Mwamnyeto afunguka mazito, amtaja beki Simba
Muktasari:
- Rushine ambaye alitua Simba msimu huu akitokea Maccabi ya Israel, huku akiwa na rekodi ya kuichezea Mamelodi Sundowns kwa misimu mitatu mfululizo.
KIWANGO cha beki wa klabu ya Simba, Rushine De Reuck hakijaishia kuwakosha mashabiki,mastaa na viongozi wa kikosi hicho, ila kimefika mbali mpaka Yanga ambapo nahodha wa Wanajangwani hao Bakari Mwamnyeto ameweka wazi kwamba,uwezo wa Msauzi huyo ni wa kiwango cha juu.
Rushine ambaye alitua Simba msimu huu akitokea Maccabi ya Israel, huku akiwa na rekodi ya kuichezea Mamelodi Sundowns kwa misimu mitatu mfululizo.
Tangu atue Simba, Rushine amekuwa mbadala bora wa beki wa zamani wa klabu hiyo Che Malone Fondoh ambaye aliondoka msimu uliopita na kwenda kuitumikia USM Alger ya Algeria ambayo imetwaa Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati anatua Simba, Rushine hakuwa anaaminiwa na viongozi wa timu hiyo, kwani usajili wake ulikuwa ni mapendekezo ya kocha Msauzi mwenzake Fadlu Davids, ambaye hakukaa sana na kikosi hicho baada ya msimu kuanza alitimkia zake Raja Casablanca ya Morocco.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwamnyeto amesema Rushine ni kati ya mabeki wanaomvutia zaidi kutokana na kiwango bora ambacho ameendelea kukionyesha hasa katika eneo lake la ulinzi.
Amesema kuwa, mabeki wazuri wapo wengi, lakini anapata vitu vingi vya kujifunza kwa Rushine, sio kwa sababu tu ni mchezaji wa Simba, bali ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na uwezo wa juu.
“Rushine ana utulivu, ana uwezo wa kuzuia mashambulizi kwa haraka, unajua kuna zile rekodi za timu kupata pointi tatu muhimu kwenye mechi na kuna ile ya kutokuruhusu mabao.
“Unamuona Rushine anavyoisaidia timu yake isiruhusu mabao hata kama itakuwa imeshinda lakini kuwafunga bado ni ngumu, lakini hii yote ni uzoefu ulioungana na ubora ndani yake,” amesema Mwamnyeto.
Ameongeza kuwa;”Sijawahi kukaa na Rushine tukazungumza zaidi ya salamu kwa sababu ya muda, mara nyingi tunakuwa kwenye mzuka wa kazi kwa hiyo huwezi kuanzisha mazungumzo marefu.
“Lakini Ibrahim Bacca naye ni moja ya mabeki bora wazawa ambao pia wanakitu kikubwa cha kujifunza akiwa uwanjani anacheza kufa au kupona ili tu kuilinda timu yake na mashambulizi ya wapinzani tena kwa akili kubwa.”
Simba imecheza michezo 25 ya ligi, huku Yanga ikicheza 24 ambapo leo inavaana na Namungo.