Biashara ya fedha inavyoikamata Tunduma

Mshami Mwakatobe akisubiri wateja wa kubadilisha fedha katika eneo la Kisimani, Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia. Picha na Regnald Miruko

Muktasari:

Ufikapo Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia, kitu cha kwanza utakachokutana nacho ni biashara ya mkononi ya kubadili fedha za kigeni au umachinga wa fedha.

Dar es Salaam. Ufikapo Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia, kitu cha kwanza utakachokutana nacho ni biashara ya mkononi ya kubadili fedha za kigeni au umachinga wa fedha.

Kwa wakazi wa miji mikubwa ukizungumzia ‘bureau de change’ au duka la kubadili fedha za kigeni, utaeleweka haraka, na maduka haya moja ya sifa yake kuu ni ulinzi imara, hii ni kwa mteja na muuzaji.

Lakini, hali hii ni tofauti na Tunduma, huko hakuna hofu ya kuibiwa wala kuhitaji kibanda cha kufanyia biashara, vijana na wazee wa umri wa kati wanajihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za mataifa mbalimbali. Huhitaji kuelekezwa mahali waliko, kwa kuwa wanaonekana wazi.

Utawabaini kutokana na kiasi kikubwa cha fedha walichonacho mikononi bila wasiwasi wowote. Si ajabu kumuona mtu amekamata Sh5 milioni au Sh10 milioni mkononi, akisubiri mteja wa kubadilishana naye kupata fedha za kigeni au kupata za Tanzania.

“Hapa kuna kila aina ya hela, zipo za shilingi za Tanzania, Kwacha za Zambia, Euro za Umoja wa Ulaya, Pauni za Uingereza, Dola za Marekani, Yuan za China, Yen za Japan na nyingine nyingi za DRC, Malawi, yaani huwezi kukosa pesa yoyote hapa,” anasema Libson Mwasambawa anayefanya biashara hiyo.

Anasema katika eneo hilo, hasa kwenye kijiwe maarufu kama Kisimani, unakuta mtu ana hadi Sh50 milioni au zaidi na kila mtu ana matumaini ya kupata.

Kwa mujibu wa Mwasambawa, biashara hiyo inawalipa na ndiyo wanaitegemea kuendesha maisha yao na familia zao.

Biashara hiyo inayofanyika kwa uwazi mikononi, imeongezeka hadi kuwa tishio kwa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, kutokana na viwango vya kuvutia wanavyotoa wamachinga hao.

Kila unayekutana naye anajua viwango vya ubadilishaji fedha kwa siku hiyo kichwani, licha ya kubadilika mara kwa mara.

Akifafanua jinsi wanavyopata faida, Mshami Mwakatobe alisema akibadili Sh10,000 ya Tanzania kwa Kwacha 50 za Zambia anabaki na Sh200 ambayo ndiyo faida yake.

 

 

Usalama wa fedha

Akizungumzia usalama wa fedha zao, Uswege Mwangilingi anasema mahali pale kuna usalama wa kutosha na wanalindana wenyewe kwa wenyewe.

“Akija mwizi hapa unadhani atatoka?” alihoji Mwangilingi akimaanisha kuwa atauawa na wafanyabiashara hao, wengi wao wakiwa ni vijana.

Mfanyabiashara mwingine, Kicha Madiba anasema likitokea tatizo la usalama wanalimaliza wenyewe, kwa sababu wakitoa taarifa polisi hawafiki kwa wakati.

 

Fedha wanazipata wapi

Mwangilingi anasema sehemu kubwa ya fedha zinazotumika katika biashara hizo ni za wafanyabiashara wakubwa wenye maduka wa pale Tunduma, mjini Mbeya na wengine Dar es Salaam ambao huzitoa kwa wamachinga hao na kusubiri tu faida.

Biashara ya aina hii hufanyika pia katika mipaka mingi, lakini kwa Tunduma imeshamiri kiasi cha kusababisha Serikali kufikiria kuwarasimisha wamachinga hao wa fedha ili iweze kukusanya kodi.

Alipoutembelea mpaka huo Januari 13, mwaka huu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji aliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha inaandaa mpango maalumu kwa ajili kudhibiti mapato yanayopotea kutokana na biashara ya ubadilishaji wa fedha kiholela.

Hata hivyo, Meneja wa TRA katika mpaka huo, Jomimasa Nsindo alisema suala hilo la ubadilishaji wa fedha haliko chini ya TRA, bali ni la Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Nsindo alisema walichofanya na kufanikiwa ni kuwazuia wabadilisha fedha wasiingie kwenye eneo la forodha.

“Nadhani umeona mwenyewe, kuanzia pale getini kwenye eneo la forodha hawaingii, sisi tunalo duka moja la kubadilisha fedha ambalo lina leseni ya BoT,” alisema Nsindo.

Nsindo alisema ukiacha suala la leseni inayotolewa na BoT, wafanyabiashara hao wanatakiwa kudhibitiwa na halmashauri ya Mji wa Tunduma.

Akizungumzia hilo, Meya wa Halmashauri hiyo, Ally Mwafongo alisema hakuna sababu ya kuwazuia wafanyabiashara hao wa chenji kwa sababu biashara ya kubadilisha fedha ni ya kawaida dunia kote.

Alisema Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kurasimisha biashara hiyo ya siku nyingi, inayofanywa na watu ambao hata mitaji hawana.

“Endapo watataka kurasimisha, wengi watashindwa kuifanya kwa sababu ya mitaji midogo na mji utazalisha wahuni wengi,” alisema Mwafongo.

Gavana wa BoT, Benno Ndulu alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema utaratibu unajulikana na endapo mtu anataka kufanya biashara ya kibenki au kubadilisha fedha, lazima aufuate kwa sababu uko kisheria.

Alisema katika utaratibu huo, lazima mtu huyo awe na mtaji unaotakiwa kisheria, aelewe fedha amezipata wapi na afunge mashine ya kukokotoa hesabu (EFD).

Wakizungumzia uamuzi huo wa Serikali, wafanyabiashara hao walisema ni uamuzi wa kisiasa unaowalenga wao kwa madai kuwa wanaunga mkono upinzani.

“Wale wanasema sisi tulipigia kura upinzani ndiyo maana wanataka eti tuzuiwe au tufungue ‘bureau de change’, nani anaweza hiyo?” alihoji Madiba.

Alisema unaweza kuona hapa watu wana hela nyingi lakini si za kwao, nyingi zinatoka madukani, lakini walio wengi hawana mtaji mkubwa wa kutoka kuwa duka la kubadili fedha.

“Huyo waziri anayetaka tulipie kodi nataka nimuone anipe hela ya mtaji, Mbona hapa hakushuka alipita kama mwewe,” alisema Hassan Waziri ‘Mwakapinini’.

 

Zambia tofauti

Wakati wafanyabiashara hao wakibeba lundo la noti kwa upande wa Tanzania, ukivuka upande wa pili wa mpaka, Nakonde, huwezi kuona mtu aliyeshika fedha mkononi kwa ajili ya kubadilisha.

Taarifa zilizopatikana ni kuwa nchini humo biashara hiyo inazuiwa na polisi wakiwaona wabadilisha fedha wanawakamata, hivyo wamachinga wa huko wanafanya shughuli hiyo kwa kificho.