Wadau walia na kuporomoka ufaulu wa somo LA Hisabati nchini
Muktasari:
- Maadhimisho hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati somo hilo likitajwa kugubikwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya wanafunzi wengi kufeli.
- Changamoto zinazolikabili somo hilo ndizo zilizowafanya wataalamu wa Hisabati kutenga siku moja ili kutafakari, kutathmini na kuweka mikakati ya pamoja namna ya kukabiliana nazo.
‘Hisabati kwa maendeleo ya viwanda’ ndiyo kauli mbiu iliyobeba maadhimisho ya Siku ya Pai Duniani, maarufu kwa jina la Siku ya Hisabati.
Maadhimisho hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati somo hilo likitajwa kugubikwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya wanafunzi wengi kufeli.
Changamoto zinazolikabili somo hilo ndizo zilizowafanya wataalamu wa Hisabati kutenga siku moja ili kutafakari, kutathmini na kuweka mikakati ya pamoja namna ya kukabiliana nazo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA), Dk Said Sima anakiri kuwa somo hilo lipo taabani.
Anasema wameamua kuikumbusha Serikali na umma kuwa hisabati ni somo muhimu, na haliwezi kukwepeka kwenye maisha ya kila siku ya binadamu.
“Ni somo linaloyazunguka maisha yetu, hatutaweza kuifikia Tanzania ya viwanda bila kuwa na mikakati ya kuinua ufaulu wa hisabati,” anasema na kuongeza kuwa somo hilo ni muhimu kwa kuwa hakuna Tanzania ya viwanda bila hesabu.
Hisabati taabani
Dk Sima anasema ufaulu mdogo wa somo hilo umekuwa ni kilio cha muda mrefu ambacho kimeonekana kukosa mwenye kukishughulikia kwa dhati.
Takwimu zinaonyesha kuwa wastani wa ufaulu katika miaka 9 iliyopita tangu 2008 hadi 2016, katika mtihani wa hisabati wa kitaifa kwa shule za msingi ni asilimia 31.86 na sekondari kidato cha nne ni 17.46.
“Kwa mfano, ufaulu wa hisabati kwa kidato cha nne mwaka 2015 ni asilimia 16.76 na 2016 ni 18.12 ambao ni chini kabisa japo kuna ongezeko la asilimia 1.36,” anasema.
Anasema kwa ujumla ufaulu mdogo unachangiwa na mambo mengi ambapo inatakiwa utafiti wa kisayansi kubainisha visababishi hivyo.
Hata hivyo anasema takwimu za ufaulu miaka ya nyuma zilikuwa si mbaya ikilinganishwa na kadiri miaka inavyosogea.
Akitoa mfano anasema kidato cha nne kutoka mwaka 1972 hadi 1976 wastani ilikuwa ni 39.22 ikiongozwa na ufaulu wa asilimia 52.7 mwaka 1975.
“Miaka ya 1993–1997 wastani wa ufaulu ilikuwa ni asilimia 24.76, hivyo kwa kidato cha nne inaonyesha ni jinsi gani ufaulu ulivyokuwa unashuka pamoja na ubora wake,” anasema.
Anasisitiza kuwa inawezekana kabisa kurudi ufaulu wa miaka ya 1970 ikiwa itawekwa dhamira ya kweli. Moja ya tatizo ambalo liko wazi ni upungufu wa walimu wa somo la hisabati.
Sababu za kusuasua hisabati
Dk Sima anasema kuwa zipo sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa kusuasua kwa somo hilo na kutaja kuwa ni pamoja na uhaba mkubwa wa walimu.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina walimu 24,718 wa masomo ya sayansi ikiwamo hisabati katika shule za sekondari.
Kwa mujibu wa takwimu hizo kutoka kitabu cha takwimu cha elimumsingi mwaka 2016 (BEST), nchi inakabiliwa na upungufu wa walimu 7,291 wa hisabati, 6,873 wa fizikia 5,373 wa kemia na 5,181 biolojia.
Mtaalamu wa somo hilo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sylvesta Rugayamu anasema ukweli ni kwamba hali ya hesabu nchini si shwari.
Anataja sababu nyingine kuwa ni baadhi ya walimu kutoiva vizuri kwenye hisabati na hivyo kuwa vigumu kuwaelewesha watoto wanafunzi.
“Unashangaa mwalimu hajaiva kufundisha hisabati na kwa sababu ya uhaba anapelekwa kufundisha, hapo tegemea kuzalisha wanafunzi wasioelewa kabisa somo hilo,” anasema.
Dk Rugayamu anasema ukweli ni kwamba, msingi wa hisabati lazima ujengwe tangu mwanafunzi anapokuwa shule ya msingi.
Anasema sababu nyingine inayozorotesha hisabati nchini ni idadi ndogo ya vyumba vya madarasa inayosababisha wanafunzi wengi kubanana.
“Hakuna mwalimu anayeweza kuwafundisha wanafunzi waliorundikana kwenye darasa moja na kuwawezesha kufaulu hisabati, ni lazima Serikali iwekeze kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa,”anasema.
Anasisitiza kuwa si rahisi kuifikia Tanzania ya viwanda ikiwa somo la hisabati halitapewa kipaumbele. Anaamini msingi mzuri wa kujifunza somo hilo lazima uanzie shule za msingi.
Pia anasema mtindo wa maswali ya hisabati kutungwa kwa mfumo wa kuchagua jibu sahihi, unachangia kwa kiasi kikubwa kuangamiza somo hilo.
Zana za kufundishia
Mwalimu mstaafu wa hisabati, Mohamed Kimaya anasema wanafunzi wengi wanachukia hesabu kwa sababu halifundishwi kimvuto.
“Walimu wanafundisha hesabu bila kuwa na zana zozote za kufundishia, somo hili halifundishwi kwa mvuto kama utaalamu wa matumizi sahihi ya zana ungekuwepo kwenye shule zote, watoto wangefaulu na hakuna ambaye angechukia,”anasema.
Anasema kiuhalisia, inatakiwa zana za kufundishia hesabu ziwekwe kwenye kila darasa na kuachwa darasani, ili wanafunzi waendelee kuzizoea na kuzitumia.
Dk Sima anasema kutotumia zana za kufundishia ni kati ya changamoto zinazolikabili somo hilo.
“Tunapaswa kutilia mkazo katika kutumia zana katika ufundishaji na ujifunzaji wa hisabati kwa sababu unapotumia zana hizi inamsadia sana mwanafunzi kuelewa na kuipenda hisabati,” anasema.
Anasema chama hicho kitazidi kutilia mkazo utumiaji wa zana hizo, ili kila mwalimu wa hesabu nchini aweze kutumia.
Dhana kuwa somo ni gumu
Baadhi ya wanafunzi wanasema dhana kwamba hisabati ni ngumu imekuwa chanzo kikubwa kwa wengi wao kufeli.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Majani ya Chai, Dar es Salaam, Johary Zedy anasema ukweli ni kwamba hisabati si somo gumu.
“Hisabati ni somo rahisi kuliko yote, lakini wanafunzi wengi wanalichukia kwa sababu halifundishwi kwa mvuto. Hesabu ni kati ya masomo matamu, na hakuna binadamu anayeweza kulikwepa kwenye maisha ya kila siku,” anasema.
Nini kifanyike?
Chama cha Hisabati Tanzania kinashauri kuwa ifanyike tathmini ya walimu wa somo hilo waliostaafu, wenye uwezo na kisha waweze kupewa ajira za mkataba za kufundisha shule zilizo karibu na maeneo wanayoishi.
Dk Sima anasema lazima Serikali iajiri walimu waliohitimu vyuo mapema wanapomaliza badala ya kusubiri muda mrefu, kwa madai kuwa wakiachwa watapata kazi kwenye sekta nyingine, wakati hisabati inahitaji walimu.
Mkakati wa Serikali
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu, anasema ipo mikakati mingi ya Serikali katika kuboresha elimu, ikiwamo kuyapa kipaumbembele masomo ya sayansi.
“Changamoto zilizotajwa zinaendelea kushughulikiwa ili kukuza ufaulu wa masomo haya ikiwamo somo la hisabati,”anasema.