Zuio la wanafunzi wanaopata mimba halihusu shule binafsi, Serikali yafafanua

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imetoa ufafanuzi hatua ya kuzuia wanafunzi wanaopata mimba kurejea shule kuwa suala hilo halizihusu shule binafsi.

Dar es Salaam. Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu hatua ya kuzuia wanafunzi wanaopata mimba kurejea shule kuwa suala hilo halizihusu shule binafsi.

Ufafanuzi huo umetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenda kwa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco) ukiwataka kutofuata maelekezo ya awali yaliyotolewa Agosti Mosi, 2017.

Katika barua ambayo imeandikwa kwa Tamongsco na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuthibitishwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo imezitaka shule binafsi kuwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo kwani zuio hilo haliwahusu wao.

“Ni kweli tumewaandikia barua Tamongsco kwani ufafanuzi huo unatokana na maelekezo ya awali kuwachanganya na yalikuwa hayawahusu wao bali shule za umma,” alisema Dk Akwilapo.

Katibu mkuu huyo alisema badala ya maelekezo hayo kuyatuma kwa shule binafsi anuani zikakosewa na kutumwa kwa shule binafsi jambo ambalo limewafanya kuwatumia barua ya ufafanuzi kuwa zuio haliwahusu na wanaweza kuendelea na wanafunzi wanaopata ujauzito na hata Rais Magufuli alisema marufuku hiyo ni kwa shule za umma.

Alipoulizwa kama mwanafunzi atakayekuwa amepata ujauzito katika shule za umma ataruhusiwa kuendelea akihamishiwa shule binafsi, Dk Akwilapo alisema, “Ataruhusiwa na atakwenda kujiunga huko kwa kufuata taratibu ikiwamo kufanyishwa mitihani.”

Julai 22, 2017, Rais Magufuli akiwa Msata wilayani Bagamoyo mkoani Pwani alisema katika muda wote atakaokuwa madarakani hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari atakayepata ujauzito atakayeruhusiwa kuendelea na masomo katika shule za umma.

“Nataka niwaambie, katika utawala wangu hakuna mwanafunzi mwenye mimba atakayerudi shuleni. Yapo mambo mengi ya kufanya, wanaweza kwenda Veta au wakajifunza kushona, maisha yakaendelea,” alisema Rais Magufuli

Mwananchi lilizungumza na mwenyekiti wa Tamongsco, Mrinde Mzava ambaye alisema hajaiona barua hiyo, huku ofisa mtendaji mkuu wa shirikisho la watoaji wa elimu wasiotegemea serikali kusini kwa jangwa la sahara (CIEPSSA), Benjamin Nkonya alisema ameiona na kupongeza uamuzi huo.

“Serikali isiishie kusema tu watakaopata mimba wakiwa huku (shule binafsi) au shule za umma na wakija kwetu tuwapokee, bali itunge sheria ya kuhakikisha atakayempa mimba mwanafunzi amsomeshe kwenye shule binafsi,” alisema Nkonya

Alisema hatua hiyo itawasaidia wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo hasa wanaokuwa shule za umma.