Prime
Mtego wa Yanga ubingwa wa 32 Bara
IJUMAA hii Yanga inacheza dhidi ya Singida Black Stars katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, huku timu hiyo ikikabiliwa na rekodi ngumu ya kutetea ubingwa iliouchukua misimu minne mfululizo.
Timu hiyo ndio vinara wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 54, baada ya kushinda mechi 16, sare sita na kupoteza moja kati ya 23 ilizocheza, ikiwazidi wapinzani wao wakubwa wa jadi hapa nchini, Simba inayoshika nafasi ya pili na pointi 52.
Moja ya rekodi ngumu inayoisaka Yanga msimu huu ni ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu huku ikitoka kuchukua taji la Kombe la Mapinduzi mwaka 2026, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa bingwa wa michuano hiyo akashinda pia Bara tangu mwaka 2007.
Yanga iliifunga Azam FC kwa penalti 5-4 na kutwaa Kombe la Mapinduzi 2026 baada ya suluhu (0-0) ndani ya dakika 120 japo rekodi zinaonyesha hakuna timu iliyochukua ubingwa huo na kushinda Ligi Kuu Bara, jambo linalosubiriwa kama litatokea mara ya kwanza.
Mwaka 2007, Yanga ilishinda ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, huku msimu wa 2006-2007, Simba ikiwa bingwa wa Ligi ndogo iliyotumika ili kumpata mshindi wa kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa. Baada ya hapo mwaka 2008, Simba ikatwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, ila ilivyokuja Bara taji likachukuliwa na Yanga msimu wa 2007-2008. Mtibwa Sugar ikabeba Kombe la Mapinduzi 2010, Simba ikachukua ligi 2009–2010.
Mwaka 2011, Yanga na Simba zikakutana katika fainali ya Kombe la Mapinduzi, Simba ikashinda mabao 2-1.
Kushinda kwa Simba 2011 ikaendeleza nuksi kwani ilikosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2010-2011 na kushuhudiwa kikosi cha Yanga kikitwaa taji hilo.
Azam ikachukua Kombe la Mapinduzi mara mbili mfululizo ambapo ni mwaka 2012 na 2013, katika kipindi hicho, bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011–2012 alikuwa Simba, kisha 2012–13 ikawa zamu ya Yanga.
Wakati Azam inatwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza msimu wa 2013–2014, bingwa wa Mapinduzi alikuwa KCC kutoka Uganda iliyoifunga Simba bao 1–0 katika fainali.
Ubingwa wa Yanga Ligi Kuu Bara msimu wa 2014–2015, ulipishana na Simba iliyobeba Kombe la Mapinduzi 2015 ilipoifunga Mtibwa Sugar kwa penalti 4–3.
Yanga ikachukua tena ubingwa wa ligi msimu wa 2015–2016 na 2016–2017, huku bingwa wa Kombe la Mapinduzi akiwa URA ya Uganda (2016) na Azam (2017). Mwaka 2018 na 2019, Azam ikabeba Kombe la Mapinduzi, upande wa ligi, bingwa akawa Simba mfululizo msimu wa 2017–2018 na 2018–2019, huku pia Wekundu hao wa Msimbazi wakibeba tena ligi msimu wa 2019-2020 ambapo Mtibwa ilikuwa bingwa wa Kombe la Mapinduzi 2020.
Mwaka 2021, Yanga ilifika fainali ya Kombe la Mapinduzi na kuichapa Simba kwa penalti 4-3 baada ya suluhu (0-0), ila kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani kilivyorudi Bara kilikosa ubingwa wa ligi msimu wa 2020-2021 uliokwenda Simba ikiwa ni msimu wa mwisho kwa kikosi hicho kuchukua na wa nne mfululizo kutwaa pia.
Fainali ya mwaka 2026, Yanga ilishinda Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga Azam FC kwa penalti 5-4 baada ya suluhu (0-0) ndani ya dakika 120, jambo linalosubiriwa kutokea ni kikosi hicho kama kitatwaa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026 na kuandika rekodi mpya. Ikiwa Yanga itashinda ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2025-2026, itaweka rekodi mpya ya timu ya kwanza kutwaa taji hilo huku ikitoka kuchukua Kombe la Mapinduzi, tangu michuano hiyo inayofanyika visiwani, Zanzibar ilivyoanza mwaka 2007.