Kasheshe la EPL kuendelea tena wikeindi hii
Muktasari:
- Man City ambayo ni miongoni mwa timu tatu zinazopewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, wiki iliyopita ilifeli kupunguza pengo la alama dhidi ya vinara Arsenal baada ya kupoteza mbele ya Newcastle kwa mabao 2-1.
MANCHESTER, ENGLAND: NI wiki nyingine katika Ligi Kuu England. Baada ya mambo kuwa mabaya kwa Pep Guardiola na vijana wake wiki iliyopita, wanatarajia kubadilisha hali hiyo wikiendi hii na itakuwa nyumbani kuumana na Leeds United kuanzia saa 12:00 jioni.
Man City ambayo ni miongoni mwa timu tatu zinazopewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, wiki iliyopita ilifeli kupunguza pengo la alama dhidi ya vinara Arsenal baada ya kupoteza mbele ya Newcastle kwa mabao 2-1.
Kwa sasa Man City ina alama tofauti ya alama saba dhidi ya Arsenal na ikiwa itashinda tofauti ya alama itakuwa ni nne, ingawa ilikuwa na uwezo wa kufanya tofauti iwe pointi moja ikiwa ingeshinda mechi iliyopita.
Mbali ya mechi hii ambayo itafuatiliwa na mashabiki wengi wa soka kutokana na umuhimu wake katika mbio za ubingwa, Kocha wa Thomas Frank na vijana wake wa Tottenham na wamekuwa na kipindi kigumu katika wiki kadhaa zilizopita, watakuwa nyumbani kuikaribisha Fulham katika dabi ya London.
Spurs haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu England ikiwa imetoka sare moja na kufungwa mbili. Kwa sasa inashika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 18.
Ikiwa itashinda mechi hii, inaweza kupanda hadi nafasi nne au tano za juu ikiwa timu zilizo juu yake zitapoteza au kupata sare.
Sunderland ambayo imerejea EPL baada ya kukosekana kwa miaka mingi, ina nafasi ya kurudi hadi nafasi nne za juu leo ikiwa itashinda mechi yake leo dhidi ya Bournemouth na timu zilizo juu yake zikapata matokeo mabaya.
Kwa sasa wababe hawa wa Championship kwa msimu uliopita, wanashika nafasi ya saba kwa pointi zao 19 ambazo ni tofauti ya alama nne dhidi ya Chelsea inayoshika nafasi ya pili katika msimamo.
Baada ya kuizuia Man City wiki iliyopia, Newcastle itakutana na vijana wa David Moyes ambao hawana msimu mzuri.
Newcastle iliyoonekana kufanya vizuri misimu miwili nyuma kwa sasa pia ina hali mbaya ikiwa inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 15.
Mechi nyingine leo itakuwa ni kati ya Brentford na Burnely inayoburuza mkia.
RATIBA KAMILI
Brentford v Burnley (Saa 12:00 jioni)
Sunderland v Bournemouth (Saa 12:00 jioni)
Man City v Leeds United (Saa 12:00 jioni)
Everton v Newcastle (Saa 2:30 usiku)
Tottenham v Fulham (Saa 5:00 usiku)