Homa mpya Simba, Yanga

Saturday August 31 2019
homa pic

Msimu mpya wa Ligi Kuu ya Bara ulioanza wiki iliyopita umekuja na homa mpya inayopasua vichwa Simba na Yanga kutokana na viwango vinavyotia shaka vya safu za ushambuliaji za miamba hao wa soka nchini.

Yanga ilianza ligi kwa kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ruvu Shooting wakati Simba iliifunga JKT Tanzania mabao 3-1.

Katika mechi hizo safu za ushambuliaji za timu zote mbili zilianza kwa kusuasua na hivyo kuibua maswali kwa mashabiki.

Yanga iliwaanzisha wachezaji wanne wa kigeni wa nafasi za ushambuliaji katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao ni Juma Balinya, David Molinga, Sadney Khoetage na Patrick Sibomana, lakini wote walishindwa kutumbukiza mpira wavuni.

Washambuliaji hao walipata nafasi tisa za kufunga, lakini walishindwa kupata bao hata moja kutokana na kukosa umakini na utulivu wa kutumia nafasi nzuri wanazopata katika lango la wapinzani wao.

Timu hiyo iliyo na viungo wengi wazuri kama Mapinduzi Balama, Mohammed Issa Banka na Feisal Salum ‘Fei Toto’, imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini safu ya ushambuliaji imekuwa butu.

Advertisement

Jambo hilo limewafanya mashabiki wa Yanga, mapema tu kumkumbuka aliyekuwa mshambuliaji wao msimu uliopita Heritier Makambo ambaye ametimkia katika klabu ya Horoya AC ya Guinea. Msimu uliopita Makambo aliifungia Yanga mabao 17 na kushika nafasi ya tatu kwenye wafugaji bora wa Ligi Kuu.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema: “Yanga itahangaika sana kwenye safu ya ushambuliaji msimu huu kwani wachezaji karibu wote wa eneo hilo ni wageni hivyo hadi wakae sawa itachukua muda.

“Nafikiri halikuwa jambo sahihi kwao kumuachia Makambo akaondoka kwani ndiye alikuwa mfungaji wao bora msimu uliopita, lakini pia alikuwa anajua mbinu za kuwatoka wapinzani na kufunga mabao kutokea katika eneo lolote lile,” alisema Mwaisabula.

Kwa upande wa Simba licha ya kuanza ligi kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Tanzania, lakini safu ya ushambuliaji ya timu hiyo nayo imeonekana haiko vizuri.

Majeraha ya John Bocco yamesababisha Meddie Kagere ‘MK14’, kucheza peke yake kama mshambuliaji halisi hivyo kulazimika kocha Patrick Aussems kuwachezesha viungo Clatous Chama, Hassan Dilunga ‘HD’ kucheza kama washambuliaji huku pengo la Emmanuel Okwi halijazibwa.

Licha ya kwamba Kagere alifunga mabao mawili katika mchezo huo lakini alikosa mabao mengi pia pamoja na wenzake jambo ambalo lilimkasirisha kocha Mbelgiji Patrick Aussems ambaye alikiri kuwa walistahili kushinda mabao mengi, lakini wachezaji wake walikuwa wakicheza kama watoto.

“Tulistahili kushinda zaidi ya mabao matano lakini wachezaji wangu kule mbele walikuwa wakicheza kama watoto. Tumetengeneza nafasi nyingi, lakini hatukuzitumia, wachezaji wangu walijiachia sana,” alisema Aussems.

Rekodi Ruvu Shooting

Msimu huu wa Ligi Kuu umekuja na neema kwa Ruvu Shooting kwani kwa mara ya kwanza imepata ushindi dhidi ya Yanga.

Katika michezo 18 ambayo timu hizo zilikuwa zimekutana tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu Bara kabla ya mechi yao ya Jumatano, Yanga iliifunga Ruvu Shooting mara 15 na timu hizo kutoka sare mara tatu, hivyo ushindi wa bao 1-0 ilioupata katikati ya wiki ni rekodi mpya kwa Shooting.

Lipuli yashangaza

Moja ya timu ambayo wengi walidhani ingeanza vibaya Ligi Kuu msimu huu ni Lipuli kwa jinsi ilivyokuwa ikisuasua katika usajili wake.

Lipuli iliondokewa kocha mkuu Seleman Matola aliyejiunga na Polisi Tanzania pamoja na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza kama Beki Ally Mtoni Sonso aliyejiunga na Yanga, Paul Ngalema (Namungo) Willium Lucian ‘Gallas’ (Polisi Tanzania), Miraji Athuman (Simba), Mussa Chibwabwa (Mwadui) na Ibrahim Job na aliyejiunga na Gwambina.

Kuondoka kwa wachezaji hao kikosini kulionekana kama kungeipunguza nguvu Lipuli kwani hata usajili wao ulikwenda taratibu.

Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa, timu hiyo imeanza ligi kwa kishindo kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1.

Hakuna kadi nyekundu.

Msimu huu Ligi Kuu imeanza bila kadi nyekundu tofauti na msimu uliopita ambapo wachezaji wawili walipewa kadi nyekundu katika mechi za kwanza za ligi.

Msimu uliopita mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu alikuwa ni Cliff Buyoya wa KMC katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania na saa chache baadaye beki Ramadhan Malima wa Mbeya City akaonyesha kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Azam FC.

Advertisement