JKT Queens na Tausi FC zashuka dimbani kuwania pointi WPL
Muktasari:
- JKT Queens itaikaribisha Ceasiaa Queeens kwenye Uwanja wa Meja Generali Isamuhyo, huku Tausi FC ikiwa mwenyeji wa Bilo Queens, mechi ikipigwa Uwanja wa KMC.
BAADA ya jana kupigwa mechi nne za mzunguko wa 13 wa Ligi Kuu Wanawake Tanzania Bara (WPL), leo ligi hiyo itaendelea zikipigwa mechi mbili kwenye viwanja tofauti jijini Dar es Salaam.
JKT Queens itaikaribisha Ceasiaa Queeens kwenye Uwanja wa Meja Generali Isamuhyo, huku Tausi FC ikiwa mwenyeji wa Bilo Queens, mechi ikipigwa Uwanja wa KMC.
JKT iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi 32, inaikaribisha Ceasiaa ambayo kwenye mechi 13 imeshinda tatu, sare tatu na kupoteza saba ikiwa nafasi ya tisa.
Kumbukumbu mbaya kwa mabinti wa kocha Ezekiel Chobanka kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza walipokutana na JKT, walipoteza kwa mabao 3-0 na leo wana kibarua cha kupambania pointi dhidi ya mabingwa watetezi.
JKT inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa kamili baada ya kumkosa winga machachari, Winifrida Gerald aliyekuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha miezi mitatu baada ya kumchezea faulo beki wa Geita Queens.
Nyota huyo ndiye mfungaji bora kwa JKT akipachika mabao nane akiwa kwenye tatu bora ya wachezaji wanaoongoza kwa ufungaji ndani ya ligi hiyo.
Akizungumzia mechi hiyo, Chobanka alisema wana kibarua cha kuwania pointi tatu dhidi ya mabingwa hao watetezi.
“Tunafahamu ugumu wa mechi hiyo na wachezaji tumeshaongea nao namna ya kukabiliana na timu inayoshambulia sana kama JKT,” alisema Chobanka. Kwa mwingine, Nahodha wa Tausi, Fatoumata Diarra, alisema: “Kila mchezaji amejipanga kuhakikisha anatoa nguvu zake kwa ajili ya kuisaidia timu kupata pointi tatu.”