Lema kuzungumzia kutekwa ‘Mo’ Dewji

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Muktasari:

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema kesho Jumanne Oktoba 16, 2018 atazungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la kutekwa kwa ‘Mo’ Dewji

Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema amekamilisha uchunguzi wa sakata la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ na kesho atazungumza.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Oktoba 15, 2018, Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, amesema, “kesho nitazungumza na waandishi kuhusu kutekwa kwa Mo.”

Amesema mkutano huo na waandishi utafanyika makao makuu ya Chadema mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Lema amesema, “Kama nilivyoandika katika Twitter kuwa niko tayari kuzungumza, nimekamilisha uchunguzi wangu.”

Katika Twitter anayoizungumzia Lema aliiandika jana ikisema, “Nafikiri kwa sasa ninaweza kuongea na waandishi wa habari kuhusu kutekwa kwa mfanyabiashara Mo Dewji.”

Familia ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ leo imezungumza na waandishi wa habari kuhusu kutekwa kwa bilionea huyo na kutangaza dau la Sh1 bilioni kwa mtu yeyote atakayewezesha kupatikana kwake.

Akisoma taarifa ya familia mbele ya waandishi wa habari leo Jumatatu jijini Dar es Salaam, Azim Dewji amesema, “yeyote atakayewezesha kupatikana kwa mtoto wetu mpendwa Mohammed atazawadiwa Sh1 bilioni.”

Azim, ambaye amejitambulisha kuwa ni mwanafamilia amesema yeyote atakayetoa taarifa zitakuwa za siri huku akiwaomba Watanzania kuendelea kuwaombea familia hiyo na mtoto wao apatikane akiwa salama.

Soma zaidi.