MAKALA YA UCHUNGUZI: Simulizi ya mwandishi wa Mwananchi ndani ya lori 4

Muktasari:

Jana, simulizi ya habari hii ya kichunguzi iliisha wakati nikiangalia takwimu za ajali za magari za Tanzania, Zambia na duniani. Kwa mujibu wa takwimu hizo watu wengi wenye umri kati ya miaka 15 na 39 hupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani. Na tayari tumeshaona huko nyuma jinsi wanavyobugia pombe kali wakati wakiwa njiani na sababu za ajali tulizokutana nazo. Leo naendelea na mahojiano na mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga anasema japokuwa madereva wote wanajua sheria na taratibu, kwamba hawatakiwi kuendesha kwa mwendo kasi, wakiwa wamelewa au kunywa pombe wakati wakiwa njiani, bado hawatii sheria.

“Madereva wanajua kwamba madereva wa masafa marefu wanatakiwa kuwa wawili, lakini wanapuuza,” anasema Kamanda Mpinga ambaye niliongea naye baada ya kumaliza uchunguzi wangu.

Kamanda Mpinga anasema kisheria gari linalosafiri zaidi ya kilometa 700 linatakiwa kuwa na madereva wawili, lakini wamiliki wa magari hayo hawafanyi hivyo au wanaweka madereva ambao hawana uzoefu.

Katika safari hii niligundua kuwa Barabara ya Dar-Tunduma ina askari wengi wa usalama barabarani ambao huvaa kiraia na kushika vifaa maalumu vyenye kurekodi mwendo wa gari, kuchukua video ya magari na picha za mnato (madereva huviita tochi), lakini madereva hutumia mbinu kukwepa kunaswa.

Tangu tunaanza safari yetu Mbezi kwa Musuguri, Temba alikuwa akiniambia maeneo yenye tochi na hujiandaa vilivyo kwa kufunga mkanda, kupunguza mwendo na kuficha viroba. Katika safari hii tumekutana na tochi mara 16, ambazo kati ya hizo, tulikamatwa mara nne.

Kila tunapokamatwa dereva huchomoa noti ya Sh5,000 na kuikunja katikati ya nyaraka za gari na kumpa trafiki. Fedha ni sabuni ya roho, huita warembo wakaitika “labeka”, sembuse trafiki!

Baada ya kupewa nyaraka zenye noti katikati, trafiki huanza kukagua gari mbele, kutazama stika za bima, leseni ya gari na mara moja chache kadi ya gari, kisha humrudishia dereva nyaraka zake. Hakuna trafiki anayemkagua dereva kujua amelewa kama ilivyokuwa kwa dereva Temba.

Mbali ya madereva hawa kujua maeneo wanayokaa trafiki, vilevile hupeana ishara njiani ili apunguze mwendo. Mara wanapopita eneo lenye askari wa tochi, huongeza kasi na kufungua mikanda.

“Bado hizi tochi zinakabiliwa na changamoto, lakini kwa sasa tuna mpango wa kutafuta teknolojia ya ‘robot’ au ‘speed radar’ na zitawekwa sehemu ambayo madereva hawatarajii, lakini zitachukua taarifa zote,” anasema Kamishna Mpinga.

Saa 6:10 mchana nachukua bodaboda hadi Tunduma ambako napata chumba kwenye nyumba ya wageni ya Nice Inn iliyoko Mtaa wa Cafcam. Kitu cha kwanza ninachokutana nacho ni biashara ya mkononi ya kubadili fedha za kigeni au umachinga wa fedha za kigeni.

Badala ya kuwa na maduka ya kubadilisha fedha (bureau de change), hapa Tunduma vijana wanashika fedha mkononi na kubadilisha bila wasiwasi.

Huhitaji kuelekezwa mahali waliko, kwa kuwa wanaonekana wazi. Utawabaini kutokana na kiasi kikubwa cha fedha walichonacho mikononi wakionekana kutokuwa na wasiwasi wowote.

Si ajabu kumuona mtu amekamata Sh5 milioni au Sh10 milioni mkononi, akisubiri mteja wa kubadilishana naye kupata fedha za kigeni au kupata za Tanzania.

Ubadilishaji huu wa fedha unaufanya mji huu kuwa na pilikapilika nyingi mbali ya biashara nyingine kama ya maduka, vyakula, matunda na vitu vinginevyo.

Jambo jingine linalosababisha Tunduma pawe mahali penye pilikapilika nyingi ni kwamba hapa ni njiapanda ya kwenda Nakonde nchini Zambia, Sumbawanga mkoani Rukwa na Mpanda mkoani Katavi. Kwa hiyo kuna watu wanaotafuta usafiri ama wa kwenda Zambia au mikoa ya Rukwa na Katavi.

Dereva wa bodaboda aliyenichukua kutoka Mpemba hadi Tunduma anajitambulisha kuwa anaitwa Godigodi. Huyu ndiye mwenyeji wangu wa kwanza. Najitambulisha kwake kuwa naitwa Doreen na kwamba natoka shirika la Women Development Wing Arusha (WDT) ambalo kazi yake ni kuwaondoa wanawake kwenye biashara ya ukahaba.

Namwambia kwamba kabla ya kuwapata, huwa tunafanya uchunguzi wa maeneo, aina ya wanawake na namna biashara ya ukahaba inavyofanyika. Namwomba awe ananisaidia usafiri na kunipeleka maeneo ninayotaka. Baadaye tunapeana namba za simu ili iwe rahisi kumwita kila nikimhitaji.

Baada ya kuachana naye narudi hotelini najifanyia usafi wa nguvu. Napata chakula cha mchana kisha naamua kwenda Nakonde, Zambia. Baada ya kufika mpakani, nabahatika kupata lori linalonichukua hadi Nakonde.

Nakonde hakuna pilipikapilika nyingi. Hata vijana wanaobadilisha fedha hawapo kwa sababu ya utaratibu maalumu wa serikali ya Zambia. Biashara ya kubadilisha fedha haijaachwa ifanyike kiholela. Baada ya kuzunguka Nakonde kwa muda wa saa mbili hivi, nakodi bodaboda nyingine hadi Tunduma.

Tofauti ya maeneo haya mawili ni kwamba moja liko Tanzania na jingine Zambia, lakini watu, hasa makahaba wanasafiri wakati wote bila kizuizi.

Baada ya kurejea Tunduma nampigia simu Godigodi na hapo ndipo kazi inaanza. Katika maongezi, Godigodi ananitajia mitaa maarufu kwa ukahaba. Pia, ananipeleka kunikutanisha na mwanadada mmoja aitwaye Sifa. Huyu ndiye anakuwa mwenyeji wangu wa pili.

Sifa anaishi katika danguro lililopo Mtaa wa Africana.

Ni mwanamke aliyeumbika vizuri ambaye mchana akiwa amevaa rinda lake refu na ametulia mahali, huonekana wa gharama sana lakini hana sifa hiyo usiku. Kama ilivyo kwa wasichana wengine, Sifa hachagui mume na wakati mwingine hajali hata afya yake.

Najitambulisha kwake kuwa naitwa Doreen natokea Arusha na kwamba nimekuja Tunduma kufanya biashara anayofanya yeye hivyo natafuta rafiki wa kunielekeza mitaa. Sifa, mwenye rangi ya maji ya kunde, mwembaba na mrefu ananieleza kuwa yeye anaishi kwenye danguro pamoja na wenzake. Tunazungumza mengi kuhusu mazingira, maisha yake na alivyosafiri kutoka kwao Mwanza hadi Tunduma.

Anasema alitoka Mwanza nyumbani kwao kuja kufanya biashara hiyo kutokana na ugumu wa maisha, ingawa anasema wazazi wake hawajui kama anafanya biashara ya ukahaba.

“Kwa sasa siwezi kukuambia uje kukaa pale kwa sababu mimi pia ni mgeni na nimeletwa na rafiki yangu. Labda baadaye nitakutafutia,” anasema Sifa. Mwenyeji wangu huyu ananipeleka hadi kwenye danguro analoishi. Dangulo hili ni nyumba ya kulala wageni ambayo imekodiwa na makahaba hawa ambao walinidokeza baadaye kuwa hulipia chumba Sh15,000 kwa wiki.

Gesti hii ina vyumba 14, ambavyo wasichana hawa wameweka samani chache kama vitanda na meza ndogo ya vipodozi. Nawakuta wasichana wengine wawili wakiwa chumba Namba 5, mmoja akiwa amelala na mwingine amekaa.

“Ukipata mwanaume, mkaelewana bei, unaingia naye katika chumba chako,” anaeleza Sifa ambaye anakuwa mwalimu wangu.

“Kama umekuja na mteja na mwenzako naye ana mteja, anasubiri mpaka umalize au kama kuna chumba kingine kipo wazi unaweza kuomba. Lakini si wanaume wote wanakubali kutumia vyumba hivi, wengine wanakodi gesti nyingine,” anasema. Tunakubaliana tuonane usiku.

Nikiwa hapa nagundua kuwa wanawake waliopo katika danguro hili, wengi si wenyeji bali hutokea mikoa mingine kwa ajili ya biashara hii.

Lakini pia wananiambia kuwa wanakuja hapa Tunduma kwa kuwa ni eneo lao la kibiashara, lina watu wengi, madereva, wafanyabiashara na wenye fedha. Lakini pia wanasema wanaume wa Nakonde upande wa Zambia, wanapenda wanawake wa Kitanzania.

Inaendelea kesho.