuzi wetu. Haipendezi kuona Watanzania wanampongeza refa wa nje wakati tuna waamuzi wetu. Hii inaonyesha kuna tatizo linalohitaji kufanyiwa kazi,” alisisitiza.
Makonda aliongeza kuwa malalamiko dhidi ya waamuzi yamekuwepo kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu hatua zichukuliwe ili kulinda hadhi ya soka la Tanzania.
Kwa mwaka huu wa 2026, Tanzania ina waamuzi 15 wenye beji za FIFA wanaochezesha Ligi Kuu Bara ambao ni Ahmed Arajiga, Nasir Siyah, Ramadhan Kayoko, Hery Sasii, Tatu Malogo na Amina Kyando, wakiwa ni waamuzi wa kati.
Waamuzi wasaidizi ni Mohamed Mkono, Hamdan Said, Kassim Mpanga, Frank Komba, Ramadhan Ally, Dismas Respicious, Glory Tesha, Zawadi Yusuph na Mary Selemani.
Hata hivyo, kuna hoja zimetajwa zikiunga mkono uletwaji wa waamuzi wa nje.
KUONGEZA UAMINIFU WA MECHI
Moja ya sababu kuu ya kuleta waamuzi wa nje ni kuongeza uaminifu wa matokeo. Dabi ya Kariakoo ni mechi yenye ushindani mkubwa na hisia kali kutoka kwa mashabiki. Kwa kutumia waamuzi wa nje, wadau wengi huamini nafasi ya upendeleo inapungua kwa kiasi kikubwa.
Hii husaidia kupunguza presha kwa waamuzi wa ndani ambao mara nyingi hukabiliwa na lawama kutoka pande zote mbili.
Katika mazingira hayo, waamuzi wa kigeni huonekana kuwa na uhuru zaidi wa kufanya maamuzi bila kuathiriwa na mazingira ya ndani.
UZOEFU NA UBORA WA KIMATAIFA
Waamuzi wengi wa kigeni wanaokuja kusimamia dabi huwa na uzoefu wa mashindano makubwa, iwe ni ligi za juu au michuano ya kimataifa. Uzoefu huo huwasaidia kudhibiti mechi kwa utulivu, kufanya maamuzi sahihi kwa haraka na kuhimili presha.
Hali hii inaweza kusaidia kuongeza ubora wa mchezo wenyewe, kwani maamuzi yenye utata hupungua na wachezaji hulazimika kucheza kwa nidhamu zaidi wakijua hakuna nafasi ya upendeleo.
JE, WAAMUZI WA NDANI WANANYIMWA FURSA?
Pamoja na faida hizo, hoja kubwa inayojitokeza ni kuhusu maendeleo ya waamuzi wa ndani. Ukweli ni kwamba, mechi kubwa kama dabi ndiyo jukwaa muhimu kwa waamuzi kujifunza na kukua.
Kwa kuwanyima nafasi hiyo, kuna hatari ya kuchelewesha ukuaji wao kitaaluma. Waamuzi wa ndani wanapobaki kusimamia mechi ndogo pekee, wanakosa uzoefu wa kuchezesha mazingira yenye presha kubwa, jambo ambalo ni muhimu katika safari yao ya kuwa waamuzi wa kiwango cha juu.
ATHARI YA KUJENGA UTEGEMEZI
Hatua ya kuzoea waamuzi wa nje inaweza pia kujenga utegemezi usio na afya katika soka la Tanzania. Klabu na mashabiki wanaweza kuanza kuamini haki inapatikana tu pale kunapokuwa na waamuzi wa kigeni.
Hii inaweza kudhoofisha imani kwa waamuzi wa ndani, hata wanapofanya vizuri. Mwishowe, mazingira hayo yanaweza kuua morali ya waamuzi wetu na kupunguza motisha ya kujifunza na kuboresha viwango vyao.
GHARAMA NA UWEKEZAJI
Kuna suala la gharama. Kuleta waamuzi kutoka nje kunahitaji fedha kwa ajili ya usafiri, malazi na posho. Fedha hizi zingetumika kuwekeza katika mafunzo ya waamuzi wa ndani, kuboresha miundombinu au hata kuanzisha teknolojia kama VAR. Kwa mtazamo wa muda mrefu, uwekezaji kwa waamuzi wa ndani unaweza kuwa na faida kubwa zaidi kuliko kutumia fedha nyingi kwa suluhisho la muda mfupi.
KAMA VIPI WACHANGANYWE
Badala ya kutegemea waamuzi wa nje pekee ni bora kutumia mfumo wa mchanganyiko. Kwa mfano, mwamuzi wa kati anaweza kuwa wa nje huku wasaidizi wake wakiwa wa ndani, au kinyume chake.
Mfumo huu unaweza kusaidia uhamishaji wa maarifa na uzoefu kwa waamuzi wa ndani, huku ukiendelea kulinda uaminifu wa mechi kubwa. Ni njia inayoweza kuleta uwiano kati ya haki ya sasa na maendeleo ya baadaye.
SIKIA HII
Mkufunzi wa Waamuzi Zanzibar anasema: “Inaua waamuzi wa ndani kisaikolojia lakini presha iliyoko kwenye dabi ya Simba na Yanga ni bora hata wachukuliwe wala wa nje maana wanakuja kufanya kazi na kuondoka bila lawama.
“Lakini saikolojia wanaharibika hawa wa kwetu, ila kwa sababu ya presha acha waje hao wa nje, shida inakuja hapo kwenye kuaminiwa kwenye michuano mikubwa ndio panapoleta changamoto ila kwa wanaojua siasa za hizi mechi hawawezi kulaumu.”
Akizungumzia uamuzi huo, mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay anasema haoni shida kwenye uamuzi huo na hatua hiyo inaongeza thamani ya mechi hiyo kuwa ni mchezo unaobeba hisia za wengi.
“Kila kitu kina faida na hasara, kwangu mimi sioni shida kwa kuwa kanuni zetu zinaruhusu kitu cha namna hii kufanyika. Tanzania hatutakuwa wa kwanza, ilianza kule Misri na sisi kama maamuzi hayo yatakubalika basi hakuna shida.
“Nadhani faida ya kwanza itakuwa tunaithibitishia dunia mchezo huu unabeba hisia za watu wengi. Ukweli, Tanzania kama wewe si Simba basi utakuwa Yanga, sasa katika kutoa haki ndiyo maana maamuzi kama haya yanakuja ingawa ina hasara yake ambayo ni gharama kubwa kufanikisha hili.”
Aliyekuwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas anasema hatua hiyo inalenga kuondoa lawama kwa waamuzi wanaoamua michezo hiyo mikubwa ambapo klabu hizo zitakubaliana na matokeo kirahisi pale wanapoona kutendewa haki.
“Nadhani ni hatua nzuri kwa TFF na TPLB kwenye uamuzi huo, ukweli ni kwamba hizi mechi kubwa zimekuwa na lawama nyingi pale zinapokuwa zinaamuliwa na waamuzi wa hapa ndani,” anasema Lucas.
“Wakati sisi tukiwa pale TFF ilikuwa ngumu kufanyika uamuzi kama huu, lakini wenzetu wameweza baada ya kubadilishwa kwa kanuni. Ukiangalia mchezo wa mwisho ambao uliamuliwa na waamuzi kutoka Misri, hakuna timu ambayo ilitoka ikalalamika 0imeonewa.
“Ukiangalia mchezo wa ligi dhidi ya timu hizi pale Zanzibar licha ya kumalizika kwa sare, lakini lawama zilikuwa nyingi kwa waamuzi na wengine mpaka wakafungiwa, kwa hiyo utaona hapo shida ilipo.
“Kwangu sioni shida, lakini ni wakati wa waamuzi wetu wa ndani kujifunza kutoka kwa kile kinachofanywa na wenzao wanapokuja kuamua mechi kama hizi. Waamuzi wetu tunakubali ni binadamu, lakini kuna wakati makosa yao yanatoka nje ya makosa ya kibinadamu. Wakijirekebisha tunaweza kuona wanakwenda hata kwenye fainali za Afrika au zile za dunia.”