Serengeti Boys uso kwa uso na vigogo Kombe la Dunia
Muktasari:
- Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 zitashirikisha idadi ya timu za taifa za vijana 48 kutoka mabara tofauti.
Baada ya kuwa timu ya kwanza Afrika kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 zitakazofanyika Qatar baadaye mwaka huu, Serengeti Boys inapaswa kujiandaa kuumana na baadhi ya timu zenye historia kubwa ya mafanikio katika mashindano hayo.
Serengeti Boys imefuzu mashindano hayo baada ya kujihakikishia kutinga robo fainali ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) yanayoendelea Morocco kufuatia ushindi wa mabao 3-0 iliyoupata dhidi ya Angola jana.
Ukiondoa bara la Afrika ambalo ni Serengeti Boys pekee iliyofuzu Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo, mabara mengine tayari yameshapata wawakilishi.
Katika timu hizo 38 zilizofuzu kutoka mabara mengine, timu zenye historia nzuri ya mashindano hayo ni Brazil, Mexico, Korea Kusini, Argentina, Hispania na Ufaransa.
Timu iliyofanikiwa zaidi ni Brazil ambayo imewahi kutwaa ubingwa mara nne, Mexico imechukua mara mbili, Korea Kusini imewahi kufika robo fainali mara nne na Argentina imewahi kushika nafasi ya tatu mara tatu, Hispania imemaliza mara nne katika nafasi ya pili na Ufaransa imewahi kutwaa ubingwa mara moja.
Serengeti Boys inakuwa timu ya kwanza ya kiume ya taifa ya Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia baada ya kujaribu bila mafanikio kufuzu katika fainali za 2017, 2019 na mwaka jana.
Pia hii ni mara ya kwanza kwa Serengeti Boys kukusanya idadi kubwa ya pointi katika Fainali za AFCON U17 ikivunja rekodi ya kizazi cha mwaka 17 kilichokusanya pointi nne.
Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakafanyika Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13 mwaka huu.