Serikali kuhamia Dodoma

Muktasari:

Wakosoaji wamekuwa wakieleza kuwa Serikali haina nia ya dhati ya kuhamisha makao yake kutoka Dar es Salaam kutokana na kuendelea kujenga ofisi zake kwenye mji huo maarufu wa kibiashara, huku Dodoma ikiendelea kuwa na ofisi ndogo za wizara.

Dodoma. Rais John Magufuli ameamua kukamilisha safari iliyoanza miaka 42 iliyopita ya kuhamishia makao makuu ya Serikali mkoani Dodoma kwa kuanza kukarabati Uwanja wa Ndege na kuhamishia sherehe za mashujaa mjini hapa.

Wakosoaji wamekuwa wakieleza kuwa Serikali haina nia ya dhati ya kuhamisha makao yake kutoka Dar es Salaam kutokana na kuendelea kujenga ofisi zake kwenye mji huo maarufu wa kibiashara, huku Dodoma ikiendelea kuwa na ofisi ndogo za wizara.

Wadau wanasema kusita huko kuhamia Dodoma kumekuwa kukisababisha Serikali kuendeshwa kwa gharama kubwa kutokana na shughuli zake kurudufiwa.

Lakini Serikali ya Awamu ya Tano inaonekana kudhamiria kukamilisha safari ya kuhamia kwenye mji huo ulio katikati ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amesema kwenye mkutano wa kitaifa wa amani ulioandaliwa na Jumuiya ya Waislamu wa Ahamadiya mjini hapa kuwa hatua ya kupanua Uwanja wa Ndege wa Dodoma ni sehemu ya Serikali ya Magufuli kuhamia makao makuu.

Amesema Rais Magufuli atazindua awamu ya kwanza ya mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja huo utakaogharimu Sh11.8 bilioni wakati atakapokuja mjini hapa kuhudhuria Mkutano Mkuu wa CCM utakaofanyika Julai 23.

“Hiyo ni miongoni mwa mipango inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuiwezesha kuhamia Dodoma,” amesema Rugimbana. “Rais ameamua kutumia baadhi ya fedha zilizobakia katika mwaka wa fedha uliopita kuufanyia ukarabati uwanja huu.”

Meneja mradi huo, Mhandisi Mbila Mdemu amesema ukarabati utahusisha njia za kuruka na kutua, barabara za viungio na maegesho ya ndege.

“Mwaka 2005 kulifanyika tathmini na usanifu kuona jinsi gani kiwanja hiki kitakavyoboreshwa na kuongezwa urefu wa barabara za kutua na kuruka kwa ndege,” amesema.