Man United sharti icheze Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kufanikisha hili
Muktasari:
- Anderson anavutiwa na Man United, lakini vyanzo vya kuaminika vinasema klabu hiyo haitaweza kushindana na vinara wa mbio za usajili, Manchester City, katika mshahara wa mchezaji huyo kama hawatacheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United italazimika kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kama kweli inataka kuwa na nafasi ya kuwasajili viungo wawili matata kabisa wa England, Elliot Anderson na Adam Wharton.
Anderson anavutiwa na Man United, lakini vyanzo vya kuaminika vinasema klabu hiyo haitaweza kushindana na vinara wa mbio za usajili, Manchester City, katika mshahara wa mchezaji huyo kama hawatacheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 aliwavutia wengi alipocheza vizuri dhidi ya Man United wakati Nottingham Forest ilipotoa sare ya mabao 2-2 katika Uwanja wa City Ground mapema msimu huu.
Yeye ni mmoja wa viungo kadhaa waliothibitisha uwezo wao katika Ligi Kuu England na tangu wakati huo Man United imekuwa ikimfuatilia.
Anderson anatarajiwa kuanza pamoja na Declan Rice katika kikosi cha England kitakachokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kumvutia kocha Thomas Tuchel.
Kwa upande wa Wharton, kufuzu kwa Man United kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni muhimu sana kama wanataka kuwa na nafasi ya kumpata.
Mchezaji huyo mwenye miaka 22 anatarajiwa kuondoka Crystal Palace katika dirisha lijalo la usajili la majira ya kiangazi, lakini anataka kujiunga tu na klabu inayoshiriki mikikimikiki hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wharton aliichezea vizuri wakati Palace ilipoifunga Man United 4-0 na 2-0 katika misimu ya hivi karibuni. Pia alianza katika Uwanja wa Old Trafford wakati Man United iliposhinda kwa taabu mabao 2-1 wiki iliyopita.
Kwa sasa Man United iko kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England, lakini ilipata kipigo chao cha kwanza chini ya kocha wa muda, Michael Carrick dhidi ya Newcastle United, Jumatano usiku.
Mechi yao ijayo watakabiliana na Aston Villa, ambayo pia ipo kwenye mchakamchaka wa kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku ikitambua ushindi ni lazima baada ya kupoteza mechi tatu na kutoa sare mbili katika mechi zao sita zilizopita kwenye Ligi Kuu.
Nafasi ya tano ina uwezekano mkubwa wa kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa timu za Ligi Kuu England msimu ujao kutokana na ligi hiyo kuwa na timu sita zilizoingia katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya Ulaya msimu huu.
Man United imeweka kipaumbele kusajili kiungo katika dirisha la usajili la majira ya joto, baada ya kusajili viungo wawili tu wa kati katika kipindi cha miaka nane iliyopita.
Casemiro ataondoka klabuni hapo mkataba wake utakapomalizika, Juni mwaka huu. Mbrazili huyo wenye miaka 34 alionekana kuwa na kiwango cha chini kabla ya kutolewa dakika ya 61 katika mechi dhidi ya Newcastle.
Wakati huo huo, Kobbie Mainoo bado hajakubali mkataba mpya wa muda mrefu baada ya kukataa ofa ya kwanza ya Man United mwaka jana, huku Manuel Ugarte akiwa hajawa na mwanzo mzuri katika miezi yake 18 ya kwanza katika kikosi hicho.
Kwa sasa Ugarte, Mainoo na Casemiro ndio viungo wa kati pekee wanaotambulika katika kikosi cha Man United baada ya klabu hiyo kuzingatia zaidi kuimarisha safu ya ushambuliaji katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Man United pia waliulizia kuhusu kiungo wa Brighton, Carlos Baleba katika dirisha lililopita, lakini Mcameruni huyo amekuwa na msimu mgumu katika Uwanja wa Amex.
Baleba mwenye miaka 22 ametolewa wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza mara nne msimu huu na pia alitolewa dakika ya 22 katika kipigo cha 1-0 dhidi ya Aston Villa mwezi uliopita.
Kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, ambaye aliitwa kwenye kikosi cha mwisho cha England mwezi Novemba, pia anavutiwa na Man United.