Shikangwa: Tulijua mabeki Yanga ni wazito, watachanganyikiwa
Muktasari:
- Simba ilikuwa mwenyeji kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara uliopigwa leo katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuondoka na ushindi wa mabao 2-1.
MFUNGAJI wa mabao mawili kwenye mechi ya dabi ya wanawake, Jentrix Shikangwa wa Simba Queens amesema walijua Yanga ina udhaifu eneo la mabeki na huchanganyikiwa dakika 15 za mwanzo wakipelekewa presha.
Simba ilikuwa mwenyeji kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara uliopigwa leo katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuondoka na ushindi wa mabao 2-1.
Shikangwa ameifunga Yanga mabao hayo na kumfanya afikishe saba akiwa mmoja wa wachezaji aliyewafunga Wananchi mara nyingi zaidi tangu ajiunge na Simba msimu wa 2022/23 akitokea Vihiga Queens ya kwao Kenya.
Anayeshikilia rekodi ya kuifunga mabao mengi zaidi timu hiyo ni Mwanahamisi Omary 'Gaucho' ambaye kwa sasa anakipiga Tausi FC aliyeifunga mabao 10.
Gaucho pekee hadi sasa anashikilia rekodi ya kufunga hat-trick kwenye ligi ya wanawake, msimu wa 2020/21 tangu hapo hakuna mchezaji aliyewahi kufunga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shikangwa amesema walitumia vizuri udhaifu wa mabeki wa Yanga kipindi cha kwanza hususan dakika 15.
"Tumetumia udhaifu wao ambao kwenye safu ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa kipindi cha kwanza na mabeki wao ni wazito, lakini pia dakika 15 za kwanza wanakuwa wamechanganyikiwa hivyo tulitumia udhaifu huo," amesema Shikangwa na kuongeza:
"Bado nina mechi sita na bado napambana kuhakikisha nafanya vizuri. Nina imani nitakuwa bora. Nimekuwa na bahati ya kufunga Chamazi kwa sababu ni uwanja mkubwa, wengine wanashindwa kuutumia sisi tunafanikiwa."
Mabao hayo yanamfanya Shikangwa aendelee kubaki nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji akifunga 14 nyuma ya Jeanine Mukandayisenga wa Yanga anayeongoza na mabao 19.
Huu ni msimu wa nne wa mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Starlets' tangu ajiunge na Wekundu wa Msimbazi msimu wa 2022/23.
Msimu wake wa kwanza kuitumikia Simba Queens aliifungia mabao 17 kwenye mechi 13 akiibuka na kiatu cha ufungaji bora na uliofuata alicheza nusu msimu akifunga mabao manane kwenye mechi tisa.
Msimu wa 2024/25 ukiwa wa tatu alifunga mara 23 kwenye mechi 18 na huu hadi sasa ametupia mabao 14.