Amorim ataja kinachoitafuna Man United
Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Ureno alianza vibaya msimu na sasa Mashetani Wekundu wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi sita na pia wameshatolewa kwenye Kombe la Carabao na timu ya Ligi Daraja la Nne, Grimsby Town.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amesema moja kati ya vitu ambavyo kikosi chake kinakosa ni wachezaji watukutu wenye ‘roho mbaya’ uwanjani.
Kocha huyo raia wa Ureno alianza vibaya msimu na sasa Mashetani Wekundu wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi sita na pia wameshatolewa kwenye Kombe la Carabao na timu ya Ligi Daraja la Nne, Grimsby Town.
Akizungumzia kinachoisumbua timu hiyo kwa sasa, Amorim amesema Manchester United haihitaji tu wachezaji viongozi, bali pia inataka wabunifu na wenye utukutu au wale wanaokuwa kama vichaa uwanjani ambao wanaweza kubadili mchezo pale mambo yanapokwenda vibaya.
“Tunahitaji wachezaji viongozi, lakini wakati mwingine nafikiria tunahitaji pia watu wenye ukichaa kidogo. Matheus Cunha yupo hivyo. Ni mchezaji mzuri, lakini hajali wewe ni nani. Anakuwa na ukichaa na akiwa anagombania mpira na wewe atafanya chochote ili aupate. Hii ni aina ya tabia tunazohitaji,” amesema Amorim alipofanya mahojiano na TNT.
“Kwa upande wa viongozi nafahamu tuna mtu kama Bruno Fernandes au hata Harry Maguire aliyewahi kuwa nahodha hapa. Lakini mambo yanapokwenda vibaya unaona tunakosa kabisa kitu kutoka kwao, timu yote huwa inakata tamaa walau sasa utamwona Bryan Mbeumo akiwa na akili tofauti na hata Cunha ukimwangalia utaona kama ana hasira, lakini huwa anajaribu kutoa ujumbe kwa wenzake kwamba tuamke tucheze mpira. Hiki ndo tunahitaji katika nyakati ngumu.
“Tunapaswa kusahau yaliyopita na wakati mwingine tunahitaji mtu wa aina hiyo (Cunha), haijalishi dunia inaweza kuwa inateketea, lakini yeye hajali. Wakati mwingine sio kiongozi tu anayehitajika, bali pia wachezaji wabunifu wanaocheza bila kukataa tamaa au kuwa na hofu,” amesema.
Licha ya kuwasifia Mbeumo na Cunha takwimu za mastaa hao bado si nzuri. Cunha bado hajatoa asisti hata moja huku Mbeumo akiwa amefunga bao moja pekee katika ligi na jingine la Kombe la Carabao dhidi ya Grimsby Town.
Kwa sasa Amorim anakabiliwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wanaotaka afukuzwe kazi huku kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate akitajwa kuwa anaweza kuchukua mikoba yake ikiwa hilo litatokea.