UCHAMBUZI: Afrika Mashariki ijipange kufuzu Afcon 2021

Monday November 25 2019

 

Kuanzia Novemba 13 hadi 19 kulichezwa mechi za raundi mbili za mashindano ya awali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) ambayo fainali zake zitafanyika Cameroon mwaka 2021.

Baadhi ya timu zimetumia vyema mechi hizo kukusanya pointi zote sita ambazo zinaziweka timu hizo katika nafasi nzuri kwenye makundi yao.

Mataifa hayo ni Nigeria, Ghana, Tunisia, Madagascar, Algeria na Senegal ambayo yanaongoza makundi yao ya kusaka tiketi za kucheza fainali hizo ambazo zinashirikisha timu 24.

Hata hivyo, wakati mambo yakizinyookea timu hizo, hali si ya kuridhisha kwa timu zinazotoka ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kushindwa kuvuna pointi zote.

Wakati mataifa kutoka kanda nyingine yakianza vizuri na kukamata usukani wa makundi yao, hali imekuwa tofauti kwa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ambazo zimeanza kwa mwendo wa kusuasua kila timu kwenye kundi lake.

Burundi, ambayo ilishiriki fainali zilizopita za Afcon zilizofanyika Misri ikiwa ni mara yake ya kwanza, imejikuta mkiani mwa Kundi E baada ya kupoteza mechi zake mbili za kwanza ilizocheza dhidi ya Afrika ya Kati na Morocco.

Advertisement

Majirani zao wa Rwanda waliopo Kundi F, nao walifuata nyayo baada ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Msumbiji ilipofungwa mabao 2-0 na baadaye wakashindwa kujiuliza nyumbani ambako walipokea kichapo cha bao 1-0.

Tanzania, licha ya kuanza vyema kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea ya Ikweta, ilipoteza mechi iliyofuata dhidi ya Libya kwa kuchapwa mabao 2-1 na hivyo kushushwa hadi nafasi ya tatu ya kundi lake.

Katika hali ya kushangaza, Kenya baada ya kupata pointi moja ugenini dhidi ya vigogo Misri, ililazimishwa sare na Togo nyumbani katika mchezo wa pili, matokeo ambayo yaliifanya iangukie katika nafasi ya pili ya Kundi G ikiwa na pointi mbili.

Kwa hesabu na tathmini ya michezo ya raundi hizo za awali ilivyokuwa ni wazi kwamba angalau Uganda ndio wenye nafasi kubwa ya kwenda Cameroon baada ya kukamata usukani wa Kundi B wakiwa na pointi nne. Pointi hizo walizipata kwa kulazimisha sare ya ugenini dhidi ya timu ngumu ya Burkina Faso ambayo ndiyo inayoonekana mpinzani wao mkuu katika kundi hilo.

Hali hiyo, inatoa taswira kuwa kama timu za ukanda wa mashariki mwa Afrika hazitakaza buti katika mechi zilizosalia, unaweza kuwa na timu moja tu au ukakosa mwakilishi katika fainali zijazo za Afcon tofauti na awamu iliyopita nchini Misri.

Ikumbukwe kwamba katika fainali zilizofanyika Misri mwaka huu, timu nne za Uganda, Kenya, Burundi na Tanzania zilipata nafasi ya kushiriki mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili, ingawa hakuna hata moja iliyoweza kufika hatua ya robo fainali.

Kutokana na kundi kubwa la timu hizi kutokuwa na historia nzuri ya kushiriki Afcon, ilipaswa zitumie vizuri mashindano haya ya kuwania pointi katika mechi za mwanzoni ili zijiweke katika nafasi nzuri ya kwenda Cameroon, jambo ambalo litakuwa ni muendelezo wa kile ambacho tayari walishakianza katika fainali za mwaka huu.

Timu za ukanda huu zilipaswa kuondoa unyonge ambao zimekuwa nao kwa kupata matokeo mazuri katika harakati hizi za kuwania kufuzu.

Hata hivyo, hilo limekuwa kinyume na inaonekana kama bado mataifa mengi ya ukanda wetu yapo usingizini na hayajatambua kwamba baada ya kushtusha kwa ukanda huu kupeleka idadi kubwa ya timu kule Misri, mataifa mengi yanazitazama timu za ukanda huu kwa jicho la tatu na yanajiandaa vizuri kukabiliana nazo yakiamini kwamba sio nyepesi na zenye viwango vya wastani.

Kutokana na hilo, matokeo ya mechi za raundi mbili za mwanzo, yanapaswa kuziamsha timu zetu na yanapaswa kuwa chachu ya kuzifanya zijiandae na kujipanga maradufu ili ziweze kurekebisha hali ya hewa kwa kupata matokeo mazuri katika mechi zinazofuata na kujihakikishia tiketi ya kushiriki Afcon.

Vinginevyo tunaweza kujikuta tunapiga hatua nyingi nyuma na kushindwa kukiendeleza kile ambacho tulikianza mwaka huu kwa kuingiza idadi kubwa ya timu katika fainali zilizofanyika Misri mwaka huu.