Gerrard: Liverpool hakuna visingizio
Muktasari:
- Jana kikosi hicho cha Kocha Arne Slot kilipoteza kwa mabao 4-1 katika dimba la Anfield dhidi ya PSV kwenye Ligi ya Mabingwa na jumla inakuwa imepoteza mechi tisa kati ya 12 zilizopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: LEJENDI wa Liverpool, Steven Gerrard amesema hakuna 'visingizio' kutokana na msururu mbaya wa matokeo ya timu hiyo.
Jana kikosi hicho cha Kocha Arne Slot kilipoteza kwa mabao 4-1 katika dimba la Anfield dhidi ya PSV kwenye Ligi ya Mabingwa na jumla inakuwa imepoteza mechi tisa kati ya 12 zilizopita.
Rekodi hiyo ni mbaya zaidi kwa klabu hiyo tangu Novemba 1953 hadi Januari 1954 na ndiyo ilipata matokeo ya aina hiyo na wakati huo pia ndiyo ilikuwa mara ya mwisho majogoo hao kushuka daraja.
Akizungumza na TNT Sports baada ya mechi dhidi PSV, mkongwe huyo, 45, amesema: "Kila tukipoteza mechi, utasikia watu wanasema timu yetu ina shida au kuna mgogoro. Sipendi kutumia maneno haya kwa sababu kwangu ninaamini tunapitia tu kipindi kifupi cha mpito, hatuhitaji muda mwingi ili kurudi katika nafasi yao. Bado wana wachezaji wazuri mno na wengi wa kikosi hiki walitwaa ubingwa msimu uliopita. Tukisema hivyo, itakuwa ni kukosa heshima kwa baadhi ya wachezaji waliojitoa kwa ajili ya kuleta mafanikio katika klabu hii."
Hata hivyo, Gerrard amesema Slot anahitaji kupata dawa haraka ili kuzuia timu isiendelee kudidimia na kurudi katika mstari.
Kipigo dhidi ya PSV pia kiliifanya Liverpool kuifikia rekodi yao mbaya ya Septemba 1992, ya kupoteza mechi tatu mfululizo kwa mabao matatu au zaidi.
Rekodi hiyo ilianza kwa kipigo cha maba 3-0 nyumbani dhidi ya Nottingham Forest na kipigo cha 3-0 ugenini dhidi ya Manchester City.
Kocha Slot anaamini wachezaji wake watapambana na kushinda mechi ijayo dhidi ya West Ham katika Ligi Kuu England na kurudisha morali.
Tangu mwaka 2017, West Ham imepata ushindi mara moja tu dhidi ya Liverpool, wakifanya hivyo mwaka 2021 ambapo ilishinda mabao 3-1.