Prime
Yanga yamwachia msala Aziz KI
KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Stephane Aziz Ki amepewa ujumbe mzito na mabosi wa klabu hiyo wanaotaka kumuona akimaliza kwanza mgogoro wa mkataba wake na klabu anayochezea Libya kabla ya kuanza mazungumzo rasmi ya kurejea Jangwani.
Aziz Ki ameacha alama kubwa ya kihistoria katika kikosi cha Yanga kwenye misimu mitatu aliyoitumikia klabu hiyo kabla ya kuuzwa kwenda Wydad Casablanca ya Morocco, Juni 2025.
Baada ya kuuzwa kwenda Wydad ambako alitumika kwa miezi minane, dirisha dogo msimu huu aliuzwa kwenda Al Ittihad ya Libya ambako alisaini mkataba wa miaka miwili kukitumikia kikosi hicho.
Aziz Ki ni miongoni mwa wachezaji waliocheza kwa mafanikio Yanga, msimu wa 2022/23 akiibuka na tuzo ya mfungaji bora akimaliza ligi na mabao 21. Aliwahi kuwa miongoni mwa nyota walioibeba Yanga kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku akitajwa mara kadhaa kuwa mmoja wa viungo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mwanaspoti linafahamu kuwa, Aziz Ki hana furaha na timu anayoichezea sasa, huku sababu za kiusalama na kifamilia zikitajwa, ikumbukwe kuwa kiungo huyo mwaka jana alimuoa mwanamitindo maarufu Tanzania Hamissa Mobetto.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa Aziz Ki ameonyesha nia ya kutaka kurejea Yanga baada ya kuona ndiko kulikompa mafanikio makubwa katika maisha yake ya soka, lakini mabosi wa mabingwa hao wa Tanzania hawapo tayari kuingia kwenye gharama kubwa za kuvunja mkataba wake uliopo Libya.
Ilielezwa kuwa Yanga imeweka wazi msimamo wake kwa nyota huyo wa Burkina Faso kwamba milango iko wazi kwake, lakini jukumu la kwanza ni kuhakikisha anamalizana na waajiri wake wa sasa ili awe huru kabla ya klabu hiyo kufikiria hatua nyingine.
“Aziz kama ambavyo nilikwambia ameomba kurudi hapa, anaona kama hapa ndio sehemu ya bahati kwake, huwezi kukataa kumrudisha mchezaji kama yeye, wote tumefurahia,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.
“Kwa sasa si rahisi sisi kuweka kichwa chetu mbele kutaka kumrudisha. Unajua amekaa pale Libya kwa muda mfupi tangu atoke Morocco, kwa hiyo tumemwambia kama anataka kuja hakuna shida, basi afanye taratibu zote za kumaliza mkataba wake na waajiri wake. Hapa nyumbani tutampokea.”
Mmoja wa watu wa karibu na staa huyo alilithibitisha gazeti hili kuwa Aziz Ki anatarajiwa kukutana na viongozi wa klabu yake nchini Libya kwa lengo la kuanza mchakato wa kuomba kuondoka, hatua ambayo inaweza kufungua njia ya kurejea Tanzania kama pande zote zitafikia mwafaka.
Makali ya Aziz yalikata alipofika Wydad kutoka kufunga mabao 39 ndani ya misimu mitatu, mpaka bao moja akiwa timu hiyo aliyoichezea nusu msimu.