DC aeleza changamoto vivuko Kigamboni

Mkuu  wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri wa tatu kutoka kulia akiambatana na kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya hiyo wakitoka kukikagua kivuko cha MV Magogoni.

Muktasari:

  • Kamati ya Ulinzi na Usalama imefanya ziara ya kutembelea vivuko vya Feri na kubaini changamoto tatu zinazovikabili vivuko hivyo na kutishia usalama wa watumiaji.

Dar es Salaam. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam imefanya ziara ya kutembelea vivuko vya Feri na kubaini changamoto tatu zinazovikabili vivuko hivyo.

Changamoto hizo ni kutokuwapo kwa namba za dharura ndani ya kivuko na eneo la kusubiri kivuko, kutofanya kazi kwa runinga zilizopo kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya matumizi ya vivuko na kamera maalumu za kurekodi matukio ya kinachoendelea ndani ya chombo hicho cha usafiri.

Kamati hiyo imefanya ziara leo Jumatano Septemba 26, 2018 ikiongozwa na mwenyekiti wake, Sarah Msafiri ambaye ni mkuu wa wilaya ya Kigamboni.

Akizungumza baada ya kufanya ziara hiyo, Msafiri amesema hajaridhishwa na namna vivuko hivyo vinavyotoa huduma hasa cha MV Magogoni kinachobeba watu 2000 na magari 60.

Amesema vifaa vya uokozi vipo lakini hakuna matangazo wala elimu inayotolewa ya namna ya kuvitumia vitendea kazi hivyo pindi linapotokea tatizo.

"(Temesa) Wakala wa Ufundi na Umeme, msikariri kila kitu badilikeni na usafiri huu ni tofauti na ule wa ardhini. Mfano likitokea tatizo wananchi watapiga kwa namba gani kwa ajili ya msaada na hamna elimu yoyote inayotolewa ya kutumia vifaa vya uokozi," amesema Msafiri.

"Naomba mzifanyie kazi changamoto hizi haraka,  sijafurahishwa na utendaji kazi wenu hapa nawapa wiki moja .Narudia tena lazima mbadilike huu ni usafiri wa tofauti," amesema.

Msafiri amesema lengo la ziara hiyo ni kujiridhisha na utendaji kazi wa vivuko hivyo hasa suala la usalama na uokoaji kwa wananchi.

Pia, amesema hatua ya kufanya ziara hiyo ilikuwapo katika ratiba zake na walianzia kwenye usafiri wa nchi kavu na kumaliza majini.

"Ishu ya kuzama kwa  MV Nyerere imetokea wakati ratiba yangu ya kutembelea vivuko hivi ilikuwapo kama kawaida," amesema.

Kaimu  Mtendaji Mkuu wa Temesa,  Mhandisi Sylvester Simfukwa amesema kazi yao kubwa ni utekelezaji baada ya maagizo hayo kutolewa na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi.

"Suala la usalama wa abiria Temesa tunalipa kipaumbele sana na la muhimu .Tutaendelea kulisimamia na sasa hivi tunaandaa kutekeleza maagizo haya," amesema Mhandisi Simfukwa.