RC Mara awafungua macho wafanyabiashara

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa.

Muktasari:

Dk Mlingwa amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya uhamasishaji kuhusu majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kwa wafanyabiashara na watendaji wa mkoa huo.

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa amewataka wafanyabiashara na watendaji kufanya kazi kwa kufuata misingi ya maadili na kutumia rasirimali zilizopo kukuza uchumi wa mkoa huo.

Dk Mlingwa amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya uhamasishaji kuhusu majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kwa wafanyabiashara na watendaji wa mkoa huo.

Amewataka wafanyabiashara kuzingatia elimu ya kusajili biashara zao ili waweze kukuza uchumi wao na wa Taifa, huku akiwahimiza kuacha tabia ya kuwekeza bila kufuata sheria na kanuni.

Pia, amewahimiza wafanyabiashara wakubwa kuchangamkia fursa za uwekezaji mkoani humo, pamoja kuacha kuzembea huku mikoa jirani ikikimbizana na fursa zinazowazunguka.

“Mkoa wa Mara unamiliki Hifadhi ya Serengeti kwa asilimia 55 na Simiyu asilimia 45, lakini mkoa unaonufaika na hifadhi hiyo ni Arusha kwa sababu wafanyabiashara wa mkoa huo wanajitambua na wanafahamu fursa za kiuchumi, amkeni acheni kulala,” amesema Dk Mlingwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi amesema awali wafanyabiashara walikuwa wakisafiri kutoka mikoani kwa gharama kubwa kwenda Dar es Salaam kusajili biashara na kampuni, lakini kwa sasa usajili unafanyika kwa njia ya mtandao.

Amesema pamoja na kurahisisha, bado wafanyabiashara wengi hawatambui namna ya kutumia mitandao, hivyo wanapita katika mikoa wakitoa elimu hiyo ya kujisajili kupitia mtandao.