Prime
Kibabage abadili upepo Simba
WAKATI beki wa kushoto Nickson Kibabage anatambulishwa kutua Simba Januari 19, 2026, usajili wake haukuonekana kama unawabariki baadhi ya mashabiki na kuona timu inatakiwa kujengwa na majembe ya maana ili kuleta mapinduzi ya kunyakua ubingwa.
Lakini ilikuwa tofauti kwa mafundi wa mpira kama mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo, Emmanuel Gabriel aliyemkingia kifua akiamini ilikuwa ni suala la muda kwa nyota huyo kuonyesha kipaji na kiwango chake, kitakachobadilisha kutoka kuchukuliwa kawaida na kuwa mchezaji muhimu kikosini.
Hata baada ya Kibabage kucheza kwa kiwango cha juu, bado Gabriel anasimamia kauli yake ya kuamini ni beki mwenye msaada mkubwa Simba.
“Nilizungumza hivyo kwa sababu Kibabage ni mzawa, nafahamu uwezo wake na talenti aliyonayo, ndiyo maana sikuwa na wasiwasi naye, kile nilichowahi kuliambia Mwanaspoti kinaonekana kwa macho,” alisema.
Legendari mwingine aliyewahi kuamini katika usajili wa Kibabage alikuwa staa wa zamani wa klabu hiyo, Zamoyoni Mogalla aliyesema: “Sina shida na usajili wake, ana talenti, kazi itakayobakia kwake ni kujituma na kucheza kwa kiwango cha juu.”
Kibabage aliyezaliwa Oktoba 12, 2000 (umri wa miaka 25), mkoani Morogoro ni kama ameondoa kelele za mashabiki waliokuwa wanaliona pengo la Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyejiunga Yanga, baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kila anapopewa nafasi ya kucheza.
Kitu ambacho mashabiki wa Simba hawakuonekana kukubaliana na usajili wake ni kitendo cha kuondoka Yanga kwa kile kilichoelezwa amekosa nafasi kikosi cha kwanza, kisha kwenda Singida Black Stars, hivyo wakaona wanachukua wachezaji ambao hawataleta mapinduzi ya kupambania ubingwa.
Tangu kuondoka kwa Tshabalala aliyeonekana angeweza kuziba pengo alikuwa Anthony Mligo, aliyekuwa pendezo la kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids aliyekuwa anaamini katika vijana zaidi, lakini bado akaonekana hatoshi.
Kivuli cha Tshabalala kimevuliwa na Kibabage, ambaye uwanjani anaweza akashambulia, anakaba na alionyesha kumudu presha ya mechi kubwa za dabi (tatu) msimu huu, mbili za ligi na moja ya Fainali ya Kombe la Muungano.
Katika dabi hizo, Kibabage alikabiliana na mafundi kama Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, huku mchango wa kiwango chake kikiisaidia timu kuchukua taji la kwanza msimu huu la Kombe la Muungano.
Ukiachana na dabi, mechi dhidi ya TRA United, iliyopigwa Aprili 09, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, ukimalizika kwa suluhu, alikabiliana vikali na winga Ramadhan Salum Chobwedo ambaye aling’ara katika matukio mengi ya uwanjani siku hiyo.
Baada ya mechi hiyo, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alikiri asingekuwa Kibabage basi Chobwedo angewafunga.
“Beki wetu kafanya kazi kubwa ya kukabiliana na Chobwedo, vinginevyo tungeongea kitu kingine,” alisema Ally.
Pia Chobwedo alikiri kwamba: “Kibabage ni beki imara, mwenye kasi na anacheza kwa kiwango cha juu, kinachoisaidia timu yake kuwa salama.”
Ukiachana na Ahmed Ally na Chobwedo, kiwango chake kimemfurahisha kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni anayesema: “Kitendo cha mchezaji kuwa imara dhidi ya maneno ya kutoaminika na mashabiki, anajitambua na amethibitisha kwa matendo na sasa wanamshangilia, mchezaji anapaswa kutambua kitu kimoja pekee kwamba mashabiki wanahitaji furaha na siyo uchungu.”
Kocha wa Dodoma Jijni, Aman Josiah, alisema: “Kibabage ni beki wa kisasa, ana kasi, anakaba na kufunga, mchango wake unaonekana anapokutana na timu pinzani.”
Wakati anaichezea Yanga, Kibabage hakuwa panga pangua kikosini ingawa alikuwa anapata nafasi ya kucheza mechi za mashindano mbalimbali. Huko alikutana na ushindani mbele ya Chadrack Boka.
Kabla ya kutua Simba, Kibabage amecheza Mtibwa Sugar (2018-2019), akaenda kujiunga na Difaa El Jadidi ya Morocco (2019-2021), akarejea nchini na kujiunga na KMC (2020 kwa mkopo), Singida Black Stars (2022-2023), Yanga (2023-2025) akarejea Singida na sasa yupo Simba (2025-2026).