Rais Brazil kumteua mwanae kuwa balozi Marekani kwa sababu ni rafiki wa watoto wa Trump

Friday July 12 2019

 

Brasília, Brazil. Jair Bolsonaro anafikiria kumteua mtoto wake wa kiume, Eduardo kuwa balozi jijini Washington, kiongozi huyo wa Brazil aliweka bayana suala hilo, akisema mtoto huyo mwenye umri wa miaka 35 ni rafiki wa watoto wa Rais wa Marekani, Donald Trump.
Eduardo, ambaye kwa sasa ni mbunge, aliambatana na baba yake wakati wa mkutano binafsi na Trump alipokuwa katika ziara ya kidoplomasia jijini Washington mwezi Machi.
"Kwa mtazamo wangu, anaweza kuwa mtu sahihi na anaweza kuwasilisha ujumbe kwa usahihi jijini Washington," akiongozi huyo wa Brazil mwenye siasa za mrengo wa kulia aliwaambioa waandishi wa habari jijini Brasilia jana Alhamisi.
Lakini uamuzi huo utategemeana na Eduardo, aliongeza. Iwapo atateuliwa, Eduardo atalazimika kujiuzulu ubunge na kuidhinishwa na seneti.
Eduardo, mtoto wa tatu kati ya wanne wa rais wa Brazil, alisema bado hajaambiwa rasmi lakini akaongeza kuwa atakubali uteuzi huo.
"Kama rais ananiamini kwa kazi hiyo, nitakuwa tayari kujiuzulu nafasi yangu ya sasa," alisema.
"Nazungumza Kiingereza, nazungumza kispaniora, nilichaguliwa kwa kura zilizoweka rekodi, ni mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa kimataifa.. Naamini sifa hizi zinanifanya nistahili."
Rais huyo wa Brazil alitangaza kuwa anafikiria kumteua mtoto wake siku moja baada ya Eduardo kufikisha umri wa miaka 35, kiwango cha chini cha umri ambaye Mbrazili anaweza kuteuliwa kufanya kazi ubalozini nje ya nchi.

Advertisement