Arsenal yamkomalia beki wa PSG Mbemba
Muktasari:
- Mbemba mwenye miaka 18 amepewa ofa ya mkataba mpya na PSG, lakini yuko wazi kuhamia klabu kubwa ya Ligi Kuu England. Arsenal wamemueleza mpango wao wa maendeleo kwa kumtolea mfano wa mafanikio ya William Saliba, ambaye aliendelea kukua baada ya kutolewa kwa mkopo katika Olympique Marseille.
Arsenal wameanza mawasiliano ya kumshawishi beki wa Paris Saint-Germain, Emmanuel Mbemba, kujiunga nao kwa uhamisho wa bure msimu huu.
Mbemba mwenye miaka 18 amepewa ofa ya mkataba mpya na PSG, lakini yuko wazi kuhamia klabu kubwa ya Ligi Kuu England. Arsenal wamemueleza mpango wao wa maendeleo kwa kumtolea mfano wa mafanikio ya William Saliba, ambaye aliendelea kukua baada ya kutolewa kwa mkopo katika Olympique Marseille.
Inaelezwa kuwa Mbemba anapendelea kujiunga na Arsenal kutokana na utulivu na mafanikio ambayo klabu hiyo imepata chini ya kocha Mikel Arteta. Arsenal pia wanamwona kama chaguo la muda mrefu katika nafasi ya beki wa kushoto, licha ya kucheza zaidi kama beki wa kati katika timu za vijana za PSG.
Rio Ngumoha
Bayern Munich wanaonyesha nia ya kumsajili winga chipukizi wa Liverpool, Rio Ngumoha.
Liverpool hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo wa miaka 17, ambaye amecheza mechi 19 katika msimu wake wa kwanza wa mafanikio. Ngumoha anatajwa kuwa mmoja wa vipaji vikubwa zaidi barani Ulaya tangu alipojiunga na Liverpool kutoka Chelsea mwaka 2024.
Baada ya msimu mzuri, alipendekezwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora Kijana wa Ligi Kuu England na pia aliitwa kwenye kikosi cha mazoezi cha England kuelekea Kombe la Dunia.
Nick Pope
Leeds United na Ipswich Town wanapambana kuwania saini ya kipa wa Newcastle United, Nick Pope.
Kipa huyo wa kimataifa wa England mwenye miaka 34 anafikiria kama ataondoka Newcastle baada ya miaka minne au apambane kubaki katika kikosi cha kwanza.
Wakati huo huo, Newcastle wanatarajiwa kumsajili kipa wa timu ya vijana ya Ufaransa, Ewen Jaouen, kutoka Stade de Reims. Pia kocha Eddie Howe anafuatilia makipa wengine kama Bart Verbruggen wa Brighton & Hove Albion na James Trafford wa Manchester City.
Thomas Berenbruch
Ripoti kutoka Italia zinaeleza kuwa Inter Milan wako tayari kumruhusu kiungo wake Thomas Berenbruch kujiunga na Cagliari Calcio.
Hata hivyo, Inter wanataka kuweka kipengele kitakachowapa nafasi ya kumrejesha baadaye, kama walivyofanya kwa Aleksandar Stankovic.
Kocha wa Cagliari, Fabio Pisacane, anavutiwa na Berenbruch baada ya kumuona mara nyingi alipokuwa akizinoa timu za vijana.
Zadok Yohanna
Brighton & Hove Albion wamekubaliana kumsajili winga wa Nigeria, Zadok Yohanna, kutoka AIK Stockholm kwa ada ya pauni21.5 milioni.
Mchezaji huyo mwenye miaka 18 atasaini mkataba wa miaka mitano mara dirisha la usajili litakapofunguliwa rasmi.
Kocha Fabian Hurzeler alisema anaamini Yohanna ana uwezo wa kuleta tofauti kubwa katika eneo la ushambuliaji.
Morgan Rogers
Nyota wa Aston Villa, Morgan Rogers, anaendelea kuvutia klabu kubwa kabla ya dirisha la usajili. Arsenal wanatajwa kuwa wamemweka juu katika orodha yao ya wachezaji wanaowahitaji msimu huu, huku pia Chelsea na Manchester City zikifuatilia maendeleo yake.
Rogers amekuwa na msimu bora akiwa Aston Villa, akifunga mabao 14 na kutoa pasi 12 za mabao katika mashindano yote.
Dani Olmo
Nyota Dani Olmo amekanusha uvumi wa kujiunga na Arsenal na kusisitiza kuwa ataendelea kubaki katika FC Barcelona. Kiungo huyo mwenye miaka 28 amesaidia Barcelona kushinda taji la La Liga kwa misimu miwili mfululizo na hana mpango wa kuondoka Camp Nou.
Licha ya taarifa kwamba Arsenal walikuwa wakijiandaa kutoa euro60 milioni kwa ajili yake, Olmo amesema anataka kuzingatia kampeni ya Hispani katika Kombe la Dunia.
Robert Lewandowski
Aliyekuwa mshambuliaji wa Italia, Giuseppe Rossi, ameishauri Manchester United kufanya juhudi za kumsajili Robert Lewandowski.
Lewandowski mwenye miaka 37 atakuwa mchezaji huru mwezi ujao baada ya mkataba wake na Barcelona kumalizika. Mshambuliaji huyo wa Poland anaondoka Barcelona baada ya miaka minne yenye mafanikio makubwa, akiwa amefunga mabao 120 katika mechi 193 na kushinda mataji matatu ya La Liga, matatu ya Kombe la Spanish Super pamoja na taji la Copa del Rey.
Ikiwa Manchester United watafanikiwa kumpata, watakuwa wameongeza uzoefu mkubwa na uwezo wa kufunga mabao katika safu yao ya ushambuliaji.