Friday, August 11, 2017

Profesa Mbarawa ataka madeni yalipwe JNIA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa  

By Cledo Michael, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekutana na wafanyabiashara katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ikiwamo ulipaji wa madeni na kupitia upya malipo ya kodi.

Akizungumza  leo Ijumaa na wafanyabiashara wakiwamo wamiliki wa mashirika ya ndege na watoa huduma, Profesa Mbarawa amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa madeni ya kodi ifikapo mwezi 30 Septemba na vinginevyo wataondolewa.

Amesema ili kuboresha huduma za anga ni muhimu kwa Serikali na wadau kunufaika na biashara hiyo hivyo ni lazima mabadiliko yafanyike kulingana na muda.

"Hatutaweza kuendelea na utaratibu wa zamani, kama tumekupangisha sehemu hii miaka 20 iliyopita na bei bado haijabadilika, hatuwezi kwenda hivyo, "amesema.

Alisema ongezeko la kodi litazingatia aina ya biashara na hali halisi ya soko hivyo kutowakandamiza wadau hao.

Hatahivyo, wafanyabiashara wamekubali kuyapokea mabadiliko ya kodi huku wakihimiza kufanyika maboresho ya huduma ikiwamo umeme, maji, huduma za afya pamoja na mifumo ya kielektroniki.

Pia, wamelalamikia juu ucheleweshwaji huduma kwa  abiria wanaingia nchini(Immigration) kutokana na kuwa na maofisa wachache.

-->