Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Amorim achekelea kuondoka Onana

Muktasari:

  • Kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon, amejiunga na klabu ya Uturuki ya Trabzonspor kwa mkopo wa msimu mzima.

MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim anaamini kuondoka kwa kipa Andre Onana ni jambo muhimu sana katika mchakato wake wa kujenga upya kikosi.

Kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon, amejiunga na klabu ya Uturuki ya Trabzonspor kwa mkopo wa msimu mzima.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun, uhusiano kati ya Onana na kocha wa Man United, Amorim, ulivurugika kabisa ndani ya mwezi uliopita.

Chanzo kimoja kilisema: “Ilikuwa kana kwamba Andre yupo tu, lakini hakuwa sehemu ya roho ya timu. Amorim alikerwa na Onana, mwenye umri wa miaka 29, baada ya kupata jeraha la msuli wa paja mwanzoni mwa maandalizi ya msimu mpya ambalo  inadhaniwa lilisababishwa na tukio lake la kucheza kwenye uwanja wa matope nyumbani kwao Cameroon Juni mwaka huu.”

Onana ni miongoni mwa nyota kadhaa ambao Amorim amewaondoa katika kikosi chake katika msimu huu kwa sababu hawapo katika mipango yake.

Hadi sasa tayari amewaruhusu Marcus Rashford, Jadon Sancho, Alejandro Garnacho na Antony kuondoka. Na beki wa kushoto Tyrell Malacia yuko karibu kujiunga na  Eyupspor ya Uturuki kwa mkopo.

Kocha huyo wa Man United anaamini kuwa ameondoa vizuizi na kufungua njia ya mustakabali bora wa timu.

Onana aliachwa nje ya kikosi cha kwanza kwenye mechi za mwanzo za Ligi Kuu dhidi ya Arsenal na Fulham. Kisha akafanya makosa kadhaa kwenye kipigo cha aibu cha Carabao Cup dhidi ya Grimsby, jambo lililomfanya aachwe tena kwenye mchezo uliofuata wa ligi dhidi ya Burnley.

Katika dakika za mwisho za dirisha la usajili, Man United ilifanya usajili wa haraka ikitumia Pauni 18.2 milioni kumchukua kipa chipukizi raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 23, Senne Lammens.

Chanzo pia kiliiambia The Sun kwamba Amorim na benchi lake la ufundi walihisi Onana hana ari wala dhamira ya kupigania timu na alionekana akikwepana kabisa na kocha wake hata kwenye mazoezi.

Kwa hali hiyo, Amorim hakuwa na tatizo lolote zaidi ya kumuacha Onana aondoke, akibaki na Lammens, kipa kutoka Uturuki, Altay Bayindir, na mkongwe Tom Heaton mwenye miaka 39.

Amorim sasa analazimika kuamua iwapo ampe Lammens nafasi ya kwanza ya kucheza kwenye uwanja wa Etihad itakapocheza mechi ya Manchester dabi dhidi ya Man City Jumapili hii, au abaki na Bayindir

Onana pia alipewa lawama zaidi baada ya kipigo cha 1-0 dhidi ya Cape Verde siku ya Jumanne, kilichovunja matumaini ya Cameroon ya kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia.

Kipa huyo alihusishwa moja kwa moja na bao la ushindi la Dailon Livramento.