Breaking News

Simba, Yanga zaizidi kete TP Mazembe

Thursday April 16 2020

 

By Charles Abel

WAKATI TP Mazembe ikizipiga bao Simba na Yanga kwa mafanikio ya uwanjani na uwekezaji, timu hiyo imeachwa kwenye mataa na klabu hizo mbili kongwe Tanzania kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya African Football Digital Benchmark, TP Mazembe inashika nafasi ya 20 katika chati ya klabu 50 zenye idadi kubwa ya wafuasi katika mitandao ya kijamii ikizidiwa na klabu tatu za Tanzania ambazo ni Simba, Azam na Yanga.
Mabingwa hao mara tano wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika wana jumla ya wafuasi takribani 655,000 katika mitandao ya kijamii ambapo Facebook wana wafuasi takribani 452,000, wafuasi 28,000 katika Instagram, twitter wana wafuasi 155,000 wakati You Tube wanao takribani 18,000.
Simba ambayo msimu uliopita ilitolewa na TP Mazembe hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ina wafuasi takribani mara mbili ya wale wa timu hiyo ya DR Congo ikiwa nao takribani milioni 2.
Idadi hiyo ya wafuasi milioni 2 sio tu wanaifanya Simba iwe mbele ya TP Mazembe bali pia imekuwa kinara hapa Tanzania, Afrika Mashariki na Kati huku ikishika nafasi ya nane (8) kwa Afrika.

Katika ukurasa wa Facebook, Simba ina wafuasi zaidi ya 619000, ina wafuasi milioni moja mtandao wa Instagram, wafuasi 208,000 Twitter wakati katika You Tube ina wafuasi 24,000.
Azam inayoshika nafasi ya 13 kwa Afrika ikiwa na zaidi ya wafuasi Milioni moja huku ikishika nafasi ya pili ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, yenyewe ina wafuasi 519,000 katika Facebook, wafuasi 426,000 kwenye Instagram, Twitter wana wafuasi 48,000 huku You Tube wakiwa nao 345 tu.
Kwa upande wa Yanga ambayo inashika nafasi ya tatu Afrika Mashariki, kiujumla ina wafuasi 957,000 na yenyewe ina wafuasi 292,000 Facebook, wafuasi 563,000 kwenye Instagram, wafuasi 65,000 Twitter na kwenye You Tube kuna wafuasi 36,000.
Mtibwa ambayo kwa Tanzania iko nafasi ya nne, kwa Afrika Mashariki ikiwa nafasi ya sita na kwa Afrika ikikamata nafasi ya 46, yenyewe Facebook ina jumla ya wafuasi 14,000 tu.
Idadi kubwa ya wafuasi wa Mtibwa Sugar ipo mtandao wa Instagram ambako wanao jumla ya wafuasi zaidi ya 154,000 na Twitter wana wafuasi takribani 15,000.
Kwa Afrika kiujumla, vinara ni al Ahly (Misri) yenye wafuasi zaidi ya milioni 27 wakifuatiwa na Zamalek (Misri) ambayo ina wafuasi milioni 12.
Meneja Utawala na Sheria wa Mtibwa Sugar,Abubakar Swabr alisema klabu yake imeandaa mikakati imara ya kuwafanya wawe na idadi kubwa ya wafuasi mitandaoni ili watumie kama fursa ya kibiashara
"Tunajitahidi kusogeza namba lakini bado tuko nyuma kidogo. Tunajipanga katika uzalishaji na tuna mpango wa kuhamia You Tube.
"Kuna mambo tunayaweka sawa ili tukianza tusiwe watu wa kubabaisha," alisema Swabr

Advertisement