Luis kufanya yake Simba ikicheza na Biashara

Friday February 21 2020

 

By CHARITY JAMES

RAHA ya mashabiki wa Simba kutoka kwa kiungo wao mpya ambaye alionyesha uwezo  mkubwa kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Luis Miquissone inatarajia kuendelea leo Jumamosi dhidi ya Biashara uwanja wa Taifa.
Luis raia wa Msumbiji amejiunga  Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo amecheza mechi tatu hadi sasa akianzia kikosi cha kwanza dhidi ya JKT Tanzania timu yake ikiambulia kichapo cha bao 1-0, alipewa nafasi tena dhidi ya Mtibwa Sugar  walishinda bao 4-0 na kushinda dhidi ya Kagera Suga bao 1-0.
Kwenye mchezo huo Luis alionyesha kuanza kulisoma soka la Bongo kutokana na kufanya kitu kikubwa zaidi ambacho kimezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii huku timu yake ikitarajia kushuka dimbani kumenyana na Biashara United inayoshika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi wakati Simba ipo kileleni kwa pointi 59.
Mbali na mechi hiyo, mechi nyingine zitakazochezwa kesho Azam watakuwa ugenini dhidi ya Namungo mchezo unaonekana kuwa mgumu ambapo mechi ya awali Azam ilishinda bao 2-1 uwanja wa Chamazi kabla haujafungwa.
Kwenye msimamo wa ligi, timu hizo hazipo nafasi mbaya kwani Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 45 huku Namungo wenyewe wapo nafasi ya tatu imekusanya pointi 40.
Mbao wenyewe watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Mwadui FC ambapo timu zote zipo kwenye hatari ya kushuka daraja, mechi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 wakati kwenye msimamo, Mbao inashika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 22 huku Mwadui wapo nafasi ya 19 na pointi zao 19.

Advertisement