MAONI YA MHARIRI: Watanzania wailinde amani yao

Wednesday August 24 2016
BONGO

Tanzania imekuwa ikionekana kuwa miongoni mwa nchi zenye amani pengine kuliko nchi yoyote ya Afrika na dunia kwa ujumla, tofauti na nchi nyingine nyingi ambazo zinakabiliwa na machafuko ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Amani na utengamano ambao Watanzania wameufaidi tangu walipopapata Uhuru mwaka 1961, si vitu ambavyo vilikuja tu, ila ni kutokana na utamaduni waliojijengea wenyewe, utamaduni wa kuheshimiana na kuvumiliana miongoni mwao bila kujali tofauti zao za makabila, dini na itikadi za kisiasa.

Tangu kuanzishwa tena kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992, tumekuwa tukishuhudia siasa za ushindani mkali huku kila upande ukijaribu kuvuta wafuasi na kunadi sera za chama chao. Ni kipindi hiki ambacho tumeshuhudia hata viongozi walio madarakani wakihojiwa kuhusu utendaji wao, tofauti na hali ilivyokuwa enzi za chama kimoja.

Hata hivyo, ushindani wa kisiasa uliopo nchini usichukuliwe kama jukwaa la kueneza uadui na vitisho ambavyo vinahatarisha amani ambayo tumekuwa tukiifaidi miaka yote.

Tunatoa ujumbe huu kwa wote ambao wapo madarakani; viongozi wa serikali na wa vyama vya upinzani. Tunasema haya kwa sababu nchi yetu sasa ipo katika wasiwasi mkubwa huku zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Septemba Mosi, siku ambayo Chadema wametangaza kufanya operesheni wanayoiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).

Kwa mujibu wa uongozi wa Chadema, utawala wa Awamu ya Tano unaendesha nchi kimabavu, hali ambayo chama hicho kimedai inawafanya wapinzani kunyimwa uhuru na haki ya kufanya mikutano ya kutangaza sera na ajenda zao.

Advertisement

Lakini, Serikali kwa upande wake imekuwa ikisisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu ulimalizika Oktoba mwaka jana, hivyo Watanzania wanatakiwa kurejea katika kazi zao za kawaida za maendeleo badala ya kupiga siasa.

Wapinzani, kwa upande wao, wanaamini kwamba siasa na maendeleo haviwezi kutenganishwa—kufanya hivyo ni sawa na udikiteta.

Mambo ambayo tumekuwa tukiyaona na kuyasikia ndio ambayo yanatufanya tuone haja ya kuzionya pande zote mbili zinazoshindana kisiasa, huku tukisisitiza kuwa wanapaswa kujua kuwa hofu imetanda miongoni mwa wananchi.

Hii ni kwa sababu, uongozi wa Chadema unasisitiza kuwa mpango wa Ukuta si wa chama hicho tu. Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amekuwa akisema kuwa vyama vingine vya upinzani ambavyo vilikuwa na mgombea mmoja kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, yaani Ukawa, vitashiriki katika operesheni hii.

Wakati huohuo, nchi imekuwa ikishuhudia vikosi vya Jeshi la Polisi vikifanya mazoezi katika mikoa mbalimbali, jambo ambalo limewafanya wanaoshuhudia kusema kuwa vikosi hivyo vinaonyesha nguvu yao, ikiwa namna ya kutoa onyo na vitisho kwa watakaoungana na Chadema katika maandamano hayo.

Kwa mtazamo wetu, yote haya hayana faida kwa Tanzania, na ni vitendo vinavyowapa hisia wapenda amani kuwa Taifa letu linaelekea kwenye machafuko. Tungependa kuwa wazi kabisa kuwa hali hii haiwezi kuupa ushindi upande wowote. Pande zote zitashindwa.

Hata katika mambo tunayoyaona sasa kutoka kwa pande zote mbili, ni kuwa nguvu nyingi na raslimali chache tulizo nazo zinatumika kwa ajili ya maandalizi ya mapambano ambayo hayapaswi kuwepo kabisa.

Ni matumaini yetu kuwa viongozi wetu wa kisiasa, dini, vyama vya kiraia na asasi za kijamii, wataona umuhimu wa kuziweka pande hizi pamoja na kuhakikisha kuwa hakuna anayehatarisha amani na usalama wa nchi yetu.

Advertisement