Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usiku wa hukumu Zanzibar, Yanga kutetea au Simba kutwaa ubingwa Muungano Cup?

Muktasari:

  • Zikitoka kucheza mechi mbili za hatua ya robo fainali na zile za nusu, timu hizo kongwe zimeonyesha kiwango kikubwa zikishinda ndani ya dakika 90 na sasa zinakwenda kuamua nani atakuwa bingwa wa taji hilo, mchezo utakaopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, hapa Zanzibar.

LEO ni siku ya hukumu hivyo usilale mapema. Ikifika saa 2:15 usiku hakikisha umeshapata chakula na kumaliza shughuli zako zote, kisha jicho lako litazame mechi kubwa ya siku wakati Yanga na Simba zitakapokuwa zinamalizana kwenye Fainali ya Kombe la Muungano.

Hapa lazima mtu apigwe, kisha atakwenda kujiuliza Jumapili katika Dabi nyingine pale Dar es Salaam.

Zikitoka kucheza mechi mbili za hatua ya robo fainali na zile za nusu, timu hizo kongwe zimeonyesha kiwango kikubwa zikishinda ndani ya dakika 90 na sasa zinakwenda kuamua nani atakuwa bingwa wa taji hilo, mchezo utakaopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, hapa Zanzibar.

Yanga ilizing’oa Muembe Makumbi City kwenye robo fainali ikishinda 4-0, kisha akafuata Azam kwenye nusu fainali nayo ikatolewa mshindanoni kwa kipigo cha mabao 2-1.

Simba nayo haikuingia kinyonge, ikaichapa Mafunzo kwenye robo fainali kwa bao 1-0, kisha ikalipa kisasi kwa kuing’oa Mlandege kwa kuishushia kipigo cha mabao 3-0.

Yanga imeonyesha makali kwenye safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Prince Dube aliyefunga mabao matatu ambayo ni nusu ya mabao yote yaliyofungwa na timu hiyo kwenye mashindano haya.

Ubora wa Yanga pia upo kwenye kiungo ambapo eneo la ukabaji usisahau kazi bora ya Mohammed Damaro ambaye kazi yake nzuri ya kupokonya mipira kisha kufanyika kwa mashambulizi ya haraka ikahusika kutengeneza mabao mawili katika mechi hizo mbili akisaidiana na Duke Abuya.

Juu ya Damaro kuna Allan Okello ambaye amekuwa mwiba kwa kutengeneza pasi za mwisho zilizozaa mabao, akiwa na asisti mbili mpaka kikosi hicho kinakwenda kucheza fainali.

Dosari pekee kwa Yanga ipo kwenye ukuta wake ambao uliruhusu bao moja katika mechi hizo mbili ambapo utatakiwa kujiimarisha kabla ya kukutana na Simba.

Hata hivyo, Yanga inaweza kurudi na ukuta wake wa mabeki Israel Mwenda kulia, katikati wakiwa Frank Assinki na Ibrahim Hamad ‘Bacca’, kisha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kushoto.

Simba nao safu yao ya ushambuliaji ipo moto ikitegemea nguvu ya mshambuliaji wake Seleman Mwalimu ambaye naye amefunga nusu ya mabao kwa timu hiyo akiweka wavuni mawili wakati Simba ikiwa na jumla ya mabao manne.

Pale kwenye kiungo tegemea kuona tena ubora wa Yusuph Kagoma na Alassane Kanté ambao wameifanya Simba kuwa ngumu kupitika kwenda kuwaona mabeki wa kati, lakini juu ya watu hao wawili kuna fundi Clatous Chama ambaye naye ana asisti zake mbili sawa na Okello.

Ukuta wa Simba umeonyesha ubora mkubwa kabla ya kucheza fainali ukiwa ndio pekee haujaruhusu bao lolote mpaka unakwenda kukutana na Yanga ukitarajiwa kupanguliwa na kurudishwa Shomari Kapombe kulia, kati wakiwa Rushine De Reuck na Ismael Toure, huku Nickson Kibabage akiwa kushoto.

Timu zote hazitakuwa na akili ya kuwapa nafasi vijana tena kwani kule pembeni Yanga itategemea nguvu ya Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, wakati Simba itakuwa na mafundi wake wawili Libasse Gueye na Anicet Oura.

Mara ya mwisho timu hizo mbili zilikutana hapahapa Uwanja wa New Amaan, mchezo ukimalizika kwa sare isiyo na mabao, kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini Simba ikionekana kwamba ilikuwa bora kushinda Yanga, hatua ambayo imeibua kejeli kwamba katika fainali hii itajulikana nani aliponea chupuchupu.

Kumbuka baada ya mchezo huu wa fainali timu hizi zitakuwa na dakika 90 zingine kwenye Ligi Kuu Bara zikitarajiwa kukutana tena Mei 3 mwaka huu, yaani siku nne kutoka leo pale Uwanja wa Meja Generali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.

Yanga ndio bingwa mtetezi wa Kombe la Muungano alipolichukua msimu uliopita pale Pemba ambapo itaingia kwenye fainali hiyo ikitafuta taji lake la nane kihistoria kwenye mashindano haya, ikiwa ndio timu iliyochukua mataji mengi mara saba miaka ya 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000 na 2025 kabla ya fainali ya leo.

Simba mara ya mwisho kuchukua ubingwa huu ilikuwa mwaka 2024 ambapo itakuwa na akili mbili kwenye fainali hii, kwanza kumaliza ukame wa mataji ambao ni mwaka wa pili sasa haijabeba taji lolote tangu ibebe kombe hili.

Akili ya pili ya Simba itakuwa kujiongezea historia katika mashindano haya ikienda kutafuta ubingwa wake wa saba baada ya kuchukua mara sita kwenye miaka ya 1993, 1994, 1995, 2001, 2002 na 2024.

Fainali hizi zitakuwa na historia nzuri kwa makocha wa timu zote mbili, huku Pedro Goncalves wa Yanga akifukuzia taji lake la pili baada ya kubeba Kombe la Mapinduzi 2026, wakati Steve Barker wa Simba litakuwa la kwanza kwake.

Bingwa wa fainali hizi atajichukulia kombe na kiasi cha Sh150 milioni kama zawadi wakati mshindi wa pili atajipatia Sh100 milioni.

Nje ya uwanja kila upande mashabiki wake wanatamba kwa rekodi zake, Simba ikitaka kusitisha vipigo dhidi ya mtani wake, ikiringia ufundi wa kocha wake na kikosi chao kipya, ikisema safari hii lazima wakafanye kweli.

Yanga nayo mashabiki wake wanatamba na rekodi zao ikisema itakwenda kuipiga Simba mara ya saba baada ya kupona kwenye mchezo uliopita wa ligi walipotoka 0-0. Kabla ya hapo, Yanga imeifunga Simba mara sita mfululizo.

Tangu mara ya mwisho Simba iiifunge Yanga kwa penalti 3-1 katika Ngao ya Jamii, Agosti 13, 2023, imepoteza mechi sita mfululizo kabla ya ile ya saba kutoka 0-0.

Ubora wa vikosi vyote mbili, utaibua ushindani mkali ndani ya uwanja kama tulivyoshuhudia mara ya mwisho zilipotoka 0-0 uwanjani hapo.

Upande wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ile vita yake na Libase Gueye itaendelea baada ya kuishuhudia awali, safari hii tutaishuhudia leo, kisha Jumapili endapo wachezaji hao wote wakiwa fiti.

Pia Anicet Oura amekuwa hatulii uwanjani, anacheza kulia na kushoto, hivyo atakutana na Tshabala, pia wakati mwingine Israel Mwenda.

Pia mabeki wa Simba, Shomari Kapombe na Nickson Kibabage watakuwa na kazi kubwa mbele ya Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na hata Allan Okello.

Pale kati ndiyo balaa. Mohamed Damaro na Duke Abuya wanaimarisha kiungo cha Yanga, wanakwenda kupimana ubavu na Yusuph Kagoma na Alassane Kante. Kila mmoja anataka kutawala ili kurahisisha mambo eneo la ushambuliaji lifanye kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi kwani viungo wakizingua, mipira haiendi mbele.