Chobanka: Ratiba mpya WPL kuongeza ufanisi
Muktasari:
Chobanka amesema hapo awali ratiba ilikuwa inazibana timu hizo kwa safari ndefu zisizo na mpangilio rafiki, hali iliyokuwa ikiathiri maandalizi pamoja na matumizi ya fedha.
KOCHA wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu ya Wanawake yamekuwa na msaada mkubwa kwa timu za madaraja ya kati na zile zisizo na uwezo mkubwa kifedha.
Chobanka amesema hapo awali ratiba ilikuwa inazibana timu hizo kwa safari ndefu zisizo na mpangilio rafiki, hali iliyokuwa ikiathiri maandalizi pamoja na matumizi ya fedha.
“Zamani ulikuwa unakuja Dar es Salaam, kisha unaenda kucheza mechi Mwanza halafu unarudi Iringa. Ukiangalia hiyo ratiba, ilikuwa ngumu sana kwa timu ambazo hazina wadhamini wakubwa,” amesema Chobanka.
Amefafanua changamoto hiyo ilikuwa tofauti kwa timu kubwa kama Simba Queens, Yanga Princess na JKT Queens, ambazo zina bajeti kubwa na uwezo wa kumudu gharama za safari na maandalizi bila presha kubwa.
Chobanka amesema msimu huu ratiba imepangiliwa vizuri na inawapa unafuu timu, jambo ambalo limepunguza gharama na uchovu wa wachezaji.
“Sasa hivi ratiba imeturahisishia sana. Tunapokuja Dar es Salaam tunacheza mechi zetu zote za huku, kisha tunarejea nyumbani kujiandaa. Hii imesaidia sana kusevu gharama za nauli na kupunguza safari zisizo za lazima,” ameongeza.