Majaliwa ataka tathmini ya uchumi nchini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Majaliwa amesema hayo akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.
  • Mbowe amesema kumekuwa na mdororo mkubwa wa uchumi na kupungua kwa mizigo katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na maeneo ya mipaka ya nchi kama Namanga, Silali, Horohoro na Tunduma, akisema imepungua kwa zaidi ya asilimia 60.

Dodoma. Wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema kujua mwenendo wa kiuchumi kunahitaji tathimini, Benki Kuu (BoT) na Ofisi ya Takwimu (NBS) zimetoa tathmini ya hali ya kiuchumi.

 Majaliwa amesema hayo akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

Mbowe amesema kumekuwa na mdororo mkubwa wa uchumi na kupungua kwa mizigo katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na maeneo ya mipaka ya nchi kama Namanga, Silali, Horohoro na Tunduma, akisema imepungua kwa zaidi ya asilimia 60.

“Serikali inalijua hilo? Je, inachukua hatua gani za makusudi kuirekebisha ili uchumi usiporomoke?” alihoji Mbowe.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema:“Kutambua kama uchumi umeshuka au vinginevyo, kunahitaji tathmini ya kutosha kujiridhisha na kupata takwimu sahihi kwenye maeneo uliyoyataja juu ya mwenendo wake miaka iliyopita na hali tuliyonayo sasa ili tujue kiwango cha kushuka na sababu zake,” alisema mtendaji huyo mkuu wa Serikali.

“Kwa sasa kukupa takwimu halisi za kuporomoka au kutoporomoka si rahisi sana. Ila nakuhakikishia Serikali itafanya jitihada zote kuhakikisha uchumi wake unapanda.”

Katika swali la nyongeza, Mbowe amesema suala hilo halihitaji utafiti wa ziada kujua uchumi umeshuka na kwamba BoT ndio taasisi muhimu kwa kuwa hutoa takwimu za ki uchumi  za miezi mitatu.

Hivi karibuni, BoT imetoa takwimu za mwenendo wa kiuchumi, zikionyesha mporomoko kwenye baadhi ya sekta, hasa ya fedha wakati NBS imeonyesha mfumuko wa bei kushuka.

Katika ripoti yake ya Juni, BoT imeonyesha kupungua kwa mikopo iliyotolewa na benki za biashara kwa sekta binafsi kutoka asilimia 21 mpaka 19.1 huku Serikali ikiendelea kutumia kiasi kikubwa kuliko makusanyo yake. Ndani ya muda huo, hifadhi ya chakula ilipungua kutoka tani 63,341 mpaka tani 61,837.

Kupungua kwa mikopo ya sekta binafsi na ile ya biashara, kumeelezwa kuwa kusababishwa na mabadiliko ya sera ya fedha ya Serikali.

Katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali imeanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye miamala yote inayolipiwa, ikiwemo mikopo.

Kuhusu hazina ya chakula, BoT inasema imepungua baada ya kuuzwa kwa idara za Serikali na wafanyabiashara.

Pia mkurugenzi wa sensa na takwimu za jamii wa NBS, Ephrahim Kwesigabo alisema mfumuko wa bei kwa mwezi uliopita ulipungua kutoka asilimia 5.1 mwezi Julai hadi asilimia 4.9.