Waishangaa Serikali kujitokeza matibabu ya Lissu wakati huu

Muktasari:

  • Wamehoji sababu ya Serikali kuibuka sasa wakati ilipaswa kuwajibika tangu awali kwa kuwa mbunge huyo alikumbwa na tukio la dharura ambalo lilipaswa kushughulikiwa kwa haraka.

Kauli ya Serikali kwamba iko tayari kugharimia matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu popote pale, imeibua mjadala mzito huku baadhi ya wasomi wakidai ni ya kujikosha baada ya kushindwa kuwajibika tangu kiongozi huyo aliposhambuliwa.

Wamehoji sababu ya Serikali kuibuka sasa wakati ilipaswa kuwajibika tangu awali kwa kuwa mbunge huyo alikumbwa na tukio la dharura ambalo lilipaswa kushughulikiwa kwa haraka.

“Sijui mantiki yake ni nini...tunashangaa wakati wote huo ilikuwa wapi na sijui huo uamuzi waliochukua ni wa dhati au inaona haya mbele ya jamii,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha.

Msomi huyo alisema kwa namna yoyote ile, kulikuwa hakuna haja ya kusubiri kufuata taratibu ili kufanikisha matibabu ya Lissu kwani jambo hilo lilipaswa kupewa kipaumbele ni kuokoa maisha yake kwanza na kwa maana hiyo uamuzi wa kumpeleka Nairobi ulikuwa sahihi.

Alisema Lissu ni mtu anayefahamika nchini hivyo Serikali ilipaswa kuzingatia ushauri uliotolewa na Chadema kuokoa maisha yake. “Tunashangaa Serikali inakuja sasa kutaka kutoa msaada... walichofanya Chadema ni kuangalia usalama wa maisha yake kwanza na ndiyo jambo la msingi kwa mtu anapopatwa na tatizo la dharura,” alisema.

Kadhalika, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alionyesha kushangazwa na kitendo cha Serikali kuchelewa kuwajibika kwa haraka katika tukio la Lissu.

Alisema maelezo yaliyotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu matibabu ya mbunge huyo yalizidi kuchanganya zaidi badala ya kutoa mwanga uliotarajiwa.

Katika maelezo yake kuhusu utaratibu wa matibabu ya wabunge, Spika Ndugai alisema anapaswa kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbuli na hali yake ikizidi kuwa mbaya anapelekwa Hospitali ya Apollo, India na si vinginevyo.

Spika Ndugai alilazimika kutoa maelezo hayo baada ya uongozi wa Chadema kukataa Lissu kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikidai kwamba ni kwa kuhofia usalama wake.

Dk Mbunda alisema Lissu alikuwa katika hali tete na kwa maana hiyo hatua zilizopaswa kuchukuliwa ni kuangalia njia zinazoweza kusaidia kuokoa maisha yake na siyo kuweka msaada wenye masharti.

“Serikali ilipaswa kulishughulikia vyema suala hili tena hasa kwa kuzingatia kuwa mwenyewe Lissu amekuwa akiituhumu kuwa inamfuatilia, sasa ingechukua fursa hii haraka ili kujisafisha,” alisema.

Alisema Lissu licha ya kuwa mwanasiasa mashuhuri lakini pia ni mbunge na kiongozi ndani ya Bunge, hivyo kwa namna yoyote ile Serikali ilikuwa na wajibu wa kuchukua hatua za kuokoa maisha yake kwa kukubaliana na hoja za familia na chama chake.

“Hakuna gharama inayofanana na uhai wa mtu... hakuna kabisa. Huyu mtu kashambuliwa tena kwa kupigwa risasi nyingi unataka nini kifanyike zaidi ya kwanza kuchukua hatua za haraka kunusuru maisha yake?”

Msomi mwingine, Profesa Abdul Sherrif alishangaa kuona suala la matibabu ya Lissu kugubikwa na hisia za kisiasa.

“Huyu ni binadamu anapaswa kwanza kuangaliwa afya yake, lakini watu badala ya kushughulikia matibabu yake wanaingiza mambo ya siasa... siyo jambo nzuri hata kidogo,” alisema.

“Hili suala watu wanaliendesha vibaya kabisa wala hawaangalii tena haki za binadamu wanalibeba kisiasa zaidi,” alisema.