KIKAO KIZITO! Mastaa Liverpool wateta, wamwondoa Arne Slot
Muktasari:
- Gakpo amefichua kuwa hoja kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kuhimizana kila mchezaji awajibike badala ya kumwacha kocha Arne Slot kubeba lawama zote kwa kile kinachoendelea katika timu kwa sasa.
LIVERPOOL, ENGLAND: STAA wa Liverpool, Cody Gakpo amefichua kuwa wachezaji wa Liverpool walifanya kikao cha dharura cha kuchanana ukweli siku ya Jumapili ikiwa ni katika juhudi zao za kuhakikisha wanarudi katika mstari baada ya kuwa na msimu mbaya.
Gakpo amefichua kuwa hoja kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kuhimizana kila mchezaji awajibike badala ya kumwacha kocha Arne Slot kubeba lawama zote kwa kile kinachoendelea katika timu kwa sasa.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi alisema ni lazima kuwe na uaminifu katika timu baada ya majogoo hao kupata kichapo cha nyumbani cha mabao 3-0 kutoka kwa Nottingham Forest wikiendi iliyopita.
Gakpo ambaye amewahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England akiwa na Liverpool, alisema: “Baada ya mechi kulikuwa na kuna hali ya aibu kwetu, kwa sababu tumepoteza nyumbani mbele ya mashabiki wetu.
“Tunajua wao huwa wako kutusaidia kwenye kila hali mbaya na nzuri, lakini pia tunapaswa kuwapa wanachohitaji. Sitaki kusema kama wachezaji tulikasirika, hapana. Tulijaribu kuzungumza na kuambiana ukweli kuhusu kile tunachopaswa kufanya ili kuwa bora uwanjani.”
Ripoti zinaeleza kuwa majadiliano hayo ya kupeana ukweli yaliandaliwa na wachezaji wenyewe bila hata ya uwepo wa kocha.
Gakpo mwenye umri wa miaka 26, alisisitiza kuwa lawama haziwezi kumwangukia kocha Slot peke yake bali wote wanapaswa kuwajibika.
“Kila mtu anatambua kuwa tunapaswa kubeba mzigo wa ndani na nje ya uwanja. Haya yalikuwa mazungumzo ya kawaida baina ya wachezaji, siyo mkutano rasmi na tukaambizana kwamba tunahitaji kuwajibika. Tulichanana ukweli kwa sababu tukioneana aibu, hatuwezi kufika na kusingekuwa na tija ya kikao.”
Beki wa majogoo hao naye alipoulizwa kuhusu kiwango cha timu yao alisema moja kati ya vitu wanavyokosa ni kushinda mechi kwa kutokea nyuma pale wanapotanguliwa na wapinzani, jambo ambalo walilifanya sana msimu uliopita.
Licha ya msimu mgumu, Liverpool imepata ushindi muhimu, kama ule wa bao 1-0 dhidi ya Real Madrid kwenye Uwanja wa Anfield katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema mwezi huu.