IGP Sirro akabidhi bendera Polisi

Friday August 23 2019

 

By Yohana Challe na Stanslaus Kayombo

MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amewakabidhi Bendera wanamichezo wa jeshi la polisi wanaoelekea Nchini Kenya kwenye Mashindano ya wakuu wa Majeshi la Polisi Ukanda wa Afrika Mashariki ( EAPCCO).
Mashindano hayo yanayoanza Agosti 26 hadi 30 yanafanyika kwa mara ya tatu, mara ya kwanza yalifanyika Uganda mwaka juzi na mwaka jana Tanzania ikawa mwenyeji wa mashindano hayo.
KAfande Sirro alisema wanakwenda kwenye michezo ili kujenga mahusiano mazuri baina ya nchi hizo, hivyo wanamichezo hao wanapaswa kuzingatia nidhamu muda wote wanaokuwa ugenini.
"Watanzania wanataka kuona mnakwenda kufanya nini maana ni watu wa Michezo, hivyo mjitahidi ili kulinyanyua Taifa pamoja na jeshi letu," alisema Sirro.
Michezo watakayokwenda kushindana Watanzania ni pamoja na Soka, Riadha, Judo, Kuvuta Kamba, Darts, Karate Shabaha, Taekwondo na Kriketi.
Msimu uliopita Tanzania iling'ara zaidi kwenye mchezo wa Riadha kwa Mwanariadha Fabiano Nelson kutamba na kuvunja rekodi ya mashindano hayo akitumia dakika 15:45:99 kwenye mbio za mita 5000.

Advertisement