Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Isamuhyo ulivyobeba maswali matano Dabi ya Kariakoo

DABI Pict


MEI 3, 2026, tunaweza kuiita siku ya kuheshimiana, hiyo ni kutokana na mchezo wa Ligi Kuu Bara unaokwenda kupigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam wakati Simba ikiikaribisha Yanga.


Tunasema siku ya kuheshimiana kutokana na wakongwe hao kila mmoja akitaka kushinda ili kuweka heshima baada ya kutoka kushuhudia Aprili 29, 2026 Simba ikiichapa Yanga bao 1-0 na kubeba Kombe la Muungano.


Kichapo hicho katika Kombe la Muungano, kimeiongezea Simba kujiamini zaidi kuelekea kuikabili Yanga ambayo awali ilionesha ubabe wake wa mechi sita mfululizo za Dabi ya Kariakoo.

Kabla ya kupoteza dhidi ya Simba, Yanga ilisimamishwa kwa matokeo ya 0-0, sasa wakongwe hao wanakwenda kukutana katika mechi ya heshima na uamuzi ndani ya Ligi Kuu Bara.

SIMBA 01

Kutoka na uzito wake, Simba baada ya kubeba Kombe la Muungano, fasta imerejea Dar kujiandaa na dabi nyingine, kwa upande wa Yanga, imebaki Zanzibar kuendelea na maandalizi.

Kila upande umetoa sababu zake, Simba imesema imewahi ili kupata muda wa mapumziko baada ya kazi kubwa kisha kuanza maandalizi kabambe ya kushinda tena.

Yanga wanasema kitendo cha kubaki Zanzibar, ni kusaka utulivu kwa wachezaji na wataendelea na maandalizi huku mipango yao ni kutua Dar siku ya mechi.

Mechi hiyo inayokwenda kupigwa Jumapili hii, ina maswali matano ambayo baada ya dakika tisini tutapata majibu yake.

SIMBA 12

HATIMA YA UBINGWA

Kwa sasa, Yanga inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Simba. Timu hizo zinashika nafais mbili za juu na mchezo huu umeshikilia sehemu ya uamuzi wa ligi.

Zikiwa zimebakiwa na mechi 11, zinaanza hesabu za kulisaka taji hilo kwa kukutana zenyewe, kisha baada ya hapo, kila mmoja anashika njia yake.

Yanga inayoongoza ligi kwa pointi 47, inasaka taji la tano mfululizo, huku Simba yenye pointi 42, ikihitaji ubingwa huo ilioukosa kwa misimu minne mfululizo.

Matokeo ya ushindi kwa Yanga, yataifanya kujikita zaidi kileleni kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Simba.

Lakini Simba ikishinda, itapunguza gepu la pointi dhidi ya Yanga na kubaki mbili.

SIMBA 11

Yanga baada ya kumalizana na Simba, mechi kumi zijazo ni dhidi ya KMC (ugenini), Coastal (nyumbani), Dodoma Jiji (ugenini), Singida Black Stars (nyumbani), Namungo (nyumbani), Mashujaa (ugenini), Fountain Gate (ugenini), Azam (nyumbani), TRA United (nyumbani) na JKT Tanzania (ugenini).

Kwa upande wa Simba, baada ya kuikabili Yanga, itacheza dhidi ya JKT Tanzania (nyumbani), Tanzania Prisons (nyumbani), Mashujaa (ugenini), Coastal Union (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani), Pamba Jiji (nyumbani), Mbeya City (ugenini), Mtibwa Sugar (ugenini), Singida Black Stars (nyumbani) na KMC (nyumbani).

SIMBA 10

Ukiangalia takwimu za msimu huu, Yanga ilipokutana na wapinzani wake hao 11 waliobaki kuanzia Simba wanaocheza nao Jumapili hii, waliambulia kukusanya pointi 27 kati ya 33, baada ya kushinda nane dhidi ya dhidi ya KMC (4-1), Coastal (1-0), Dodoma Jiji (3-1), Singida Black Stars (3-0), Namungo (1-0), Mashujaa (6-0), Fountain Gate (2-0), na JKT Tanzania (5-0). Sare zikiwa tatu zote bila ya mabao dhidi ya Simba, Azam na TRA United.

Simba matokeo dhidi ya wapinzani wake waliobaki, walikusanya pointi 25, hiyo ilitokana na kushinda mechi saba dhidi ya JKT Tanzania (2-1), Tanzania Prisons (2-0), Mashujaa (2-0), Coastal Union (2-0), Mbeya City (3-0), Singida Black Stars (2-1) na KMC (2-0), huku sare zikiwa nne dhidi ya Yanga (0-0), Do-doma Jiji (0-0), Pamba Jiji (1-1) na Mtibwa Sugar (1-1).

SIMBA 08

Hivyo basi, Kariakoo Dabi ya Jumapili hii, Simba ina uhitaji mkubwa wa kushinda ili kurudisha heshima yake mbele ya Yanga, lakini pia kupunguza gepu la pointi kutoka tano la sasa hadi mbili ili kuisogelea nafasi ya kwanza.

Simba haijachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo ambapo Yanga imeendelea kutawala, hivyo umuhimu wa ushindi kwao ni mkubwa zaidi.

Hata hivyo, Yanga nayo ina umuhimu wa kusaka ushindi wa mechi hii kwani inahitaji kutanua wigo la pointi dhidi ya mtani wake huyo wa jadi na kuusogelea ubingwa, pia kuendeleza ubabe wake kwa Simba.

SIMBA 07

Hii itakuwa Kariakoo Dabi ya tatu kuwakutanisha Steve Barker wa Simba na Pedro Goncalves wa Yanga tangu wakabidhiwe mikoba ya kuviongoza vikosi hivyo.

Pedro aliyetambulishwa Oktoba 25, 2025 kuchukua nafasi ya Romain Folz, huku Barker akitambulishwa Desemba 19, 2025 akimrithi Dimitar Pantev, walikutana kwa mara ya kwanza Machi Mosi 2026 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika bila ya kufungana, kisha wakakutana tena Aprili 29, 2026 katika fainali ya Kombe la Muungano ambapo Barker aliibuka kidedea mbele ya Pedro, hivyo mechi ya tatu haitakuwa rahisi kwa wote kwani Pedro atataka kulipa kisasi, Barker akisaka kuendeleza ubabe.

SIMBA 09

MAJIBU DABI YA ZENJI

Wapo wanaosema Simba ilikuwa na bahati kuifunga Yanga katika fainali ya Kombe la Muungano kwa sababu kama ingeishia dakika tisini, basi tungeshuhudia sare nyingine bila ya mabao kama ilivyokuwa duru la kwanza wakubwa hao walipokutana kwenye ligi.

Lakini kwa kuwa ni mechi ya fainali na bingwa lazima apatikane, sheria ya kuongeza dakika 30 baada ya zile 90 kutopata mshindi, ikatumika, ndipo madhambi yaliyofanywa dakika ya 118 na winga wa Yanga, Edmund kwenda kwa kiungo wa Simba, Clatous Chama ndani ya boksi, mwamuzi Dickens Mimisa Nyagrowa raia wa Kenya akaamuru penalti iliyokwenda kufungwa na Seleman Mwalimu, likawa bao pekee la mchezo huo.

Ushindi huo wa Simba umekuja baada ya kucheza mechi saba mfululizo dhidi ya Yanga bila ya kushinda, zaidi ikiambulia sare moja katika ligi msimu huu, kabla ya hapo ilichapika mara sita zikiwamo mbili Ngao ya Jamii na nne Ligi Kuu Bara.

SIMBA 01

Simba kabla ya kushinda Dabi huko Zanzibar, mara ya mwisho kuifunga Yanga ilikuwa Agosti 13, 2023 kwa penalti 3-1 katika Ngao ya Jamii, mechi ambayo muda wa kawaida iliisha 0-0.

Majibu ya kama Simba ilibahatisha kuifunga Yanga, tunaweza kuyapata Jumapili hii ambapo dakika tisini zitaamua kwamba ni sare ama ushindi utaenda Msimbazi au Jangwani.


MBINU ZA MAKOCHA

Pedro alianza na mshambuliaji mmoja, Prince Dube, huku pia akimuweka nje Duke Abuya, kiungo ambaye amekuwa muhimili mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga.

Katika ulinzi, kulia alianza na Yao Kouassi anayerejea kwa kasi tangu apate majeraha yaliyomuweka nje takribani msimu mzima, kushoto akawa Chadrack Boka kutokana na Mohamed Hussein kuumia.

Katika mechi hii ya Jumapili, pale kiungo cha kati kutakuwa na mabadiliko, Mudathir anayeanza kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, hatakuwepo na badala yake Duke atacheza sambamba na Mohamed Damaro, lakini kuna uwezekano mkubwa Pedro akasimamisha washambuliaji wawili, Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ ambao tumeshawaona wakicheza pamoja na kufanya vizuri.

Kwa upande wa Barker ambaye katika fainali ya Kombe la Muungano alirudia kile alichofanya Dabi ya kwanza palepale Zanzibar kwa kuanza bila ya mshambuliaji halisi, pengine hapa anaweza kubadilika.

Mchezaji ambaye alianza naye aliumia mapema, Anicet Oura, hivyo kutokana na maumivu ya nyama za paja, anaweza kukosekana, Seleman Mwalimu ambaye ndiye mshambuliaji halisi, kuna nafasi ya kuanza.

DAB 08

Hayo ni mabadiliko ya kimbinu anayoweza kuja nayo Barker kwa sababu atahitaji kuwachanganya Yanga ambao mara mbili alipokutana nao, hakuanza na mshambuliaji halisi.


KITANZI CHA MASTAA/MAKOCHA

Dabi ya Kariakoo imekuwa ukiwapandisha mastaa na kuwashusha. Wapo ambao baada ya kuzingua katika mechi hizi za upinzani wa jadi ndiyo anapotea kabisa.

Lakini upande mwingine, wanaong’ara wanabaki kuwa mashujaa wa timu. Dabi iliyopita, Edmund John wa Yanga alisababisha pigo la penalti ambalo limeigharimu timu hiyo zikibaki dakika mbili tu mechi kumalizika kwa sare lakini tukio hilo likaamua matokeo ya ushindi kwa Simba.

DAB 07

Achana na hilo, kwa hivi karibuni, Hussein Kazi wakati anaitumikia Simba, alisababisha penalti ambayo iliipa Yanga bao katika ushindi wa 2-1, Aprili 20, 2024. Baada ya pale, maisha yake ndani ya Simba yakawa magumu, hivo sasa yupo Namungo.

Kwa sasa tunapoelekea kumaliza msimu, kuna mastaa ndani ya timu hizi ambao mikataba yao inaelekea ukingoni, hivyo wanaweza kujijengea sifa au kuiharibu kupitia mchezo huu.

Si tu kwa wanaomaliza mikataba, hata wale ambao wamekuwa wachezaji tegemeo kwenye timu, wakizingua usishangae kuona mwisho wa msimu wanapewa mkono wa kwaheri.

Presha ya Dabi haijawahi kuzoeleka, hivyo unapofika mchezo wa aina hii, umakini unaongezwa muda wote ili tu mtu asiharibu. Usisahau pia hata makocha nao wamewahi kuondoshwa baada ya kupoteza Dabi. Mara ya mwisho Robert Oliveira ‘Robertinho’ baada ya Simba kufungwa 5-1 na Yanga, safari yake pale Msimbazi ikaishia hapo.

DAB 06

KUJENGA JINA

Shiza Kichuya aliibuka shujaa wa Simba Oktoba 1, 2016 alipofunga bao la kona ya moja kwa moja dakika ya 87 katika sare ya 1-1 dhidi ya Yanga. Hadi leo, Kichuya ambaye alipoondoka Simba amepita timu kadhaa ikiwamo Namungo na JKT Tanzania na sasa anaitumikia Coastal Union, bado jina lake linakumbukwa mitaa ya Msimbazi.

DAB 02

Ile kona goli imempa heshima huku mwenyewe akikiri kwamba bao lile limempatia umaarufu na kwa wakati ule alipata fedha za kutosha kutoka kwa wadau waliokuwa wakimpongeza namna alivyoiokoa timu na kipigo zikibaki dakika tatu.

Fiston Mayele na Stephane Aziz KI licha ya kwamba hivi sasa hawapo Yanga, lakini wanakumbukwa mitaa ya Jangwani kwa kuinyanyasa Simba kipindi wapo Ligi Kuu Bara. Kariakoo Dabi ni mechi inayompandisha mchezaji na kumshusha, hivi sasa Seleman Mwalimu amejijengea jina baada ya bao lake kuipa Simba ubingwa wa Muungano mbele ya Yanga.

Zamu ya nani sasa kuimbwa? Tusubiri dakika tisini za Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Jumapili hii.