Prime
Siri ya kivuli cha Mwameja na penalti ya Seleman Mwalimu
JANA Jumatano usiku, Simba ilibeba Kombe la Muungano likiwa ni taji lao la kwanza msimu huu baada ya kuifunga watani zao, Yanga bao 1-0, shukrani kwa penalti ya Seleman Mwalimu iliyopeleka kilio Jangwani.
Ubingwa huo umeifanya Simba kuifikia Yanga kwa idadi ya makombe zikilingana kwa kubeba mara saba kila moja na Wanajangwani hao ndio walikuwa watetezi wa taji hilo linaloshindaniwa kuadhimisha Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani (Unguja na Pemba).
Hii ni mara ya Sita kwa miamba hii watani hawa kukutana kwenye mechi ya fainali visiwani Zanzibar katika mashindano tofauti na katika tano zilizopita mambo yalikuwa hivi.
YANGA 2-0 SIMBA - 1975
Hii ilikuwa fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame), iliyofanyika Januari 13, 1975 kwenye Uwanja wa Amaan ambao ulitoka kuzinduliwa mwaka 1972. Simba iliingia kwenye mashindano hayo kama bingwa mtetezi baada ya kutwaa Kombe mwaka 1974 kwenye mashindano ya kwanza kabisa yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mechi hii iliyoanza saa mbili na robo usiku, ilikuwa ya kwanza kwa Yanga na Simba kuchezwa usiku. Yanga ilishinda 2-0 kwa mabao ya Sunday Manara na Gibson Sembuli. Baada ya hii mechi, mgogoro mkubwa ukaibuka Simba kwa wanachama kumlaumu mwenyekiti wao, Hassan Haji alitoa siri kwa Sunday Manara ili awafunge.
Manara, ambaye ni baba yake Haji Manara, alikuwa nyota wa Yanga aliyemuoa binti wa Hassan Haji.
Kabla ya fainali hii, Yanga na Simba zilikutana kwenye fainali ya klabu bingwa ya Taifa mwaka 1974 mjini Mwanza na Wekundu wa Msimbazi ilifungwa mabao 2-1, wafungaji wakiwa ni Manara na Gibson Sembuli.
Kwa hiyo Manara alipofunga tena Zanzibar, wanachama wa Simba wakasema mwenyekiti wao amempa siri mkwewe...kwa nini alikuwa hatufungi kabla hajaoa binti yako? Walihoji. Hassan alitoka Simba na akaenda kuanzisha Klabu ya Nyota Nyekundu.
SIMBA 1-1 YANGA (penati 6-5)- 1992
Watani wakakutana tena mwaka 1992 kisiwani Unguja kwenye Uwanja wa Amaan kuwania Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Kama ilivyokuwa fainali ya mwaka 1975, Simba iliingia kwenye mashindano hayo kama bingwa mtetezi kwa kushinda Kombe mwaka 1991 Dar es Salaam.
Kocha wa Yanga, marehemu Syllersaid Mziray alionyeshwa kadi nyekundu, akipinga kutolewa kwa kadi kama hiyo kwa beki wake wa kushoto, Kenneth Mkapa.
Simba ilifunga bao la kuongoza lililowekwa kimiani na Hussein Marsha, kabla Said Mwamba Kizota hajasawazisha.
Matokeo yakabaki 1-1 hadi dakika 120 ndipo changamoto ya mikwaju ya penati ilipohusika na Simba ikashinda kwa penalti 5-4 baada ya David Mwakalebela wa Yanga kupoteza yake.
Katika mechi hiyo Joseph Lazaro wa Yanga alikataa kupiga penalti yake ndipo Mwakalebela akachukua nafasi yake na wakati anasimama, kipa wa Simba, Mohamed Mwameja akaanza kushangilia na kuwahamasisha mashabiki wao washangilie pia.
Mwakalebela kuona hivyo, akaingiwa hofu, akakaa chini...akasimama na kukaa tena...akawa tayari ameshapoteza kujiamini. Alipopiga, Mwameja akaokoa... Simba ikawa bingwa.
YANGA 0-1 SIMBA - 1992
Ilikuwa fainali ya Ligi Kuu ya Muungano. Hii ilikuwa mara ya pili kwa ligi hiyo iliyokuwa kuu Tanzania, kuchezwa kwa mtindo wa mtoano, baada ya 1990 pale Pamba ya Mwanza ilipocheza na Small Simba ya Zanzibar kwenye uwanja huohuo wa Amaan.
Bao la tik tak la winga mfupi wa Simba mwenye asili ya Burundi, Damien Kimti likatosha kuipa Simba ubingwa.
SIMBA 2-0 YANGA - 2011
Ilikuwa Januari 12, 2011 pale watani wa jadi walipokutana kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi. Yanga waliingia kwenye mechi hii wakiwa hawajapoteza mechi yoyote kwenye ligi kuu, kama ilivyo mwaka huu...na Simba walikuwa wamepoteza mechi moja tu, kama mwaka huu.
Dakika 90 za fainali, Simba ikashinda mabao 2-0 ya Mussa Hassan Mgosi na mzambia Felix Sunzu.
SIMBA 0-0 YANGA (penalti 3-4) - 2021
Hii ilikuwa mechi iliyoanzisha safari ya makombe kurudi Jangwani baada ya kupotea kwa muda mrefu. Utawala wa GSM ulikuwa na mwaka mmoja Yanga na msimu mmoja uliotangulia na Injinia Hersi Said alitamba Yanga lazima itakuwa bingwa wa ligi kuu na isipokuwa hivyo, basi aulizwe yeye.
Ubingwa ikaukosa na maswali yakarudi kwake... akajificha kuyajibu. Hamad ndio ikaja fainali hii, Yanga ikataka kuitumia kuficha kilichotokea msimu uliopita.
Wakashinda kwa penati 4-3 baada ya sare tasa ya dakika 120. Yanga ikalifanyia gwaride la heshima (parade) kombe lao kwenye mitaa ya Dar es Salaam iliporudi nalo.