Kagera Sugar yapanga kuiharibia sifa Simba SC

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Kyaruzi alisema msimu huu kama wachezaji wamejipanga ipasavyo kuhakikisha wanafanya vyema na malengo yao hasa ni kunyakuwa ubingwa huo kwa mara ya kwanza.

KAGERA Sugar msimu huu imeanza vyema Ligi Kuu lakini nahodha wake, Erick Kyaruzi amesema msimu huu wamejipanga kama watashindwa kutwaa ubingwa basi angalau washike nafasi ya pili kwenye mashindano hayo.

Kagera Sugar inataka ubingwa ambao pia unapiganiwa na Simba ili kutetea taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

Mpaka sasa Kagera Sugar imecheza mechi tisa, imepoteza mechi moja huku ikikusanya pointi 17 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kyaruzialisema msimu huu kama wachezaji wamejipanga ipasavyo kuhakikisha wanafanya vyema na malengo yao hasa ni kunyakuwa ubingwa huo kwa mara ya kwanza.

“Kwani inashindikana vipi kutwaa ubingwa kikubwa ni kuendelea kupambana kwa kila mchezo kuhakikisha tunapata ushindi na tukikosa, basi tupate pointi moja,” alisema Kyaruzi.

Alisema kilichofanya waanze msimu kwa kufanya vizuri ni ushirikiano kati ya wachezaji, benchi la ufundi na uongozi ambapo utaendelea kupambana ili kuipa mafanikio klabu hiyo.

“Ligi ni ngumu sana tunapambana kwelikweli kila mchezo kwetu ni kama fainali kikubwa tunataka kuipa mafanikio timu, hivyo tutaendelea kujituma na kusikiliza kwa umakini maelekezo ya benchi la ufundi,” alisema Kyaruzi

Nahodha huyo aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuipa ushirikiano kwani inahitaji sapoti yao katika kipindi hiki.